JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


BASATA YAWAPIGA MSASA VIONGOZI WA VYAMA VYA WASANII

Share This
 Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Bw. Godfrey Mngereza (Kulia) akisisitiza jambo wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi wa vyama vya wasanii yaliyoandaliwa na Baraza hilo mapema wiki hii. Kulia kwake ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utamaduni anayeshughulikia Lugha kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bi. Shani Kitoga
 Msanii mkongwe wa Sanaa za Maonesho Bw. Kassim Mbelemba maarufu kwa jina la Mzee Jangala akipokea cheti chake kutoka kwa Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utamaduni anayeshughulikia Lugha kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bi. Shani Kitoga baada ya kumaliza mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi wa vyama vya wasanii yaliyoandaliwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) mapema wiki hii.  
 Mwezeshaji wa mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi wa vyama vya Wasanii katika eneo la Hakimiliki na Hakishiriki Bw. John Kitime akipokea zawadi kutoka kwa mmoja wa viongozi wa vyama vya wasanii baada ya kutoa mafunzo kwa viongozi hao. 
Viongozi wa vyama vya Wasanii walioshiriki mafunzo ya Kujengewa Uwezo wakiwa kwenye picha ya pamoja na mgeni rasmi Bi. Shani Kitoga
IMETOLEWA NA KITENDO CHA HABARI NA MAWASILIANO, BASATA.

BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) limewapa mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo katika maeneo mbalimbali viongozi wa vyama na taasisi zinazojihusisha na wasanii ili kujenga ufanisi zaidi katika sekta ya Sanaa.

Mafunzo hayo yaliyofanyika kwa siku tatu kuanzia Jumanne hadi Alhamisi ya wiki hii yalijikita katika kuwajengea uwezo Wasanii kwenye maeneo ya uandaaji bajeti, uandaaji wa mipango mikakati na sheria ya hakimiliki na hakishiriki na mikataba kwenye kazi za Sanaa. 

Akizungumza kwenye hafla ya kuyafunga mafunzo hayo, Katibu Mtendaji wa BASATA Godfrey Mngereza alisema kwamba ana matumaini makubwa kwamba mafunzo haya kwa viongozi wa wasanii yataamsha ari katika utawala na utendaji wa sekta ya Sanaa na kufanikisha kupiga hatua kwa sekta hii muhimu.

“Nina imani katika mafunzo haya tutawaona viongozi wa wasanii mnakuwa na mipango ya muda mrefu, wa kati na mfupi maana hakuna jinsi tunaweza kuwaongoza wasanii bila kuwa na mipango” alisisitiza Mngereza.

Kuhusu suala la hakimiliki, hakishiriki na mikataba kwenye kazi za Sanaa  alisema kuwa ni tatizo linalowakumba wasanii wengi hivyo imani ya BASATA ni kuona viongozi hawa waliopatiwa mafunzo wanakuwa msaada kwa wasanii walio chini ya vyama vyao.


“Suala la hakimiliki linamgusa kila msanii, naamini kwenye suala hili mmejifunza vya kutosha. Aidha, mmejifunza suala la mikataba katika kazi za Sanaa, nawaomba muwe mabalozi katika kuwaelimisha wasanii umuhimu wa mikataba katika kazi wanazozifanya” Aliongeza Mngereza.

Awali akiongea kabla ya kukabidhi vyeti kwa washiriki, mgeni rasmi ambaye alimwakilisha Mkurugenzi wa Idara ya Utamaduni kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bi. Shani Kitoga aliwataka viongozi hao kuzingatia mafunzo waliyoyapata na kuhakikisha wanakuwa mabalozi wa mabadiliko kwenye sekta ya Sanaa.

“Sanaa tunasema ni kazi hivyo lazima mafunzo haya mliyoyapata myatafsiri katika vitendo kwa kuonesha utendaji kazi ulio bora na unaozingatia mipango” alisema Bi. Kitoga.

Akiongea kwa niaba ya viongozi wa wasanii zaidi ya arobaini (40) waliohudhuria mafunzo hayo, Msanii mkongwe wa Sanaa za Maonesho Kassim Mbelemba maarufu kwa jina la Mzee Jangala alilipongeza BASATA kwa kuandaa mafunzo hayo na kuwaeleza wasanii kuwa sasa hakuna sababu ya kulalamika bali kuyafanyia kazi yale waliyojifunza.

Mafunzo haya ambayo ni sehemu ya kutekeleza mpango mkakati wa BASATA yaliwezeshwa na wakufunzi Rashid Masimbi ambaye ni mtaalam wa kuandaa mipango mikakati, Mrisho Mtumwa ambaye ni mtaalam wa kuandaa bajeti na John Kitime ambaye ni Msanii na mtaalam wa masuala ya hakimiliki na hakishiriki. 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad