Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt Hassan Abbasi amewakaribisha wananchi na wadau mbalimbali kuchangamkia fursa za uwekezaji zinazopatikana kwenye hifadhi za misitu ya Serikali nchini.
Akizungumza na Waandishi wa habari
kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere maarufu sabasaba
alipotembelea maonesho ya 47 ya kimataifa ya Dar es salaam leo tarehe
08/07/2023 kuona namna Wizara ya Maliasili na Utalii inavyoshiriki
katika maonesho hayo.
Dkt Abbasi amesema Serikali kupitia Wizara
ya Maliasili na Utalii imejikita katika kubuni fursa mbalimbali
zinazolenga kumkwamua mwananchi hasa kwenye maeneo ya uwekezaji katika
sekta ya Utalii, misitu na malikale.
"Serikali inapanga mikakati
mingi kuongeza fursa kwenye maeneo ya uhifadhi na tayari wataalamu wetu
wanaandaa mkakati mmojawapo unaoitwa "achia shoka kamata mzinga" maana
yake uache kukata miti ili utundike mizinga ufuge nyuki,"
"Pamoja
na kwamba elimu kwa wananchi haijawa kubwa lakini tayari asali
inachangia kwa asilimia kubwa pato la taifa na sasa tunataka hamasa na
elimu itolewe zaidi ili kuongeza uwekezaji katika ufugaji nyuki"
Amesema Dkt Abbasi.
Ameongeza kuwa kwenye maeneo mengi ya
hifadhi za misitu kuna fursa ya kuwekeza kwenye shughuli za utalii hasa
ujenzi wa miundombinu na huduma za chakula na malazi na hivyo
kuwakaribisha wadau mbalimbali kuchangamkia fursa hizo hasa katika
kipindi hiki ambapo utalii umeonesha mafanikio makubwa kutokana na
Filamu ya Royal Tour.
Aidha, Dkt Abbasi amepongeza Mamlaka,
Wakala na taasisi za Wizara kwa kushiriki maonesho ya 47 ya kimataifa ya
biashara ya Dar es salaam ya 2023 huku akisisitiza taasisi hizo
kuongeza matumizi ya teknolojia na mifumo ya kidijitali katika utoaji wa
huduma hasa huduma za utalii.
Naye Kamishna wa uhifadhi TFS,
Prof. Dos Santos Silayo ambaye ameambatana na Katibu Mkuu kwenye ziara
hiyo amewakaribisha wananchi na wadau kutembelea banda la Maliasili na
utalii hususani eneo la TFS ambapo watapata uelewa kuhusu faida za
uhifadhi endelevu wa misitu.
"Nitoe wito kwa wananchi na wadau
kutembelea maeneo yetu kwenye maonesho haya lakini kuna wengine
hawajaweza kufika bado lakini wanaweza kujifunza kupitia vyombo vya
habari ambavyo tumekuwa tukitumia kwenye maonesho haya wapate uelewa
kuhusu fursa za uwekezaji kwenye ufugaji nyuki, biashara ya asali,
utalii ikolojia, uvunaji na usafirishaji wa mazao ya misitu."
Hata
hivyo Prof. Silayo ameendelea kusisitiza utunzaji wa misitu yote nchini
ili kuleta matokea chanya ya uhifadhi ikiwa ni pamoja na kupanda miti
kwa wingi na kuhakikisha miti inayopandwa au iliyopo inatunzwa kwaajili
ya kizazi cha sasa na cha baadae.
"Kumekuwa na changamoto nyingi
kwenye uhifadhi lakini changamoto kubwa ni moto, moto unaharibu sana
misitu na hivyo natoa wito pia kwa wananchi kuendelea kushirikiana na
aerikali kwa kujiepusha na uanzishaji wa moto holela lakini pia
kuudhibiti haraka pale unapozuka,” Amesema Prof. Silayo.
Sambamba
na hilo Prof. Silayo amemshukuru Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na
Utalii Dkt Hassan Abbas kwa kutenga muda wa kutembelea banda la
Maliasili na Utalii na kukutana na wadau walileta vioneshwa kwenye
maonesho hayo.
Maonesho ya 47 ya kimataifa ya Dar es
salaam(sabasaba 2023)yanaendelea jijini Dar es salaam kwa kauli mbiu
isemayo "Tanzania mahali sahihi kwa biashara na uwekezaji" na
yanatarajiwa kufungwa tarehe 13/07/2023
No comments:
Post a Comment