Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh.Riziki Pembe akikabidhi mfano wa hundi kwa Mshindi wa kwanza katika kipengele cha Riwaya cha Tuzo ya Safal ya Kiswahili ya Fasihi Afrika 2025 , Bw. Salim Hussein Ng’azi huku wageni wengine pamoja na viongozi wa Safal Group wakishuhudia. Hafla hiyo ilifanyika katika Chuo Kikuu Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
WASHINDI wa Tuzo ya Kiswahili ya Safal ya Fasihi ya Afrika wametangazwa leo katika shughuli iliyofana Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Paul Makonda ambaye aliwakilishwa na waziri mwenzake kutoka Zanzibar Mh. Riziki Pembe.
Waziri Makonda, katika hotuba yake, aliipongeza Kampuni ya Safal Group kupitia kampuni zake tanzu-Mabati Rolling Mills ya Kenya na ALAF Limited ya Tanzania kwa kudhamini tuzo hityo kwa miaka 10 sasa.
“Hii ni namna bora ya kukuza lugha ya Kiswahili hapa Tanzania na nchi za nje kama tunavyofahamu Kiswahili kwa sasa kinazungumzwa kote duniani ikiwemo nchi za ng’ambo ambako baadhi ya watanzania wameajiriwa ili wafundishe lugha hii,” alisisitiza.
Aliendelea kusema kuwa serikali itaendelea kutangaza lugha ya Kiswahili na kuhakikisha inatumika ipasavyo huku pia ikiandaa matukio mbalimbali yanayolenga matumizi ya lugha hii.
“Tutaendelea kufanya kazi kwa karibu na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na taasisi zingine zinazohimiza matumizi ya lugha hii ya Kiswahili,” alisema.
Aliwapongeza washindi wa mwaka huu na kuwahimiza kutumia vipaji vyao vya uandishi kujiendeleza na kuhakikisha pia wanajiingizia kipato kwa kuuza machapisho yao duniani kote.
Washindi wa mwaka huu ni:
Riwaya:
1. Salim Hussein Ng’azi (TZ) – Mwanamkasi ndio basi (5000USD)
2. Dickson Damas Mtalaze (TZ) – Shamba la mawe (2500 USD)
Ushairi:
1. Ali Hilal Ali (TZ) – Diwani ya vizikwa ya kale (5000USD)
2. Leonard Barnaba Mtesigwa (TZ) – Rima la miiko la balaa (2500 USD)
Hadithi Fupi:
1. Dominic Maina Oigo (KENYA) Mbunge mtarajiwa na hadithi nyingine (2500 USD)
Mwaka huu miswada 230 kutoka nchi saba ziliwasilishwa kwa majaji.
Afisa Mtendaji Mkuu wa ALAF Limited Bw. Bibhu Nanda alisema kampuni yake imedhamini tuzo hiyo kwa miaka 10 sasa kutokana na umuhimu wa lugha ya Kiswahili na jinsi imeendelea kuwaunganisha sio wakazi wa Afrika Mashariki tu bali watu tofauti duniani.
“Tukiwa tunaadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwa tuzo hii, tunapenda kuwashukuru wabia wetu wote ambao wamesimama na sisi katika kipindi hiki chote kwa lengo la kukuza na kutangaza lugha ya Kiswahili ambayo pamoja na mambo mengine imesaidia katika kurahisisha ufanyaji wa biashara katika ukanda huu,” alisema.
Tuzo ya Kiswahili ya Safal ya Fasihi ya Afrika ilianzishwa mwaka 2014 na Dkt. Lizzy Attree na Dkt. Mukoma wa Ngũgĩ ili kutambua kazi za uandishi katika lugha za Kiafrika sambamba na kuhamasisha kazi za utafsiri kwa lugha adhimu za asili ya Kiafrika.
Tuzo hiyo ambayo kwa mwaka huu inaadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2015, imekuwa ikitolewa kila mwaka isipokuwa mwaka wa 2020, kutokana na kuweko janga la Covid 19 duniani kote.
Akiongelea tuzo hiyo, Dkt. Lizzy Attree amesema kwamba miaka 10 tangu kuanzishwa kwake ni hatua kubwa. Aliongeza, "Tayari tumeshatoa zaidi ya dola 150,000 kwa waandishi zaidi ya 40 mchango ambao umewawezesha kuchapisha zaidi ya vitabu 20. Ni matumaini yetu kuwa lugha zaidi za Kiafrika zitaendelea kutambuliwa kwa njia hii na kwamba kazi hii inaendelea kuikuza fasihi ya Kiswahili duniani".
