Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umeongeza ufanisi katika ulipaji wa madai ya vituo vya kutolea huduma za afya, ambapo muda wa wastani wa malipo umepungua kutoka siku 120 hadi siku 50, ikiwa ni miongoni mwa mafanikio ya miaka 25 ya Mfuko huo.
Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dkt. Irene Isaka, amesema hayo leo Novemba 6, 2026 jijini Dat ea Salaam, wakati wa mkutano na wahariri wa vyombo vya habari ulioratibiwa na ofisi ya msajili wa hazina, akieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na kuboresha usimamizi wa rasilimali na kudhibiti matumizi.
Amesema katika kipindi hicho, mapato ya Mfuko yameongezeka kwa asilimia 10.3, huku matumizi yakipungua kwa asilimia 10. Aidha, uwiano wa matumizi ya matibabu ukilinganishwa na mapato umeshuka kutoka asilimia 87 hadi asilimia 71.
Dkt. Isaka amesema idadi ya wanachama wakuu imeongezeka kwa asilimia 17 na wategemezi kwa asilimia 6.2, huku mtandao wa vituo vya kutolea huduma za afya vinavyoshirikiana na NHIF ukifikia zaidi ya vituo 10,300.
Katika kuadhimisha miaka 25, NHIF imepanga maonesho ya siku saba katika viwanja vya Kinangari, Dodoma, kuanzia Novemba 23 hadi 29, 2026, pamoja na mbio za marathon zinazotarajiwa kushirikisha zaidi ya watu 10,000.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, ameipongeza NHIF kwa kutambua mchango wa wanahabari katika kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa bima ya afya.
Balile amesema nafasi 100 za bima ya afya zilizotolewa kwa wanahabari ni fursa muhimu, akishauri ziwanufaishe zaidi waandishi na wahariri walio kazini ambao hawana bima. Ameeleza kuwa TEF itashirikiana na NHIF kuweka utaratibu wa kuwapata wanahabari hao.
Naye Mratibu wa Elimu kuhusu Bima ya Afya kwa Wote kutoka Wizara ya Afya, Said Makora, amesema Serikali inaendelea kuongeza watumishi wa afya kujiandaa na mahitaji yatakayoongezeka wakati wa utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote.
Amesema kati ya ajira 5,000 zilizotolewa katika sekta ya afya, watumishi 808 wamepelekwa katika ngazi ya huduma za afya ya msingi, zikiwemo hospitali na vituo vya afya.
Hata hivyo, amesema bado kuna upungufu wa watumishi, huku Serikali ikiendelea na mikakati ya kuongeza wataalamu katika kada muhimu, ikiwemo huduma za mama na mtoto pamoja na matibabu ya saratani.


.jpeg)

.jpeg)


No comments:
Post a Comment