Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
JUMLA ya wananchi 1,940 wamepata huduma za uchunguzi wa macho na ushauri wa kitabibu bila malipo katika Banda la MIXX kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika banda hilo, Mtaalamu wa Macho na Huduma kwa Jamii kutoka Taasisi ya Bilal Muslim, Patrick Martine, alisema huduma hiyo imewezesha wananchi kupimwa afya ya macho na kupatiwa miwani bure kulingana na mahitaji yao.
Alisema kati ya wananchi waliopimwa, watu 41 walibainika kuwa na tatizo la mtoto wa jicho na wataendelea kupatiwa matibabu kupitia Taasisi ya Bilal Muslim.
Martine alisema ushirikiano kati ya MIXX na Taasisi ya Bilal Muslim umewezesha wananchi wengi kupata huduma ambazo kwa kawaida zingehitaji gharama kubwa, huku akiwataka wananchi kutumia fursa hiyo kabla ya maonesho kumalizika.
Aidha, alieleza kuwa baadhi ya changamoto za macho zinazoongezeka kwa sasa zinachangiwa na matumizi ya muda mrefu ya vifaa vya kielektroniki kama televisheni na simu, pamoja na sababu nyingine za kiafya zinazohitaji uchunguzi wa mapema.
Kwa upande wake, Meneja wa Banda la MIXX, Omega Mwakifuna, alisema utoaji wa huduma za macho ni sehemu ya mkakati wa kampuni wa kurudisha kwa jamii kwa kuwasaidia wananchi kupata huduma muhimu za afya bila gharama.
Alisema MIXX itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha wananchi wote watakaotembelea banda hilo na kuhitaji huduma za macho wanapata fursa ya kupimwa na kupatiwa ushauri wa kitaalamu.
Baadhi ya wananchi walionufaika na huduma hiyo wameipongeza MIXX kwa kuwaletea huduma karibu yao.
Mkazi wa Kijichi, Cecilia Kapituka, alisema amepimwa macho na kupatiwa miwani miwili bure, jambo ambalo limemsaidia kupata suluhisho la tatizo lililokuwa likimsumbua kwa muda mrefu.
Naye mkazi wa Mabibo, Daud Bernad, alisema amefurahishwa na huduma hiyo baada ya kupimwa na kupatiwa miwani bila malipo, huku akiwahamasisha wananchi wengine kutembelea Banda la MIXX katika Maonesho ya Sabasaba ili kunufaika na huduma hiyo muhimu.



.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)


No comments:
Post a Comment