bashiryakub.blogspot.com
Na Bashir Yakub.
MARA kadhaa migomo ya wafanyakazi imekuwa ikizaa athari mbaya kwao. Hii ni kutokana na kugoma bila kufuata taratibu. Waajiri wao ni wajanja. Huwa makini sana linapoibuka wazo la kugoma na huwa tayari muda woote kufuatilia nyendo ili panapo kosa kidogo watumie mwanya huo kuwadhibiti wagomaji.
Na kikubwa wanachofanya hali ikishakuwa hivi ni kusema mgomo haukuwa halali na hapo kupata nafasi ya kuwashugulikia waliohusika katika kugoma mmoja baada ya mwingine. Katika mazingira kama haya ni vema wafanyakazi kufahamu taratibu za kisheria zinazohusu mgomo ili wakati wa kufanya hivyo asitokee yeyote kati yao wa kuathiriwa na ugomaji huo.
1.SHERIA INAMRUHUSU MFANYAKAZI KUGOMA.
Wapo wanaodhani kugoma ni uasi. Kwa mfanyakazi hili si kweli. Kugoma ni haki ya mfanyakazi kama zilivyo haki nyingine. Kama ilivyo haki ya kupokea mshahara, haki ya kulipwa muda wa ziada, haki ya muda maalum wa kufanya kazi, likizo na haki nyinginezo kwa ujumla wake. Kugoma si dhambi isipokuwa takwa halali la kisheria. Kitaalam mgomo wa wafanyakazi huitwa “strikes” . Ni hatua ambapo wafanyakazi hugomea kuingia maeneo ya kazi au huingia maeneo ya kazi lakini wasitoe huduma kama ilivyo ada yao.
Kisheria kugoma ni jukwaa la kuitisha mjadala wa kujadii maslahi ya kazi kati ya mwajiri na mwajiriwa. Kugoma ni Jambo halali kisheria ndicho ninachotaka kusema na kuwatoa hofu baadhi wajuao kugoma ni uasi na usaliti.Na haya ni kwa mujibu wa kanuni namba ya 42,sheria namba 6 ya ajira na mahusiano kazini.
2. WAFUATAO HAWARUHUSIWI KUGOMA.
Makundi ya wafanyakazi watoao huduma muhimu katika jamii migomo kwao imeharamishwa. Huduma muhimu katika jamii hutegemea na mahitaji ya jamii husika. Yumkini hapa kwetu huduma muhimu katika jamii hujumuisha watumishi katika idara za afya, maji safi na salama, nishati na umeme, vyombo vya ulinzi na usalama, zimamoto na watoa huduma ya kuongoza ndege. Sababu kubwa za kuzuia makundi haya kugoma ni kuwa kugoma kwao huweza kuleteleza hasara ambazo kwazo haziwezi kufidiwa na kitu chochote baada ya kutokea kwake. Na hasara kubwa zaidi hapa ni vifo na ulemavu wa kudumu vitu ambavyo haviwezi kufidiwa kwa namna yoyote na kitu chochote .
3. WANAOTAKA MGOMO HALALI WAFUATE UTARATIBU HUU.
( a ) Kwanza kabisa hakikisheni mgomo wenu unahusu maslahi ya kazi yenu. Usiwe mgomo ambao nyuma yake wako watu hasa wanasiasa wanaowasukma ili kutimiza haja zao fulani. Au usiwe mgomo ambao umeandaliwa lengo likiwa kumkomoa mwajiri. Ni lazima kuwepo na nukta muhimu na ya wazi kabisa inayohusu maslahi katika kazi yenu.
( b ) Kabla ya kugoma lazima muwe mmepitia hatua ya usuluhishi( mediation). Na mnapokuwa mmepitia hatua hii ni lazima iwe imethibitika kuwa hatua hiyo imeshindwa kutatua mgogoro wenu na sasa hatua inayofuata ni ya kugoma. Ikiwa hatua ya usuluhishi imefanikiwa na kutoa majawabu ya mgogoro itakuwa ni haramu kwa yeyote kugoma. Kugoma ni pale tu hatua ya usuluhishi inaposhindwa na hatua hii hutakiwa kuchukua muda wa siku thelathini. Ni muda huo utakaotumika kutafuta muafaka kabla ya kutangaza mgomo.
( c ) Ikiwa mgomo utakuwa umeitishwa na chama cha wafanyakazi basi kura za wengi ndizo zitakazotoa ruhusa ya kugoma. Ikiwa wengi watakataa basi hakuna mgomo.
( d ) Baada ya usuluhishi kushindikana wafanyakazi wanaolenga kugoma watatakiwa kutoa taarifa(notice) ya masaa 48 sawa na siku mbili kwa mwajiri kabla ya kuanza kugoma. Ni baada ya muda huo ndipo mgomo utaanza.
( e ) Ikiwa mgomo utaahirishwa baada ya masaa 48 yaliyokuwa yametangazwa kupita, basi kama mnatarajia kuendelea na msimamo wa kugoma mtatakiwa kutoa muda mwingine wa masaa 48.
Kama wafanyakazi watafuata utaratibu huu kugoma hakuna madhara yoyote mabaya yatakayotokea kwao ikiwa ni pamoja na kutishiwa kufukuzwa kazi.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE , GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO. 0784482959, 0714047241 bashiryakub@ymail.com
No comments:
Post a Comment