JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


BODABODA WILAYANI KILINDI WAPIGWA MSASA SHERIA USALAMA BARABARANI

Share This
Na Mwandishi Wetu, Kilindi

SHIRIKA la Amend kwa kushirikiana na Ubalozi wa Uswiss nchini Tanzania wameendelea na kampeni ya kutoa mafunzo ya usalama barabarani kwa waendesha bodaboda wilayani Kilindi mkoani Tanga.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Mkuu wa Wilaya ya Kilindi Hashim Mgandilwa amesema anatoa shukrani kwa Amend kwa kuona umuhimu wa mafunzo hayo kwa waendesha bodaboda na katika wilaya hiyo vijana 180 wamepatiwa mafunzo yaliyofanyika katika vituo vinne.

Amevitaja vituo ambavyo vimetumiwa kutolewa kwa mafunzo hayo ni Songe Mjini, Kwa Madoti, Kibirashi na KwediBoma huku akisisitiza kuwa mahitaji ya mafunzo hayo ni makubwa kwani waendesha bodaboda wengi hawana elimu ya usalama barabarani, hivyo ni muhimu Amend ikawafikia bodaboda wengi zaidi.

“Kama Wilaya tumekuwa tukishirikiana na wadau mbalimbali kama Chuo cha VETA hapa Kilindi kwa ajili ya kutoa mafunzo ya usalama barabarani na tayari vijana 100 wamepatiwa mafunzo haya.Kutokana na mahitaji kuwa makubwa tumefungua milango kwa wadau wengine na Amend wameitikia maombi yetu na sasa vijana 180 wameshiriki kampeni hii,”amesema Mgandilwa.

Awali akizungumza mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Mratibu wa Shirika la Amend Ramadhan Nyanza amesema kutolewa kwa mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa kampeni ya usalama barabarani kwa vijana katika Mkoa wa Tanga.

Amefafanua katika kufanikisha mafunzo hayo wamekuwa wakishirikiana na wadau muhimu kama Jeshi la Polisi pamoja na Usalaba Mwekundu ambao wamekuwa wakitoa mafunzo kuhusu utolewaji wa huduma ya kwanza inapotokea ajali.

Pia ametumia nafasi hiyo kusisitiza kuwa Amend kupitia ufadhili wa Ubalozi wa Uswiss nchini wataendelea kuwafikia vijana hasa waendesha bodaboda katika maeneo mbalimbali na imani yao hadi mradi huo utakapofika mwisho watakuwa wamefikiwa vijana wengi zaidi.

Kwa upande wake Shaban Abdallah ambaye ni mmoja ya waendesha bodaboda waliopatiwa mafunzo hayo, amesema kabla ya mafunzo hayo alikuwa akiendesha bodaboda kwa kutumia uzoefu lakini sasa amefahamu sheria za usalama barabarani na hivyo atakuwa balozi mzuri kwa vijana wenzake ambao hawajapa mafunzo hayo.








No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad