JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


Serikali yawekeza maandalizi ya wataalamu wa Sayansi ya Nyuklia Kupitia Samia Scholarship

Share This
SERIKALI imeanza kwa vitendo kuwekeza katika maandalizi ya wataalamu wa sayansi ya nyuklia na teknolojia za kisasa kupitia programu ya ufadhili wa masomo ya Samia Scholarship.

Hatua inayotajwa kulenga kuijengea Tanzania uwezo wa kitaalamu katika sekta nyeti za maendeleo ya Taifa na kuondoa uhaba wa wataalamu wa sayansi ya nyuklia ili nchi iweze kufaika na rasilimali muhimu.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alieleza hayo jana Dar es salaam wakati wa hafla ya kuwaaga wanafunzi 16 wanufaika wa Samia Scholarship DS/AI waliopata ufadhili wa kwenda kusoma Chuo Kikuu cha Johannesburg, Afrika Kusini.

Akizungumza katika hafla hiyo profesa Mkenda alisema Tanzania inamiliki madini ya urani lakini ina uhaba mkubwa wa wataalamu wa sayansi ya nyuklia, hali inayozuia nchi kunufaika kikamilifu na rasilimali hiyo muhimu.

Alisema  Sayansi ya nyuklia ni muhimu sana katika masuala ya tiba, kilimo, maendeleo ya teknolojia na  mengine hivyo wanahitajika wataalamu zaidi.

"Tumeshaanzisha Samia Scholarship katika maeneo ya Sayansi ya nyuklia,  kwani nchi imekuwa na uhaba mkubwa wa watanzania waliosomea fani hiyo wakati nchi ina madini ya Urani ambayo yanahitaji uelewa katika maeneo hayo," alisema Profesa Mkenda.

Aliongeza tayari walishapeleka watanzania kusoma shahada ya pili katika masuala ya Sayansi ya nyuklia na hao wanapewa utaratibu wao kupitia utaratibu wa tume ya nguvu za atomi Tanzania.

Alisema kwa shahada ya kwanza wanachukua wanafunzi waliofanya vizuri zaidi katima masomo ya sayansi na hesabu baada ya kumaliza kidato cha sita, ambao wanakwenda kusomeshwa nje ya nchi.

Alisema sasa hivi wameanza na wanafunzi 50, watakaosoma nje ya nchi na wengine watapata ufadhili wa kusoma ndani ya nchi,  akisisitiza programu hiyo inatolewa kwa haki na uwazi bila upendeleo wowote kigezo kikuu cha kunufaika na ufadhili huo ni ufaulu wa kitaaluma.

"Kwa upande wa shahada ya pili, wamewekwa kwa madaraja na matokeo,hatuangalii sura, tunaangalia umefanya vipi katika mitihani yako, imani yetu ni kwamba huko mnakokwenda mtaendelea kufanya vizuri darasani,” alisisitiza Profesa Mkenda.

Aliongeza; "Kigezo cha kuingia katika Samia Scholarship ni kufanya vizuri darasani, ninyi ni wababe ndio maana mmechaguiwa, nitoe salamu kwa wazazi na wanafunzi kwamba wakifanya vizuri katika masomo ya sayansi serikali itawasomesha ndani au nje ya nchi".

Pia alisema kupitia utaratibu huo wa ufadhili wameweka fedha za kuwasomesha watanzania kwa shahada ya pili katika vyuo vikuu hapa nchini iliwemo Chuo kikuu cha India ambacho kina tawi Zanzibar kinachochukua wanafunzi kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Alisema chuo kingine ni Nelson Mandela Institute Science and Technology, akisisitiza sayansi ni muhimu kwani nchi nyingi zinaendelea kwa sababu ya sayansi na teknolojia na nchi ambayo haiwekezi katika sayansi ni vigumu kuendelea.

"Watanzania wanahaki ya kupata fursa hizi zinazobeba jina la Rais wetu,zinagawanywa kwa haki na uwazi bila uoendeleo, asije kukosa mtoto wa mkulima kwasababu mtoto wa Mkenda anataka kwenda kusoma kule, uwazi huo tunautangaza ili ukiona tunaenda isivyo sahihi mtuambie au mwende takukuru mkawaambie" alisema 

Mmoja wa wanafunzi ambao ni wanufaika wa ufadhili, Malaika Florence akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake, aliishukuru serikali na Rais Samia Suluhu Hassan kupitia ufadhili huo.

"Tunajua taifa limetuamini tunaahidi kuwa watu bora, tutasoma kwa bidii ili tuwe sehemu ya kutimiza malengo ya dira ya taifa ya 2050" alisema Malaika.


































No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad