Friday, June 24, 2016

RAIS DKT. MAGUFULI AKUTANA NA BALOZI WA NORWAY, FINLAND NA MJUMBE MAALUM KUTOKA OFISI YA WAZIRI MKUU WA MALAYSIA, IKULU JIJINI DAR ES SALAAM.


  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na balozi wa Norway hapa nchini Hanne-Marie Kaarstand watatu kutoka kushoto mara baada ya kumaliza mazungumzo  yao Ikulu jijini Dar es Salaam.
 wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Balozi wa Norway hapa nchini Hanne-Marie Kaarstand Ikulu jijini Dar es Salaam.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Balozi wa Norway hapa nchini Hanne-Marie Kaarstand mara baada ya kumaliza mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es Salaam.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisoma barua ya pongezi iliyowasilishwa kwake na Waziri kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu wa Malaysia Dato Sri Idris Jala ambaye ni Mjumbe Maalum wa Waziri Mkuu wa Malaysia.

PROF. MBARAWA AKAGUA UPANUZI WA UWANJA WA NDEGE DODOMA


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa Mkandarasi Kampuni ya Chico, anayefanya upanuzi wa njia ya kuruka na kutua ndege katika Uwanja wa ndege wa Dodoma.
Ujenzi wa Barabara ya Kuruka na kutua ndege katika Uwanja wa ndege wa Dodoma ukiendelea. Ujenzi huo kwa kiwango cha lami unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi miwili.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa Meneja wa Miradi wa Mamlaka ya Viwanja Vya Ndege Tanzania (TAA) Eng. Mbila Mdemu ( wa pili kulia), wakati alipokagua maendeleo ya mradi wa upanuzi wa uwanja wa ndege wa Dodoma.

Meneja wa Miradi wa Mamlaka ya Viwanja Vya Ndege Tanzania (TAA) Eng. Mbila Mdemu, akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alipokagua maendeleo ya upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Dodoma.

————————————————————-

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ametoa miezi miwili kwa mkandarasi Chicco anaefanya upanuzi wa njia ya kuruka na kutua ndege katika uwanja wa ndege wa dodoma kuhakikisha kuwa ujenzi huo unakamilika.

Akizungumza mara baada ya kukagua kazi ya upanuzi wa uwanja huo, Prof. Mbarawa amemtaka Mkandarasi huyo kuhakikisha kuwa ujenzi wa uwanja huo unafanyika kwa kuzingatia viwango vilivyokubalika katika mkataba na kuukabidhi kwa wakati.

“Hakikisheni upanuzi huu unakamilika kwa wakati ili kuupa hadhi inayostahili uwanja wa ndege wa Dodoma,hasa mkizingatia umuhimu wake kitaifa’, amesema Prof. Mbarawa.

Naye Mkandarasi anaejenga uwanja huo amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa atahakikisha ujenzi wake unazingatia viwango na kuukabidhi katika muda uliokubalika kimkataba.

Zaidi ya shilingi bilioni 11.8 zinatarajiwa kutumia katika upanuzi huo na hivyo kuwezesha ndege nyingi zaidi kutumia uwanja huo.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MAKAMU WA RAIS MHE. SAMIA SULUHU AKUTANA NA WAZIRI KUTOKA MALAYSIA NA MAKAMU WA RAIS WA TIGO AFRIKAMakamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akizungumza na Waziri asiye na Wizara Maalum katika Ofisi ya Waziri Mkuu wa Malaysia na Mkurugenzi Mtendaji wa kitengo kinachoshughulikia masuala ya utendaji Na utekelezaji wa miradi ya serikali Dk. Sri Idris Jala ,Ikulu jijini Dar es Salaam.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Makamu wa Rais wa Tigo Afrika Bi. Rachel Samren (Kushoto) wakati Bi. Rachel Samren alipomtembelea Makamu wa Rais ofisini kwake Ikulu jijini Dar es salaam leo tarehe 24 Juni 2016.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Waziri asiye na Wizara Maalum katika Ofisi ya Waziri Mkuu wa Malaysia na Mkurugenzi Mtendaji wa kitengo kinachoshughulikia masuala ya utendaji Na utekelezaji wa miradi ya serikali Dk. Sri Idris Jala (kushoto) mara baada ya mazungumzo ,Ikulu jijini Dar es Salaam.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Waziri asiye na Wizara Maalum katika Ofisi ya Waziri Mkuu wa Malaysia na Mkurugenzi Mtendaji wa kitengo kinachoshughulikia masuala ya utendaji Na utekelezaji wa miradi ya serikali Dk. Sri Idris Jala na ujumbe wake mara baada ya mazungumzo ,Ikulu jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa pamoja na Makamu wa Rais wa Tigo Afrika Bi. Rachel Samren wengine pichani kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano na Masuala ya Kisheria Bi. Sylvia Balwire na Bi. Halima Okash Afisa Uhusiano (wa kwanza kushoto) Ikulu jijini Dar es salaam leo tarehe 24 Juni 2016.
——————————————————–

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania SAMIA SULUHU HASSAN ameiomba serikali ya MALAYSIA kujenga ofisi za ubalozi wake hapa
nchini ili kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Makamu wa Rais ametoa kauli hiyo leo Juni 24, 2016 alipokutana na kufanya mazungumzo Waziri asiye na Wizara Maalum Dkt SRI IDRIS JALA ambaye
aliongozana na Balozi wa MALAYSIA aliye na makazi yake jijini Nairobi Kenya, ISMAIL SALAM walipomtembelea ofisini kwake Ikulu jijini Dar Salaam.

Makamu wa Rais amesema ujenzi wa ofisi za ubalozi huo hapa nchini utarahisisha kwa kiasi kikubwa Watanzania wanaotaka kusafiri kwenda nchini MALAYASIA kwa ajili ya shughuli mbalimbali zikiwemo za masomo na biashara kuliko hali ilivyo sasa ambapo ofisi za balozi hizo zipo Nairobi – Nchini KENYA.

Kwa upande wake Waziri asiye na Wizara Maalum Dkt SRI IDRIS JALA amemhakikishia Makamu wa Rais kuwa nchi yake itaendelea kuimarisha,kukuza na kuendeleza mahusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Malaysia hasa uanzishaji wa ubalozi wake hapa nchini.

Hata hivyo, Waziri huyo amesisitiza umuhimu wa kuanzishwa kwa Makubaliano ya pamoja ya ushirikiano kati ya Tanzania na Malaysia ambayo yatajikita katika sekta mbalimbali zikiwemo za elimu, uchukuzi na biashara.

Wakati huo huo, Makamu wa Rais SAMIA SULUHU HASSAN pia amekutana Makamu wa Rais wa TIGO – Afrika RACHEL SAMREN ambapo wamezungumzia masuala mbalimbali ikiwemo namna kampuni hiyo itakavyosadia katika kuwawezesha wanawake kuondokana na umaskini hapa nchini.

Katika kuhakikisha taifa linaongeza ukusanyaji wa mapato,
Makamu wa Rais ameuhimiza uongozi wa kampuni ya Simu ya Tigo hapa nchini kuhakikisha unalipa kodi kwa uwazi ili fedha hizo ziweze kusaidia serikali katika kuimarisha utoaji wa huduma za kijamii hapa nchini.

Rais Magufuli apokea ujumbe wa Waziri Mkuu wa Malaysia na pia akutana na mabalozi wawili


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli amemhakikishia Waziri Mkuu wa Malaysia Mhe. Najib Razak kuwa serikali yake ya awamu ya tano itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano na Malaysia hususani katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kukuza biashara na uwekezaji.

Rais Magufuli amesema hayo leo tarehe 24 Juni, 2016 Ikulu Jijini Dar es salaam baada ya kupokea barua yenye ujumbe wa Waziri Mkuu wa Malaysia iliyoletwa kwake na Mjumbe Maalum wa Waziri Mkuu huyo Mhe. Dato Sri Idris Jala ambaye ni Waziri katika ofisi ya Waziri Mkuu wa Malaysia.

Pamoja na kupokea barua hiyo, Rais Magufuli na Mhe. Dato Sri Idris Jala wamezungumzia miradi mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Malaysia, na wametilia mkazo umuhimu wa kuitumia vizuri sekta binafsi katika uwekezaji kwenye miradi ya maendeleo hususani viwanda, miundombinu na maendeleo ya makazi.

"Naomba unifikishie shukrani zangu za dhati kwa Waziri Mkuu wa Malaysia Mhe. Najib Razak na umwambie kuwa serikali yangu itaendelea na kukuza zaidi ushirikiano na Malaysia na nitafurahi zaidi kama mahusiano na ushirikiano wetu utajikita katika kubadilishana uzoefu juu ya kupata mageuzi katika uchumi kama ambavyo Malaysia imefanya.

"Nawakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Malaysia na kwa kuwa nchi yenu ina shirika kubwa la ndege basi itakuwa ni vyema kama uzoefu mlionao tukashirikiana kwa kuwa nasi tumeamua kufufua shirika letu la ndege na kwa kuanzia tutanunua ndege tatu hivi karibuni" Amesema Rais Magufuli.

Katika hatua nyingine Rais Magufuli amekutana na kufanya Mazungumzo na Balozi wa Norway hapa nchini Mhe. Hanne-Marie Kaarstand ambapo pamoja kuzungumzia uhusiano na ushirikiano kati ya nchi hizi mbili katika masuala mbalimbali yakiwemo uwekezaji katika sekta ya nishati na kilimo, wamezungumzia kuendeleza ushirikiano huo katika mapambano dhidi ya rushwa na ujangili kwa kuimarisha vyombo vinavyohusika ambavyo ni Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU), Mahakama na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP).

