JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


TTCL Yaimarisha Huduma za Kidijitali, Yaahidi Kuendeleza Uwekezaji katika Teknolojia za Kisasa

Share This

 




Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limesema litaendelea kuimarisha huduma za mawasiliano nchini kwa kuendeleza matumizi ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, kupanua huduma za kidijitali na kuwekeza katika teknolojia za kisasa ili kuongeza mchango wake katika ukuaji wa uchumi wa kidijitali.

Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Moremi Marwa, amesema mafanikio yanayoendelea kupatikana ndani ya shirika hilo yametokana na maboresho ya kiutendaji na kibiashara yaliyofanyika katika kipindi cha hivi karibuni, hatua ambayo imewezesha TTCL kuongeza mapato, kupata faida na kuboresha huduma kwa wananchi.

Akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Marwa alisema TTCL imeutumia mkutano huo kama jukwaa la kuonesha teknolojia na huduma mbalimbali zinazochochea maendeleo ya uchumi wa kidijitali kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

Alisema miongoni mwa huduma zinazotolewa ni intaneti ya kasi ya juu ya Supersonic Speed, kituo cha FTTX Experience Center kinachowawezesha wananchi kujionea matumizi ya teknolojia ya nyumba janja (Smart Home), pamoja na huduma za Cloud Computing kupitia Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data (National ICT Data Centre – NIDC).

Marwa alifafanua kuwa huduma za Cloud Computing zinazotolewa kupitia NIDC zinawapa wateja fursa ya kuhifadhi taarifa na mifumo yao kwa usalama wa hali ya juu bila kulazimika kuwekeza gharama kubwa katika miundombinu ya kuhifadhi data, jambo linalosaidia kuongeza ufanisi wa shughuli za taasisi na biashara.

Akizungumzia utendaji wa shirika hilo, alisema TTCL imepata faida ya takribani shilingi bilioni 23 katika mwaka wa fedha 2024/2025, huku matokeo ya awali ya mwaka wa fedha 2025/2026 yakionyesha kuongezeka kwa mapato, faida na idadi ya wateja wanaotumia huduma za shirika hilo.

Alisema mafanikio hayo yametokana na utekelezaji wa maboresho ya kimkakati yaliyofanywa kufuatia maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha TTCL linaendeshwa kwa misingi ya kibiashara, linaongeza mapato na kuondokana na utegemezi wa hasara.

Marwa alisisitiza kuwa TTCL itaendelea kuwekeza katika teknolojia za kisasa na kuboresha miundombinu ya mawasiliano ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora, salama na za uhakika zinazochangia maendeleo ya uchumi wa kidijitali na Taifa kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad