Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KAMPUNI ya GF Group imeandika historia kwa kutwaa tuzo ya Banda Bora kwa Ujumla katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) kwa mwaka wa pili mfululizo, mafanikio ambayo yameelezwa kuwa ni matokeo ya ubunifu, nidhamu, mshikamano na kujituma kwa wafanyakazi wake.
Akizungumza na Wafanyakazi pamoja na Wadau Mbalimbali Mkurugenzi Mtendaji wa GF Group Imran Karmali amesema tuzo walioipata ni ushindi ulipatikana sio kwa bahati mbaya bali ni matokeo ya uthibitisho wa dhamira ya kampuni ya kuwa kinara katika sekta ya magari na viwanda nchini Tanzania.
Amesema kuwa miaka 19 tangu kuanzishwa kwake GF Group kutoka kuwa na maono ya kawaida hadi kuwa miongoni mwa makundi makubwa ya biashara ya magari nchini, ikiwa inawakilisha chapa mbalimbali za kimataifa, kuunganisha magari hapa nchini, kuwekeza katika maendeleo ya watu, kuzalisha ajira na kuchangia ukuaji wa sekta ya viwanda.
Ilielezwa kuwa kampuni hiyo haijikiti tena katika uuzaji wa magari pekee, bali sasa inaunganisha magari nchini, inaleta teknolojia mpya, inajenga uwezo wa wataalamu wa ndani na kuwekeza katika uzalishaji unaoifanya Tanzania kuwa kitovu cha maendeleo ya sekta ya magari.
Aidha, GF Group imetangaza hatua nyingine muhimu ya kihistoria kwa kuanza kuingiza sokoni bidhaa zinazobeba chapa yake yenyewe ya GF, hatua ambayo inaonyesha uwezo wa kampuni hiyo kutengeneza na kukuza bidhaa za Kitanzania zenye ubora wa kimataifa.
Kwa mujibu wa kampuni hiyo, lengo si kutengeneza magari kwa ajili ya Tanzania pekee, bali kuzalisha bidhaa zinazobuniwa kwa mahitaji ya Afrika, kutengenezwa nchini Tanzania na kuaminiwa katika duniani.
Karmali amesema tuzo hiyo haihusu uzuri wa banda pekee, bali ni ishara ya kutambuliwa kwa ubunifu, weledi, maono na uwezo wa kutekeleza mipango mikubwa kwa mafanikio.
Hata hivyo amesema wafanyakazi wa GF Group walihimizwa kuendelea kuwa mabalozi wa kampuni kwa kuhakikisha kila huduma wanayotoa, kila uamuzi wanaoufanya na kila gari wanalolizalisha linaendelea kujenga sifa ya kampuni hiyo ndani na nje ya Tanzania.
Amesema GF Group katika sekta ya magari duniani inaendelea kubadilika kutokana na ujio wa magari ya umeme na teknolojia za kidijitali, hivyo kampuni imejipanga kuwa sehemu ya kuunda mustakabali huo badala ya kuusubiri.
Uongozi huo ulisisitiza kuwa ushindi wa mwaka huu ni hatua moja tu katika safari ndefu ya kujenga kampuni ya Kitanzania inayoweza kushindana na kampuni bora barani Afrika kwa ubora wa bidhaa, ubunifu, uadilifu, uzalishaji wa kisasa na uwezo wa kuunda fursa kwa Watanzania.
Karmali amesema wafanyakazi wote wana mchango wao katika mafanikio hayo huku akiahidi kuendelea kuinua viwango vya utendaji na kuacha urithi utakaowanufaisha vizazi vijavyo.


.jpeg)



No comments:
Post a Comment