728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Thursday, September 29, 2016

  PATO LA TAIFA LAKUA KWA ASILIMIA 7.9-NBS.

  Mkurugenzi Mkuu wa  Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo.

  Mkurugenzi Mkuu wa  Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, kuhusu hali ya pato la Taifa kwa robo ya pili  kuanzia Aprili hadi Juni 2016 jijini Dar es Salaam leo. Kushoto ni Meneja wa Takwimu za Pato la Taifa, Daniel Masolwa na kulia ni Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi, Joyce Sawe.
  Baadhi ya Viongozi mbalimbali wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa  Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo.
  Picha na Avila Kakingo, Globu ya Jamii. 

  PATO la Taifa limeendelea kukua kwa asilimia 7.9 katika kipindi cha mwezi Aprili hadi Juni 2016 ikilinganishwa na kasi ya asilimia 5.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2015.

  Takwimu hizo zimetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa  Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya pato la Taifa kwa robo ya pili  kuanzia Aprili hadi Juni mwaka 2016.

  Dkt Chuwa  alisema kuwa ukuaji wa pato la Taifa umetokana na shughuli za kiuchumi ikiwemo kilimo, mifugo, misitu na uvuvi ambapo shughuli  hizo zilikuwa kwa asilimia 3.2 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 1.9 katika kipindi kama hicho mwaka 2015.

  Kwa upande wa shughuli za uchumi za viwanda na ujenzi, Dkt. Chuwa alisema kumekuwa na ongezeko la asilimia 20.5 katika kipindi hicho ukilinganisha na ukuaji wa asilimia 11.2 mwaka 2015 katika shughuli za uchimbaji madini, mawe na kokoto.

  Aidha katika shughuli za uzalishaji bidhaa na viwanda kumeongeza kwa asilimia 9.1 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2016 ukilinganisha na kasi ya asilimia 5.2 ya mwaka 2015.

  Katika shughuli za uchukuzi na uhifadhi, Dkt Chuwa alisema kuwa shughuli hizo zimekuwa kwa kiwango cha asilimia 30.6 zimetokana na usafirishaji wa abiria kwa njia ya reli na barabara ikiwa ni pamoja na usafiri wa UDART.

  Hata hivyo katika shughuli za fedha na bima ziliongezeka kwa kasi ya asilimia 12.5 ikilinganishwa na asilimia 10.0 iliyopatikana katika kipindi kama hicho mwaka 2015.

  Wakati huo huo huduma za elimu zilikuwa kwa kasi ya asilimia 8.0 katika robo hiyo ya mwaka ikilinganishwa na aslimia 7.4 ya kipindi kama hicho kwa mwaka 2015 ambapo ukuaji wa shughuli hii imetokana na ongezeko la wanafunzi waliodahiliwa mwaka 2016.

  Mbali na hayo pato la Taifa kwa nchi za Afrika ya Mashariki zimechambua na kutoa tathimini hiyo katika kipindi kinachoishia Juni 2016, ambapo Rwanda imeendelea kukuwa kwa asilimia 5.4 ukilinganisha na asilimia 7.2 ya miezi kama hiyo mwaka 2015, kwa upande wan chi za Kenya, Uganda na Burundi zinaendelea na uchambuzi wa takwimu hizo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: PATO LA TAIFA LAKUA KWA ASILIMIA 7.9-NBS. Rating: 5 Reviewed By: MICHUZI BLOG
  Scroll to Top