JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


TANESCO Yaonesha Teknolojia za Kisasa ya Jumba Janja, Sabasaba

Share This

 

*Yawahamasisha Wananchi Kutumia Umeme kwa Ufanisi na gharama nafuu

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limewahimiza Watanzania kutembelea banda lake katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) ili kujionea teknolojia mbalimbali za kisasa zinazolenga kuboresha matumizi ya umeme kwa usalama, ufanisi na gharama nafuu.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO, Irene Gowele, alisema maonesho ya mwaka huu yamebeba ubunifu unaowawezesha wananchi kujifunza namna teknolojia ya umeme inavyoweza kuboresha maisha yao ya kila siku.

Alisema mbali na shughuli za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme, TANESCO imejikita kuonesha thamani ya matumizi ya umeme katika sekta mbalimbali za maisha na uzalishaji.

Kivutio kikubwa katika banda hilo ni Nyumba Janja (Smart Home), ambayo imewekewa mfumo wa kisasa wa umeme wa kidijitali unaoongeza usalama wa nyumba dhidi ya majanga kama moto, huku ukimruhusu mmiliki kudhibiti vifaa vya umeme akiwa popote duniani kupitia simu ya mkononi.

Gowele alisema mfumo huo humwezesha mtumiaji kuwasha au kuzima vifaa vya umeme kwa njia ya programu maalumu pamoja na kufuatilia kiwango cha umeme kinachotumiwa na kila kifaa, hatua inayosaidia kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na gharama za bili.

Aidha, alisema TANESCO inaendelea kuhamasisha matumizi ya vifaa vinavyotumia umeme kwa ufanisi mkubwa (energy efficient), ambapo nyumba hiyo imewekewa vifaa vinavyotumia kiwango kidogo cha umeme ili kuwaonesha wananchi namna wanavyoweza kupunguza matumizi ya nishati bila kuathiri huduma.

Pia aliwakumbusha wananchi kuhusu mpango wa TANESCO wa kukopesha majiko ya umeme, akisema wanaotembelea banda hilo wanaweza kupata majiko hayo kwa kununua au kwa mkopo kwa kutumia namba ya mita ya umeme pamoja na Namba ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA) kwa ajili ya uhakiki.

Alieleza kuwa majiko hayo yana ufanisi mkubwa na yana uwezo wa kupika chakula cha Kitanzania kwa gharama ya chini ya shilingi 356 za umeme, hivyo kuwa mbadala wa gharama nafuu ukilinganisha na baadhi ya nishati nyingine za kupikia.

Katika maonesho hayo, wananchi pia wanapata fursa ya kujionea kwa teknolojia ya kidijitali miradi mikubwa ya uzalishaji umeme inayotekelezwa na TANESCO, ikiwemo Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere na Mradi wa Umeme wa Jua wa Kishapu mkoani Shinyanga unaozalisha megawati 50.

Vilevile, banda hilo linatoa elimu kuhusu matumizi ya umeme katika sekta ya usafiri kupitia magari, pikipiki na bajaji zinazotumia umeme, huku TANESCO ikisisitiza kuwa Tanzania ina umeme wa kutosha unaoweza kusaidia wananchi kupunguza gharama za usafiri na kuchangia utunzaji wa mazingira kwa kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa.

"TANESCO imekuja ki-smart Sabasaba mwaka huu. Tunawakaribisha wananchi wote kutembelea banda letu wajifunze, wajionee teknolojia hizi na namna zinavyoweza kuboresha maisha yao huku zikipunguza gharama za matumizi ya nishati," alisema Gowele.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad