Na Karama Keyunko,Blogu ya jamii.
MAHAKAMA ya Hakimu
Mkazi Kisutu leo, imeruhusu mfanyabiashara Yusuf Manji na wenzake watatu kupelekwa
polisi na kuhojiwa dhidi ya kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili ili kukamilisha
upelelezi.
Uamuzi huo umetolewa
na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi kufuatia barua ya maombi kutoka kwa Mkuu
wa upelelezi Kanda maalumu ya Dar es Salaam, (ZCO), ndipo akaandika hati ya kuwatoa
washtakiwa mahabusu (remove order) ili kuwafanyia mahojiano katika kesi namba
33/2017
Amesema hawawezi
kukataa maombi hayo ya polisi kwani kufanya hivyo ni sawa na kupingana na kauli
ya mahakama ya kukamilisha upelelezi, na ndio maana ikatolewa hati ya kuwatoa
mahabusu kwa ajili ya mahojiano. “Hii sio mara ya kwanza kuwatoa washitakiwa
kwa upelelezi," alisema Hakimu Shaidi.
Aidha amewaagiza
polisi kuhakikisha washtakiwa wanatendewa ikiwemo kuzingatia afya zao kwani
wanawakabidhi wakiwa na afya nzuri na kama watahitaji uwakilishi wa mawakili
wao wapate uhuru wa kuwakilishwa kwenye jambo lolote na isiwe kificho.
Hakimu Shahidi
amesema, "Namkabidhi Koplo Dotto kama barua inavyoelekeza kuwa nimkabidhi Sajenti
Mkombozi au Doto lakini kwa kuwa Mkombozi hayupo basi namkabidhi Doto ila
washitakiwa warudishwe kesho ndani ya muda wa kazi.
Mbali na Manji,
washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Meneja Rasilimali watu wa Kampuni ya
Quality Group Ltd, Deogratius Kisinda (28), Mtunza stoo, Abdallah Sangey (46)
na Thobias Fwere (43) mkazi wa Chanika wanakabiliwa na mashitaka ya
uhujumu uchumi.
Mapema, akiwasilisha
maombi hayo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi aliiomba mahakama
iruhusu washitakiwa waweze kukabidhiwa kwa Polisi ili kutimiza matakwa ya
upelelezi ambapo amedai kifungu
Cha 59 cha CPA kinawapa
mamlaka Polisi kufanya upelelezi.
Hata hivyo, wakili wa
utetezi Hudson Ndusyepo alipinga watuhumiwa kwenda kuhojiwa kwa madai kuwa, mahakama
hiyo haina mamlaka ya kutoa amri hiyo sababu DPP hajatoa Kibali kwa mahakama
hiyo kusikiliza kesi hiyo zaidi ya kutaja tarehe, alidai mahakama hiyo
imefungwa mikono ya kutoa amri dhidi ya maombi hayo au yoyote yale.
Naye wakili Hajra
Mungula aliiomba mahakama kukataa ombi hilo kwa madai kuwa washitakiwa hao wako
chini ya ulinzi na kwamba upande wa mashitaka uliwashitaki washitakiwa kwa
mbwembwe na kuwasilisha hati ya kuwazuia dhamana huku wakijua kwamba
hawajakamilisha upelelezi
Hata hivyo, Wakili
Kishenyi alidai mahakama imekuwa ikisisitiza kukamilisha upelelezi na kwamba
wanachofanya ni sehemu ya kukamilisha upelelezi.
Pia alidai washitakiwa
hao wanahaki ya kuwakilishwa hivyo maombi yao yakubaliwe.
Washtakiwa hao
wanadaiwa kukutwa na sare za na vifaa mbali mbali vya jeshi.
Mfanyabiashara
Yusuph Manji, akitoka Mahakamani baada ya Hakimu Mkazi, Huruma Shahidi
kuruhusu yeye na wenzake watatu wanaokabiliwa na tuhuma za uhujumu
uchumi kupelekwa polisi kuhojiwa ili kukamilisha upelelezi.
No comments:
Post a Comment