Kwa upande wake Balozi wa Norway hapa nchini Mhe. Hanne-Marie Kaarstand amesema tangu miaka ya 60 mpaka sasa Norway imetumia dola za kimarekani Bilioni 2 kuunga mkono miradi mbalimbali ya maendeleo na huduma za kijamii kwa Tanzania na kwamba itaendelea kushirikiana na Tanzania kama ambavyo hivi sasa inafanya kazi na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) katika kudhibiti matumizi na kuimarisha ukusanyaji wa mapato.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Finland hapa nchini Mhe. Pekka Hukka ambapo Balozi huyo amesema Finland inatambua na inaunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Magufuli katika kuhimiza uchapa kazi, ulipaji wa kodi na kukabiliana na rushwa.

Mhe. Pekka Hukka pia amemhakikishia Dkt. Magufuli kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo mbalimbali ya maendeleo yakiwemo kuwajengea uwezo viongozi, utunzaji wa misitu na hifadhi za wanyama pamoja na maendeleo ya elimu.

Kwa upande wake Rais Magufuli amemuomba Balozi huyo kufikisha shukrani zake kwa Rais wa Finland Mhe. Sauli Niinisto na kumweleza kuwa serikali yake ya awamu ya tano itaendeleza na kuimarisha zaidi ushirikiano na Finland, na ameiomba nchi hiyo kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha vyombo vya kupambana na rushwa ambavyo ni TAKUKURU, Mahakama na Ofisi ya DPP.
 
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
24 Juni, 2016

Rais Dkt. Shein afanya uteuzi wa viongozi katika Taasisi mbali mbali za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar .

IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR

———————————

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein amefanya uteuzi wa viongozi katika Taasisi mbali mbali za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar .

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, katika Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Nd. Bakari Khamis Muhidin ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Uendeshaji na Utumishi.

Mkurugenzi wa Idara ya Mipango ya Raslimaliwatu ni ndugu Khamis Haji Juma na Ofisa Mdhamini wa Wizara ya Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Pemba Nugu Masoud Ali Mohamed.

Katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara maalum za Serikali Mkurugenzi wa Idara ya Mipango, Sera na Utafiti ni Ndugu Daima Mohammed Mkalimoto.Wizara ya Fedha na Mipango alieteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Uendeshaji na Utumishi ni Ndugu Ali Bakari Ishaka, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Barabara ni Ndugu Mwalim Ali Mwalim na Ofisa Mdhamini wa Wizara hiyo Pemba ni Ndugu Ibrahim Saleh Juma.

Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto Kamishana wa Kazi ni Ndugu Fatma Iddi Ali, Mkurugenzi wa Idara ya Ustawi wa wazee Ndugu Wahida Maabad Mohamed na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana Ndugu Mwanaidi Mohamed Ali.

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Wanawake na Watoto Ndugu Nasima Haji Choum na Ofisa Mdhamini, Wizara ya Kazi Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto Pemba Ndugu Khadija Khamis Rajab.

Dkt. Fadhil Mohamed Abdullah anakuwa Mkurugenzi wa Kinga na Elimu ya Afya katika Wizara ya Afya na Mkurugenzi wa Huduma za Hospitali ni Dkt. Mohammed Dahoma.

Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Naibu Katibu Mkuu (Mifugo na Uvuvi) ni Dkt. Islam Seif Salum. Mkurugenzi wa Mipango, Sera na Utafiti ni Ndugu Sheha Idrissa Hamad na Mkurugenzi wa Uendeshaji na Utumishi Ndugu Noah Saleh Said.

Mkurugenzi wa Idara ya Kilimo ni Ndugu Mohamed Khamis Rashid, Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Maliasili zisizorejesheka Ndugu Yussuf Haji Kombo wakati Dkt. Bakari Saad Assed anakuwa Mkurugenzi wa Chuo cha Kilimo, Kizimbani.Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo, Kizimbani ni Dkt. Suleiman Shehe Mohammed, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi Ndugu Mussa Aboud Jumbe, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mifugo Dkt. Yussuf Haji Khamis na Ofisa Mdhamini, Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Pemba ni Ndugu Sihaba Haji Vuai.

Katika Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo Ndugu Hassan Abdalla Mitawi ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu (Habari), Mkurugenzi wa Mipango, Sera na Utafiti Ndugu Mahmoud Omar Hamad.Ndugu Imane Duwe ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa ZBC ni Nassra Mohammed Juma.

Katibu Mtendaji wa Tume ya Utangazaji ni Ndugu Rafii Haji Makame, Mhariri Mtendaji wa Shirika la Magazeti ya Serikali Ndugu Yussuf Khamis Yussuf, Mkurugenzi wa Habari (Maelezo) Ndugu Hassan Vuai.Mkuu wa Chuo cha Uandishi wa Habari ni Chande Omar Omar na Ofisa Mdhamini, Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo Pemba Ndugu Khatib Juma Mjaja.

Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Mkurugenzi wa Uendeshaji na Utumishi ni Ndugu Bimkubwa Abdi Nassib. Mkurugenzi wa Mipango, Sera na Utafiti Ndugu Khatib Mohamed Khatib na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri Baharini ni Ndugu Abdalla Hussein Kombo.

Kwa mujibu wa Taarifa hiyo, Mkurugenzi wa Baraza la Mitihani katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ni Ndugu Zubeir Juma Khamis.Ofisa Mdhamini Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Pemba ni Ndugu Juma Bakari Alawi na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) ni Dkt. Said Seif Mzee.

MASAHIHISHO YA TAREHE KUTOA MAONI KUHUSU MUSWADA WA SHERIA YA MANUNUZI 
Katika kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia matakwa ya Kanuni ya 117 (9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Januari 2016; Kamati ya Bunge ya Bajeti imepanga kufanya mkutano wa kusikiliza maoni ya wadau wote wa masuala ya Ugavi (Public Hearing) kuhusu Muswada wa Sheria ya Manunuzi ya Umma wa Mwaka 2016(Public Procurement Act 2016) kabla Muswada huo haujapitishwa na Bunge kuwa Sheria .
                                                        
Mkutano huo wa kusikiliza maoni ya wadau (Public Hearing) unatarajiwa kufanyika  siku ya Jumatatu Juni 27, 2016 Bungeni Dodoma kuanzia saa Tano Asubuhi katika Ukumbi wa Pius Msekwa, Bungeni - Dodoma.

Kwa kuzingatia umuhimu wa Muswada huo, Kamati inawaalika wadau wote kufika na kuwasilisha maoni yao mbele ya Kamati kabla kupelekwa katika hatua nyingine. Maoni ya wadau yanaweza pia kuwasilishwa kwa njia ya Posta au Barua pepe kwa anuani ifuatayo:

Katibu wa Bunge,
Ofisi ya Bunge,
S.L.P. 941,
DODOMA
Barua pepe: cna@bunge.go.tz

Imetolewa na,

Kitengo cha Habari, ElimunaMawasiliano.
Ofisi ya Bunge,
S.L.P 941,
DODOMA

24 Juni, 2016.

WAZIRI MWIGULU AFUNGA MAFUNZO YA AWALI YA JESHI LA POLISI NA UHAMIAJI NAMBA 1/2015/2016, CCP MJINI MOSHI


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba akikagua gadi ya wahitimu wa Jeshi la Polisi na Uhamiaji kabla ya kuyafunga mafunzo ya wahitimu hao wa mafunzo ya awali yaliyofanyika katika Chuo Cha Polisi (CCP) mjini Moshi. Jumla ya wahitimu 3,904 walimaliza mafunzo.
Wahitimu wa mafunzo ya awali ya Jeshi la Polisi na Uhamiaji wakimuonyesha Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba (hayupo pichani) jinsi miili yao ilivyokuwa imara kwa pikipiki kupita juu ya matumbo yao. Jumla ya wahitimu 3,904 walimaliza mafunzo hayo ambayo yamefungwa rasmi na Waziri Nchemba
Kikosi cha gwaride la heshima kikitoa heshima mbele ya mgeni rasmi Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba (kushoto jukwaa kuu) wakati wa sherehe yao ya kumaliza mafunzo ya awali ya Jeshi la Polisi na Uhamiaji, Chuo cha Polisi (CCP) mjini Moshi. Jumla ya wahitimu 3,904 walimaliza mafunzoWaziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba akimkabidhi zawadi mhitimu Irene Joji (kushoto) kwa kufanya vizuri katika masomo yake wakati wa mafunzo ya awali ya Polisi na Uhamiaji yaliyofanyika katika Chuo Cha Polisi (CCP) mjini Moshi. Jumla ya wahitimu 3,904 walimaliza mafunzo hayo ambayo yamefungwa rasmi na Waziri Nchemba mjini humo leo. 
 
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba (kushoto) akisalimiana na Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Abdulrahman Kaniki wakati Waziri huyo alipokuwa anawasili katika viwanja vya Chuo Cha Polisi (CCP), mjini Moshi kwa ajili ya kufunga mafunzo ya awali ya Polisi na Uhamiaji, kulia ni Kaimu Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Victoria Lembeli na watatu kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadick.

PICHA ZOTE NA KITENGO CHA MAWASILIANO YA SERIKALI

WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI.

KAMPUNI YA AIRTEL KUZINDUA MSIMU WA AIRTEL RISING STAR JUNI 26 JIJINI DAR ES SALAAM.

Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii.
KAMPUNI  ya Simu ya Airtel imeweka mikakati ya kuinua soka la vijana kwa kuweka wazi hatua yao ya kuzindua msimu wa sita wa Airtel Rising Stars utakaofanyika Juni 26 mwaka huu huku akiwataka wadau kujitokeza ili kuweza kuinua soka la vijana.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel, Beatrice Singano amesema kuwa msimu huu wa sita utakuwa na mabadiliko makubwa sana kwani kwa sasa wanamikakati mikubwa ya kuinua soka la vijana hasa baada ya kuona timu ya vijana ya chini ya miaka 17 Serengeti Boys kufanya vizuri kwenye michezo waliyocheza ya kirafiki pamoja na mashindano ya AIFF yaliyofanyika nchini India na kufanikiwa kushika nafasi ya tatu.

Naye Kocha Mkuu wa  timu hiyo Bakari Shime amesema kuwa hiyo ni hatua nzuri sana kwa Kampuni ya Airtel kuendelea kusapoti michezo hususani kwa vijana kwani ni moja ya msingi mzuri wa kuinua michezo pamoja na kuwjenga wachezaji wakiwaangali wadogo

  Mkufunzi wa soka la vijana Nchini Kim Poulsen amewashikiri Airtel kwani katika mashindano hayo anaeweza kupata wachezaji wazuri ambao watawajenga na kuleta ushindani wa soka baaadae.
 Mkurugenzi wa Mawasiliano Airtel, Beatrice Singano akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani katika uzinduzi wa sita wa Airtel Rising Stars utakaofanyika Juni 26 mwaka huu pamoja na kuweka mikakati katika kusaidia kuinua soka la vijana Nchini na kuwataka makampuni kujitokeza kuwekeza soka la vijana.
Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 Serengeti Boys akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani katika uzinduzi wa sita wa Airtel Rising Stars utakaofanyika Juni 26 mwaka huu huku akizungumzia maandalizi ya kikosi chake kueleka mchezo wao dhidi ya Timu ya Taifa ya Visiwa vya Shelisheli siku ya Jumapili  kuwania kufuzu kucheza Mataifa Afrika nchini Madagascar  2017.
 Mkufunzi wa soka la vijana nchini Mholanzi, Kim Poulsen akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani katika uzinduzi wa  Airtel Rising Stars msimu wa sita unaotarajiwa kufanyika Juni 26 mwaka huu.
Kikosi cha vijana chini ya miaka 17 Serengeti Boys wakiwa katika picha ya pamoja  Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel, Beatrice Singano  (katikati) na  Mkurugenzi wa soka la vijana  TFF, Ayoub Nyenzi katika uzinduzi Airtel Rising Stars msimu wa sita unaotarajiwa kufanyika Juni 26 mwaka huu.

Watanzania waaswa kuzingatia umri katika kuangalia filamu na maigizo

Na Raymond Mushumbusi WHUSM

Watanzania wameaswa kuzingatia umri katika kungalia filamu katika majumba ya sinema na sehemu mbalimbali.

Wito huo umetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Bibi. Joyce Fisso wakati akifafanua masuala mbalimbali kuhusu tasnia ya filamu nchini kwa waandishi wa habari.

Bibi Joyce Fisso amesema kuwa Bodi yake inafanya kazi ya kuzipa kiwango kazi za filamu na maigizo ikiwemo umri sahihi wa kuangalia filamu na hili linapaswa kuzingatiwa na waoneshaji na waangaliaji wa Filamu.

“ Natoa wito kwa watanzania hasa wazazi kuzingatia umri katika kuangalia filamu, ukiona imeandikwa umri wa miaka 18 ujue ni maalum kwa ajili ya umri huo na mtoto chini ya hapo hatakiwa kuangalia kwasababu maudhui ya filamu au maigizo hayo hayamuhusu alisisitiza Bibi. Joyce.

Bibi Joyce Fisso ameongeza kuwa jukumu la kujenga maadili kwa watanzania hasa watoto lipo mikononi mwa wazazi wao na kuwaasa wazazi kuzingatia umri katika kuangali filamu na maigizo mbalimbali ili kupunguza wimbi la mmomonyoko wa maadili nchini.

Aidha Bibi Joyce Fisso ameshauri waandaaji wa filamu na maigizo nchini kuandaa filamu na maagizo yenye maudhui ya watoto ya kuwajenga katika Mila, Desturi na Tamaduni za kitanzania kwa kuwa ndio kizazi cha baadae na kinatakiwa kulelewa katika maadili mema.

Bodi ya Filamu inapokea filamu na maigizo mbalimbali kwa ajili ya kupata kibali cha kusambazwa na zaidi ya asilimia 70 ya filamu hizo maudhui yake ni mapenzi hivyo basi jamii inatahadharishwa kuzingatia umri uliowekwa katika filamu na maigizo hayo ili kuepukana na mmomonyoko wa maadili kwa watoto uanaozidi kuongezeka siku hadi siku kwa kuangalia filamu na maigizo yenye maudhui yasiyowahusu.

VIJIJI 10 VYAPATA MAFUNZO YA HAKI ZA ARDHI IRINGA

WAJUMBE wa kamati za uamuzi za vijiji 10 vya wilaya za kilolo na Mufindi mkoani Iringa wamepata mafunzo ya haki za ardhi na utawala yatakayowaongezea uelewa juu ya sheria za ardhi, haki za ardhi kwa wanawake na makundi maalum pamoja na utatuzi wa migogoro ya ardhi.

Mafunzo hayo yaliyofanywa kwa siku nne katika kila wilaya yametolewa na mtandao wa Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali yanayofanya kazi na wakulima na wafugaji wadogo nchini Tanzania (PELUM Tanzania).

Afisa Mradi wa PELUM Tanzania, Angolile Rayson alivitaja vijiji hivyo kuwa ni pamoja na Ikuka, Mbigili, Mawala, Mawambala na Masalali kwa upande wa wilaya ya Kilolo na  Isaula, Magunguli, Makungu, Usokami na Ugesa kwa upande wa wilaya ya Mufindi.

Alisema mafunzo hayo yanatolewa kupitia mradi wa kuhusisha jamii ya vijijini katika uwajibikaji wa masuala ya ardhi ya kijiji unaojulikana kwa jina la CEGO unaotekelezwa kwa uratibu wa mtandao huo na ufadhili kutoka shirika la kimataifa la maendeleo la Marekani (USAID).

Rayson alisema mradi huo wa miaka minne ulianza kutekelezwa mwaka 2013 ukihusisha pia vijiji vingine 20 vya wilaya nne katika mikoa ya Morogro na Dodoma. “Shughuli kuu za mradi huo ni kuongeza na kuimarisha uelewa wa haki za ardhi kwa wananchi wa vijijini pamoja na viongozi wao kupitia mafunzo, machapisho  na mijadala mbalimbali,” alisema.

Alisema lengo likiwa ni kuhakikisha kunakuwepo na matumizi mazuri na endelevu ya ardhi ya kijiji kwa ajili ya uhakika wa chakula na kipato kwa wananchi. Akifunga mafunzo hayo wilayani Mufindi juzi, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Isaya Mbenje alisema ardhi ni mojawapo ya rasimilali muhimu sana kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika nchi.

“Hivyo ni muhimu kwa jamii yetu kuwa na uelewa wa kutosha juu ya sera na sheria za ardhi ili ardhi ya Tanzania itumike kwa manufaa ya watanzania wote na kwa usawa,” alisema.

Akiishukuru PELUM Tanzania kwa kuleta mradi huo mkoani Iringa, Mbenje ili matumizi yake yawe endelevu ni muhimu wananchi vijijini wakaijua Sheria ya ardhi namba 4 na 5 ya mwaka 1999.

“Na ni muhimu uelewa wa viongozi juu ya majukumu yao katika usimamizi wa ardhi ya kijiji, na utatuzi wa migogoro ya ardhi kwa njia ya amani pasipo kuvunja mahusiano mazuri baina ya watumiaji wa ardhi ukaongezeka,” alisema.

Awali mmoja wawashiriki wa mafunzo hayo, Festo Katingasa wa kijiji cha Usokami, Mufindi alisema mafunzo ya matumizi bora ya ardhi waliyopata kupitia mradi huo atayatumia kusaidia utatuzi wa migogoro ya ardhi katika kijiji chake. “Chanzo cha migogoro mingi ya ardhi katika kijiji chetu ni ukosefu wa hati miliki za ardhi inayoonesha mipaka aya ardhi kwa matumizi mbalimbali,” alisema.

Naye Salima Nyato wa kijiji cha Magunguli alisema kwa miaka mingi wanawake wamekuwa wakikosa haki ya kumiliki ardhi na kwamba mafunzo hayo yatawasaidia kuipata haki hiyo.

WAZIRI KAIRUKI AFUNGA MAADHIMISHO YA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA 2016 MKOANI DODOMA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah Kairuki (Mb) akitoa ufafanuzi kuhusu hoja zilizowasilishwa na Watumishi wa Umma mkoani Dodoma wakati wwa kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2016
Watumishi wa Umma mkoani Dodoma wakisikiliza Hotuba ya Waziri wa Nchi-Utumishi na Utawala Bora Mhe. Angellah Kairuki (Mb)
  Waziri wa Nchi-Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah Kairuki (Mb), katikati akisikiliza hoja za Watumishi wa Umma mkoani Dodoma. Kulia ni Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Jordan Rugimbana na kushoto, Katibu Tawala wa Mkoa huo Bi. Rehema Madenge.
Mmoja wa watumishi akiwasilisha hoja kuhusu madai mbalimbali ya watumishi.
Katibu wa Chama Cha Walimu (CWT)-Chunya Mbeya Bw.Sauli George akiwasilisha hoja.
Bw. Richard Kasogoto akiwasilisha hoja kuhusu watumishi kuonewa maeneo ya kazi.

KARATE CLUB OF JUNDOKAN SO HONBU SYSTEM TANZANIA YAPATA USAJILI NCHINI

Na Zainab Ally Khamis 
Dar es salaam School of Journalism(DSJ)

Habari za uhakika zimetufikia kuwa chama cha Karate club of Jundokan So Honbu System Tanzania kimepata usajili.
 
Tanzania itasonga mbele na kushika nafasi za kimataifa baada ya usajili huo kwani Mkufunzi mkuu au Chief instructor wa chama hicho anayetambuliwa kimataifa na baraza la dunia la karate lenye makao yake Okinawa Japan Sensei Rumadha Fundi, mwenye uzoefu wa vyama vitatu vya Goju Ryu tofauti, pia, alithibitisha hayo baada ya kupata msaada mkubwa chini ya watu walio karibu sana nae ambao pia imekuwa ni nguvu kubwa inayo mpa moyo wa kuwa na mfumo huo asilia toka visiwa vya Okinawa, Japan.

Jundokan So Honbu, ni mfumo unaofundisha mtindo wa Okinawa Goju Ryu katika utamaduni na utaratibu uliyowekwa na Master Chojun Miyagi na kusambazwa na mwanafunzi wake ambaye ni mwanzilishi wa JUNDOKAN, Master Eiichi Miyazato 1957, huko wilaya ya Asato,mji wa Nana, katika kisiwa cha Okinawa, Japan.

Maana ya Jundokan " Sehemu ya mafundisho us mwanzilishi"JUN +DO+ KAN, "jun"ni imechuliwa toka jina la mwanzilishi wa Goju Ryu, Chojun na "Do" ikimaanisha mwenendo, " Kan" ikimaanisha shule au mafunzo.
Hivyo ndivyo hasa lengo kuu la mfumo huu asilia usio badilishwa au kugeuzwa jinsi unavyofundishwa tokea ulipo undwa na Master Miyagi.

Mipango ipo njiani kuwa na tawi lenye lengo na nia kufuata sheria na kanuni za mfumo asilia tu, bila kubadilisha mbinu na "Kata" kama jinsi inavyo bainika na mbinu za " Sports Karate" hasa uchezaji wa "kata" kiujumla.
Hivi karibuni, huko visiwani Okinawa katika makao makuu ya tawi hilo, jumuiya ya sanaa ya mapambano " Okinawan BUDOKAN & Karate Federation", imeitambua "Jundokan So Honbu" kama moja ya mitindo asili"Original" kutoka Okinawa inayozingatia maadili na mafunzo yaliyo achwa na mua sisi wa mtindo wa Okinawa Goju Ryu.

Pindi mnamo miezi ijayo, tutatoa taarifa ya ufunguzi rasmi wa shule ya karate na uteuzi wa wanafunzi wa kuu wasaidizi ambao Sensei Rumadha atajitoa muhanga kuwasaidia kimbinu na ubora wa umahili wa mtindo huu na kuhakikisha mnamo muda wa miaka michache wanapata fursa ya kuwa walimu ( sensei) na kusambaza JUNDOKAN SO HONBU Tanzania yote.
 
"Msingi tunao mzuri na imara kwa wengi wataojumuika nami kuendeleza hii sanaa hapa nyumbani Tanzania", alisema Sensei Rumadha mwenye uzoefu wa mafunzo hayo ya karate zaidi ya miaka 37 chini ya " ma-sensei" wakuu toka pande zote za dunia, hasa toka Okinawa, Japan.

Bodi ya Filamu yakutana na wadau wa filamu katika kuadhimisha wiki ya Utumishi wa Umma


Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Bi Joyce Fisso (kushoto) akizungumza na wadau wa filamu (hawapo pichani) kujadili changamoto na namna ya kuendeleza tasnia ya filamu nchini ikiwa ni utaratibu wa kukutana na wadau hao kusikiliza changamoto zao na kuzipatia ufumbuzi ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma, kulia ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Genofeva Matemu. Mwanasheria wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bw. Patrick Kipangula (kulia) akifafanua hoja za kisheria katika kikao kati ya Bodi ya Filamu Tanzania na wadau wa filamu nchini ikiwa ni utaratibu wa kukutana na wadau hao kusikiliza changamoto zao na kuzipatia ufumbuzi ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma.
Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) Bw.Simon Mwakifwamba akichangia hoja katika kikao kati ya Bodi ya Filamu Tanzania na wadau wa filamu nchini ikiwa ni utaratibu wa kukutana na wadau hao kusikiliza changamoto zao na kuzipatia ufumbuzi ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya Utumishi. Muandaaji na msanii wa filamu nchini Bw. William Mtitu akichangia hoja katika kikao kati ya Bodi ya Filamu Tanzania na wadau wa filamu nchini ikiwa ni utaratibu wa kukutana na wadau hao kusikiliza changamoto zao na kuzipatia ufumbuzi ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma.
Mmoja ya wadau wa filamu Bw. Hussein Kimu akichangia hoja katika kikao kati ya Bodi ya Filamu Tanzania na wadau wa filamu nchini ikiwa ni utaratibu wa kukutana na wadau hao kusikiliza changamoto zao na kuzipatia ufumbuzi ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma.Picha zote na Shamimu Nyaki WHUSM

WAZEE JIMBO LA KIWAJUNI ZANZIBAR KUPATA HUDUMA YA MATIBABU BURE


Mbunge wa Jimbo la Kikwajuni ambae pia ni Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni(kulia), akimsikiliza mmoja wa wananchi wa Jimbo hilo mara baada ya kutoa muda wa kusikiliza kero mbalimbali za wananchi wakati wa mkutano uliofanyika Ofisi ya Jimbo hilo, Zanzibar. 

Mbunge wa Jimbo la Kikwajuni ambae pia ni Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, akizungumza na wananchi wa Jimbo hilo wakati wa mkutano uliofanyika katika Ofisi ya Jimbo ambapo alitoa taarifa juu ya watu wazima kuanzia umri wa miaka 70 kupata huduma ya matibabu bure. 


Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Tawi la Zanzibar, Ismail Kangeta, akitoa ufafanuzi juu ya huduma ya matibabu itakayoanza kutolewa bure kwa wananchi wa Jimbo la Kikwajuni, wakati wa mkutano uliofanyika Ofisi ya Jimbo.Wapili ni Mbunge wa Jimbo la Kikwajuni ambae pia ni Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni. Mwakilishi wa Jimbo la Kikwajuni, Nassor Salim Jazeera (kulia), akimsikiliza mwananchi wa Jimbo hilo mara baada ya kutoa muda wa kusikiliza kero mbalimbali za wananchi wakati wa mkutano uliofanyika Ofisi ya Jimbo hilo, Zanzibar.
Wananchi wa Jimbo la Kikwajuni, Zanzibar wakimsikiliza Mbunge wa Jimbo la Kikwajuni ambae pia ni Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (hayupo pichani) wakati akizungumza katika mkutano uliofanyika katika Ofisi ya Jimbo ambapo alitoa taarifa juu ya watu wazima kuanzia umri wa miaka 70 kupata huduma ya matibabu bure. Mwananchi wa Jimbo la Kikwajuni akisoma kipeperushi kilichotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ambacho kina majina ya Hospitali ambazo wafaidika wa huduma ya matibabu bure wanaweza kwenda kupata huduma hiyo wakati wa mkutano uliofanyika Ofisi ya Jimbo hilo Kikwajuni Zanzibar.

(Picha na Mpiga Picha Wetu)

MAOMBI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU 2016/2017.

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Inapenda kutoa taarifa kwa Umma na wadau wake wote kuwa inatarajia kuanza kupokea maombi ya Mikopo kwa mwaka wa masomo 2016 /2017 kuanzia tarehe 27 Juni 2016 hadi tarehe 31 Julai 2016.

Katika kipindi hicho waombaji wa mikopo watarajiwa wanapaswa kusoma mwongozo wa utoaji mikopo na ruzuku uliopo kwenye tovuti ya Bodi www.heslb.go.tz ili kufahamu sifa za mwombaji na taratibu kufuata kabla ya kuomba mikopo kwa njia ya mtandao.

Utoaji wa Mikopo unaongozwa na Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya juu Na. 9 ya 2004 (kama ilivyorekebishwa) hususani vifungu vyake vya 16 na 17.

Kwa taarifa hii, waombaji wote wa mikopo wanatakiwa kusoma mwongozo huo kabla ya kujaza maombi ya mikopo na wazingatie kuwa tarehe ya mwisho ya kuomba mikopo ni Julai 31, 2016.

IMETOLEWA NA:
KITENGO CHA HABARI, ELIMU NA MAWASILIANO
BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU
TAREHE 24 JUNI 2016.

 
Nafasi Ya Matangazo