Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) leo tarehe 30 Januari, 2026 umepokea ugeni wa wanafunzi 30 wa Kitengo cha Petroleum Engineering kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), chini ya Chama cha wahandisi wa mafuta (Society of Petroleum Engineers -SPE),waliotembelea Wakala huo kwa lengo la kujifunza kwa vitendo kuhusu utendaji kazi wa PBPA na namna Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (BPS) unavyotekelezwa nchini.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kaimu Meneja wa Kitengo cha Lojistiki za Mafuta PBPA, Mhandisi Sophia Kidimwa, alisema kuwa wanafunzi hao wamepata fursa ya kuelewa mchakato mzima wa upatikanaji wa mafuta nchini kuanzia hatua za uagizaji hadi usimamizi wa lojistiki za kupokea mafuta.
“Tumepokea ugeni wa wanafunzi wa mwaka wa nne kutoka UDSM na DMI waliokuja kujifunza kuhusu taratibu zote za upatikanaji wa mafuta hapa Tanzania, jinsi mafuta yanavyoingia nchini, mchakato mzima wa uletaji wake pamoja na lojistiki za kupokea mafuta na manufaa ya Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (BPS),” alisema Sophia.
Aliongeza kuwa PBPA imekuwa ikipokea wageni kutoka taasisi mbalimbali zinazopenda kujifunza kuhusu mfumo wa BPS kutokana na mafanikio na manufaa yake kwa Taifa.
“Kama taasisi, tumekuwa tukitoa uelewa huo kwa wageni wetu na wamekuwa wakionyesha kuridhika. Tunaendelea kuwakaribisha wadau wote wanaopenda kujifunza kuhusu Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Mhandisi kutoka Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Prudence Laurean, alisema wanafunzi hao walipitishwa katika mifumo yote ya PBPA kuanzia hatua za uagizaji wa mafuta hadi mafuta yanapofika kwenye maghala ya kuhifadhia, ikiwemo matumizi ya Mfumo wa SCADA katika ufuatiliaji wa mafuta wakati wa kushushwa kutoka melini kwenda kwenye maghala ya Serikali na binafsi.
“Mafunzo haya ni muhimu sana kwa wanafunzi kwani yanawajengea uelewa wa kina kuhusu kazi za PBPA na faida zitakazowasaidia kitaaluma hapo baadaye,” aliongeza.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi, Sifrina John, mwanafunzi wa mwaka wa nne Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema ziara hiyo imelenga kuwaunganisha wanafunzi na uhalisia wa kazi katika sekta ya mafuta nchini.
“Lengo letu ni kuunganisha yale tunayojifunza darasani na mazingira halisi ya kazi katika sekta ya mafuta, na kuelewa kwa vitendo jinsi PBPA inavyofanya kazi katika uagizaji na usimamizi wa ugavi wa mafuta nchini,” alisema Sifrina.
Aliongeza kuwa wanafunzi wamefurahishwa na mafunzo waliyoyapata na namna PBPA inavyosimamia ugavi wa mafuta pamoja na mchango wake katika uchumi wa Taifa.
“Tumepata uelewa wa kina kuhusu mchakato wa uagizaji wa mafuta, usimamizi wa ugavi na mchango wa PBPA katika uchumi wa nchi. Mafunzo haya yametujenga kwa kiasi kikubwa kwa kuunganisha nadharia na vitendo,” alisisitiza.
Ziara hiyo ni mwendelezo wa juhudi za PBPA katika kuimarisha ushirikiano na wadau kutoka taasisi mbalimbali nchini sambamba na kukuza uelewa wa vijana kuhusu mifumo ya kimkakati inayosimamia sekta ya mafuta na mchango wake katika uchumi wa Taifa.









No comments:
Post a Comment