Kwa upande wake Profesa Mukoma wa Ngũgĩ alielezea kuhusu mfumo wa uchapishaji unaohusiana na fasihi ya Kiswahili kwa kipindi cha mwongo mmoja, mfumo ambao amesema umeunganisha waandishi walioshinda tuzo mbalimbali moja kwa moja na wachapishaji wakiwemo Mkuki na Nyota na Mfuko wa Vitabu vya Ushairi wa Kiafrika (APBF).
Aliongeza, "Tunashukuru uongozi wa kampuni ya Safal, ambayo imetoa mchango mkubwa unaokuza tamaduni za Kiafrika. Tunatoa wito kwa serikali mbalimbali Barani Afrika, kupitia wizara zao za utamaduni kuunda mfumo ikolojia utakaohusisha lugha zote za Kiafrika".
Kwa mwaka huu, jumla ya kazi 230 kutoka mataifa saba ziliwasilishwa kwa ajili ya kuwania tuzo hizo
Akitangaza uamuzi wa Majaji kuhusiana na tuzo hizo, Mwenyekiti wa jopo la majaji wa tuzo kwa mwaka huu, Profesa Rayya Timammy kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi, alisema kuwa ushindani wa Tuzo ya Kiswahili ya Safal ya 2025 ya Fasihi ya Afrika ulikuwa mkubwa sana.
Alisema hali hiyo imesababishwa na idadi kubwa ya mawasilisho yaliyopokelewa kuwa na vipaji vya hali ya juu na kipekee vilivyoonyeshwa na waandishi waliowasilisha kazi zao hizo.
Profesa Timammy aliongeza, "Jopo la majaji lilikabiliwa na changamoto kubwa katika kuchagua washindi kwa sababu ya ubora wa kazi zilizowasilishwa. Bila shaka hii inaonyesha kwamba vipaji vya fasihi vinaendelea kukua na kushamiri kwa kasi ya ajabu".
Munyao Kilolo, Mkurugenzi wa Tuzo hiyo, alisema kwamba ukuaji huo umeendelea kukua kwa kipindi chote cha miaka 10 iliyopita. "Mwanzoni tulikuwa tukipokea mawasilisho chini ya 50 kwa mwaka, sasa hivi wanapokea mamia ya mawasilisho kila mwaka. na chini ya hati 50, na sasa tunapokea hati kwa mamia kila mwaka," alisema.
Kilolo alibainisha zaidi kwamba ukuaji huo umeenda sambamba kukua kwa jumuiya ya waandishi ambao mbali na wazo la uweko wa zawadi pia huwa wanashirikiana katika kukuza fasihi ya kiswahili.
Majaji wengine walioungana na Prof. Rayya Timammy katika kusoma na kuteua machapisho ambayo yatashiriki shindano la tuzo kwa mwaka wa 2025 walikuwa ni pamoja na Dkt. Masoud Mohammed wa Chuo Kikuu cha Zanzibar na aliyewahi kuwa mfanyakazi wa chuo kikuu cha Makerere Prof. Austin Bukenya.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Tuzo hii, Abdilatif Abdalla, aliongeza, “Ni jambo la kufurahisha mno kuona kwamba tangu mashindano yalipoanzishwa mwaka 2015, bado Tuzo hii inaendelea kuwavutia washiriki kutoka nchi mbalimbali na kwa idadi kubwa. Pia kiwango cha ubora wa miswada inayoshindanishwa kinaongezeka kila mwaka, na kwa hivyo kuitajirisha Fasihi ya Kiswahili.”
Mbali na zawadi hizo, machapisho yaliyoshinda pia yatapata fursa ya kuchapishwa kwa Kiswahili na kampuni ya uchapishaji ya Mkuki na Nyota iliyoko nchini Tanzania, ambapo mashairi yaliyoshinda yatatafsiriwa kwa lugha ya Kiingereza na kuchapishwa na Mfuko wa Vitabu vya Ushairi wa Kiafrika (APBF).

.jpeg)



No comments:
Post a Comment