JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


WAZIRI MKUU AKABIDHI MAGARI YA KUBEBA WAGONJWA

Share This
 WAZIRI MKUU Mizengo Pinda(Pichani) amekabidhi magari mawili ya kubeba wagonjwa yenye thamani ya sh. milioni 150 kwa uongozi wa Wilaya ya Ngorongoro ili yapelekwe kwenye kituo cha afya cha Enduleni na hospitali ya Wasso ambayo inatumika kama hospitali ya wilaya.

Waziri Mkuu amekabidhi magari hayo ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa Septemba 2013 alipofanya ziara ya kikazi ya mkoa wa Arusha na kubaini adha ya usafiri iliyokuwa ikiwapata wakazi wa kata za Wasso na Enduleni zilizoko wilayani Ngorongoro.

Akizungumza na watumishi wa idara ya afya na wananchi waliohudhuria makabidhiano hayo leo mchana, (Jumanne, Septemba 8, 2015), Waziri Mkuu alisema aliyapata magari hayo kwa wafadhili kutoka Japan na sehemu nyingine ambayo haikuitaja.

“Nikiwa ziarani Japan, Machi mwaka huu, nilikutana na Watanzania waishio Japan nikawaomba kama wanaweza kunisaidia gari la wagonjwa hata kama limetumika sababu najua kule magari yaliyotumika huwa yanakuwa hayajachoka. Watanzania wale walikubali na kuamua kunisaidia kutekeleza ahadi yangu,” alifafanua Waziri Mkuu.

Alisema mara baada ya ziara yake, alipeleka maelekezo ya kupata magari kwa ajili ya Wasso na Enduleni kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii lakini kutokana na upatikanaji mgumu wa fedha za bajeti, ombi hilo halikufanikiwa ndipo akaona atafute njia nyingine ya kuwasaidia wakazi hao.

“Ahadi ya Serikali ya kuwapatia gari la wagonjwa wakazi wa Wasso na Enduleni bado iko palepale lakini niliona ni vema wakati wakiendelea kusubiri fedha zipatikane, bora tutafute njia nyingine ya kuwasaidia kupunguza tatizo la usafiri kwa wagonjwa linalowakabili wakazi hao,” aliongeza.

Waziri Mkuu alikabidhi funguo za magari hayo mawili kwa Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Bw. Hashim Mgandilwa pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Bw. John Kurwa.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Felix Ntibenda Kijiko na viongozi wengine wa mkoa wa Arusha na waganga wakuu vituo vya Enduleni na Wasso.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, SEPTEMBA 8, 2015.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad