JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


Benki ya CRDB yaadhimisha Siku ya Wajasiriamali Duniani ikitooa Shilingi Bilioni 995 mpaka Mei 2024

Share This
Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa Benki ya CRDB, Bruce Mwile (kulia) akiwa pamoja na Mkurugenzi wa Wateja wa Awali na Kati wa Benki ya CRDB,  Bonaventure Paul wakizindua rasmi Akaunti ya Biashara  'CRDB Biashara Account' kwenye hafla ya maadhimisho ya Siku ya Wajasiriamali Duniani iliyofanyika kwenye makao makuu ya benki hiyo, jijini Dar es salaam Juni 27, 2024.
Dar es Salaam. Tarehe 27 Juni 2024: Benki ya CRDB imeungana na wadau wengine kuadhimisha Siku ya Wajasiriamali Duniani (International MSME Day) kwa kuendesha semina kwa wateja wake na baadhi ya wabia wa kimkakati.

Sherehe za maadhimisho hayo zimefanyika makao makuu ya Benki ya CRDB zikifunguliwa na Afisa Mkuu wake wa Uendeshaji, Bruce Mwile aliyesema kuwa kipaumbele chao siku zote ni kumhudumia Mtanzania na kuhakikisha anaboresha maisha yake kwa kumpa huduma zinazoendana na kukidhi mahitaji yake.
Ili kukuza ujasiriamali, Mwile amesema Benki ya CRDB inatambua kuwa shughuli zake zikichangia asilimia 27 ya Pato la Taifa na ili itoe mchango wake ipasavyo kunahitajika huduma na mifumo shirikishi itakayowasaidia wajasiriamali kuyafikia malengo waliyojiwekea.

“Kutokana mikakati tuliyojiwekea, Benki yetu imekuwa kinara katika uwezeshaji wajasiriamali kwani hadi Mei 2024 tulikuwa tumetoa zaidi ya shilingi bilioni 995.346 kwa zaidi ya wajasiriamali 21,470 katika sekta mbalimbali ikiwamo sekta ya kilimo, ujenzi na makazi, miundombinu, usafirishaji, afya, elimu, nishati, madini, biashara na viwanda, pamoja na uchumi wa buluu ili kuimarisha shughuli zao,” amesema Mwile.

Mwile amesema sekta ya ujasiriamali imekuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi wa mataifa mengi duniani kwa kuchochea ubunifu na uanzishaji biashara mpya ambazo huongeza ajira na kuimarisha kipato cha watu binafsi na jamii kwa ujumla. 
“Kwa kuanzisha biashara ndogo na za kati, wajasiriamali huchangia moja kwa moja kwenye ukuaji wa pato la Taifa na kuongeza mapato ya serikali kupitia kodi. Sekta hii pia ina mchango mkubwa katika kuboresha teknolojia na kuongeza ufanisi katika uzalishaji wa bidhaa na huduma, hivyo kufanya uchumi kuwa na ushindani zaidi kimataifa,” amesema Mwile.

Taarifa za Umoja wa Mataifa (UN) zinasema wajasiriamali ni injini muhimu ya kufanikisha utekelezaji wa Maendeleo Endelevu (SDG) kwani kundi hili linachangia asilimia 90 ya biashara zote zilizopo duniani ambazo hutoa kati ya asilimia 60 mpaka 70 ya ajira zenye staha na kuchangia zaidi ya nusu ya pato la dunia. Tanzania kuna zaidi ya biashara ndogo za ujasiriamali milioni 3 zinazowapa uhakika wa kipato wamiliki wake.
Ili kumkuza mjasiriamali kuanzia ngazi ya chini kabisa, Mwile amesema Taasisi ya CRDB Bank Foundation ambayo ni kampuni tanzu ya Benki ya CRDB inatekeleza programu ya Imbeju inayotoa  elimu ya ujasiriamali na fedha kwa wanawake na vijana pamoja na kuwapa mitaji wezeshi inayoanzia shilingi 100,000. Hadi sasa tayari programu hiyo imewafikia wajasiriamali zaidi ya 400,000 na kutoa mitaji wezeshi zaidi ya shilingi bilioni 10.

Sambamba na maadhimisho hayo, Benki ya CRDB imezindua ‘CRDB Biashara Account’ ambayo ni mahsusi kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo wenye malengo ya kukuza miradi yao ili kuongeza idadi ya wateja wanaowahudumia, kukuza mapato yao ili wakue zaidi na kuanzisha kampuni kubwa zitakazohudumia nchi nzima hata nje ya mipaka pia.
Akizungumza kwenye mjadala uliofanyika katika maadhimisho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Royal Mark, Johnson Kapira amesema kwa Mtanzania kuwa masikini kunatokana na kutokuwa na ujasiri wa kufanya uamuzi binafsi wa kuzichangamkia fursa zilizopo.

Akieleza jinsi alivyoanza mwanzoni mwa miaka ya 1990 baada ya kuhitimu chuo kikuu, amesema kutokana na changamoto za kupata ajira zilizokuwapo alianzisha kampuni yake na akawa anaomba mikopo ya kufanikisha kazi alizokuwa anazipata na mpaka sasa anakopesheka kiasi kikubwa zaidi.

“Nilianza nikiwa mfanyabiashara mdogo sana. Nilianza biashara mwaka 1995 nikiomba zabuni serikalini na kampuni binafsi. Mtaji ulikuwa changamoto lakini Benki ya CRDB imenikuza hasa huduma yake ya Purchase Order Agreement. Leo hii naweza kukopa mpaka shilingi bilioni nne,” amesema Kapira.
Naye Josephat Kibwanga ambaye naye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Qualitas amesema: “Mimi ni mteja mkubwa wa Benki ya CRDB. Mikopo yao imeniwezesha kuimarisha huduma katika hospitali yangu na kwa sasa utakuwa muujiza iwapo mgonjwa atakuja hospitalini kwetu na akaambiwa hakuna dawa. Haya yote yamewezekana kutokana na mikopo inayopatikana kwa wakati kutoka Benki ya CRDB.”

Maneno ya wajasiriamali hao yana akisi kile alichokisema Mwile wakati akifungua maadhimisho hayo aliposema: “Leo hii tukiwa tunaadhimisha Siku ya Wajasiriamali Duniani niwahakikishie kuwa Benki yetu ya CRDB itaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuwawezesha wajasiriamali na biashara changa, ndogo na za kati nchini tukiamini kwa kufanya hivyo tunachochea ongezeko la ajira, kuimarisha kipato binafsi na kukuza uchumi wa Taifa letu kwa ujumla wake. Ahadi yetu ni kwamba tupo tayari kuwahudumia na kutembea nanyi katika safari yenu ya mafanikio.”
Mkurugenzi wa Wateja wa Awali na Kati wa Benki ya CRDB,  Bonaventure Paul akizungumza katika hafla ya uzinduzi rasmi wa Akaunti ya Biashara  'CRDB Biashara Account' iliyoenda sambamba na maadhimisho ya Siku ya Wajasiriamali Duniani iliyofanyika kwenye makao makuu ya benki hiyo, jijini Dar es salaam Juni 27, 2024.



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad