.jpeg)
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amehukumiwa kifungo cha miaka minne jela baada ya kupatikana na hatia ya kosa la uchochezi.
Hukumu hiyo imetolewa leo Novemba 6, 2026, na jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, likiongozwa na Jaji Dustan Ndunguru, akisaidiana na Majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji Ndunguru amesema Mahakama imezingatia hoja mbalimbali zilizowasilishwa na Lissu, ikiwemo hali yake ya kiafya, kuwa mkosaji wa mara ya kwanza na hoja kuhusu uwezekano wa kutoa adhabu ya faini badala ya kifungo.
Jaji Ndunguru amesema Kifungu cha 390 hakijaainisha adhabu, hivyo Mahakama imezingatia Kifungu cha 35 cha Kanuni ya Adhabu, kinachohusika pale ambapo kifungu husika hakijaainisha adhabu.
Amesema adhabu inayoweza kutolewa ni kifungo kisichozidi miaka mitano, faini au vyote viwili, huku akieleza kuwa Mahakama imepitia maamuzi mbalimbali kuhusu masuala yanayohusiana na kesi hiyo.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Lissu aliomba Mahakama izingatie kuwa hajawahi kutiwa hatiani kwa kosa lolote la jinai, akisema amekuwa akikabiliwa na mashtaka kwa zaidi ya miaka 24 tangu mwaka 2002 bila kupatikana na hatia.
Pia aliieleza Mahakama kuwa ana msiba wa mtu aliyemlea na kumsaidia kuwa mwanasheria, Mzee Alutte, ambaye ni kaka yake, na kwamba alitarajia kupata nafasi ya kwenda kumzika.
Lissu aliomba Mahakama izingatie kuwa amekaa gerezani kwa mwaka mmoja na miezi saba, akisema amekuwa akinyimwa fursa ya kuwasiliana na mawakili wake, viongozi wenzake wa Chadema na hata kuomba Mungu, kama ilivyoelezwa na jopo la majaji watatu katika uamuzi mwingine.
Aidha, aliieleza Mahakama kuwa hali yake ya kiafya si nzuri, akisema ana historia ya kufanyiwa operesheni 25, anaishi na risasi moja iliyoshindwa kutolewa mwilini kati ya risasi 16 alizopigwa, pamoja na kuwa na kisukari kwa miaka sita.
Alisema anatakiwa kwenda kupata matibabu katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Leuven nchini Ubelgiji, lakini amekosa miadi minne ya matibabu kutokana na kesi hiyo.
Katika hoja zake, Lissu pia aliomba Mahakama impe dhamana ili aweze kukata rufaa akiwa nje na kupata nafasi ya kushiriki mazishi ya kaka yake.
Akizungumzia hoja za upande wa mashtaka, Lissu alipinga kuhusishwa na vurugu za Oktoba 2025, akisema Mahakama haikuoneshwa ushahidi wa hotuba ya Jaji Chande wala Jaji huyo hakuitwa kutoa ushahidi kuthibitisha waliohusika na vurugu hizo.
Alisema pia kuhusishwa kwake na matukio yaliyotokea wakati akiwa gerezani ni hoja inayopaswa kuzingatiwa na Mahakama.
Hata hivyo, Mahakama imemhukumu kutumikia kifungo cha miaka minne jela, huku ikieleza kuwa ana haki ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.


No comments:
Post a Comment