JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


Serikali, Wadau Waimarisha Mikakati ya Kupunguza Msongamano wa Magari Dar es Salaam

Share This

 


Na Mwandishi Wetu
SERIKALI  kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Shirika la Reli Tanzania (TRC) inaendelea kutekeleza mpango wa kujenga bandari kavu katika maeneo mbalimbali nchini ili kupunguza msongamano mkubwa wa malori jijini Dar es Salaam.

Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Barabara kutoka Wizara ya Uchukuzi, Andrew Magombana, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Godius Kahyarara, wakati wa kufungua Mkutano Mkuu wa Kwanza wa mwaka wa Chama cha Wasafirishaji wa Shehena kwa Barabara Tanzania (TRFA) uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Magombana alisema kuwa miradi ya ujenzi wa bandari kavu mkoani Morogoro pamoja na vituo vya usafirishaji vya Malindi na Bahi inaendelea vizuri. Alieleza kuwa miradi hiyo ikikamilika itawezesha mizigo kuchukuliwa kutoka Morogoro na Dodoma badala ya Dar es Salaam, hatua itakayopunguza msongamano wa magari na kuharakisha usafirishaji wa mizigo kwa wateja.

Aliongeza kuwa Bandari Kavu ya Kwala, ambayo tayari imekamilika, imechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza msongamano wa malori jijini Dar es Salaam kwa kuboresha ufanisi wa ushughulikiaji na usafirishaji wa mizigo. Pia aliipongeza TRFA kwa kushiriki kikamilifu katika utoaji wa huduma za usafirishaji kupitia bandari hiyo, akisema imeongeza ufanisi katika sekta ya lojistiki.

Magombana pia aliisifu TRFA kwa ushirikiano wake na Serikali kupitia majukwaa mbalimbali ya sekta ya uchukuzi na biashara, ikiwemo Kamati ya Maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam ambayo hujadili namna ya kuboresha ufanisi wa bandari na kutatua changamoto za usafirishaji.

Alisisitiza kuwa sekta ya uchukuzi ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania, huku akiielezea Tanzania kuwa lango muhimu la biashara kwa zaidi ya nchi nane za Afrika Mashariki, Kusini na Kati kutokana na nafasi yake ya kimkakati.

Magombana amesema bandari za Tanzania zilihudumia tani milioni 19.9 za shehena kati ya Julai na Desemba 2025. Serikali inatarajia kiasi hicho kuongezeka na kufikia zaidi ya tani milioni 40 ifikapo mwisho wa mwaka wa fedha 2025/26, kutoka tani milioni 32.75 zilizohudumiwa mwaka uliotangulia, na hivyo kuvuka lengo la kuhudumia tani milioni 30 ifikapo mwaka 2030/31.

Aidha, alisema awamu ya kwanza ya Kituo cha Lojistiki cha Kurasini chenye uwezo wa kuhudumia makasha 37,000 imekamilika, na kinatarajiwa kupunguza zaidi msongamano wa malori katika maeneo yanayozunguka Bandari ya Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TRFA, Hussein Ahmad Wandwi, alisema chama hicho kilianzishwa mwaka 2022 na kusajiliwa rasmi Desemba 23, 2022 chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Alisema uanachama umeongezeka kutoka wanachama 15 mwaka 2022/23 hadi zaidi ya wanachama 550 mwaka 2024/25, jambo linaloonyesha imani kubwa ya wadau kwa chama hicho.

Wandwi alieleza kuwa dhamira ya TRFA ni kuwakilisha, kuwawezesha, kuwashauri na kufanya tafiti kwa niaba ya wasafirishaji wa mizigo kwa njia ya barabara nchini.

Aliongeza kuwa chama hicho kinalenga kujenga sekta ya usafirishaji iliyo salama, yenye ufanisi na kuaminika, ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kupunguza gharama za usafirishaji huku kikihimiza uzingatiaji wa kanuni na sheria za Serikali.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad