
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Stanslaus Nyongo, amezindua maabara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Kibaha, mradi uliogharimu jumla ya Shilingi milioni 188, uliotekelezwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Capitalpay Foundation.
Akizungumza Novemba 11, 2026, wakati wa uzinduzi huo, Nyongo ameipongeza Capitalpay Foundation kwa kushirikiana na Serikali katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuimarisha matumizi ya teknolojia katika sekta ya elimu.
Aidha, ametoa wito kwa taasisi na wadau wengine wa maendeleo mkoani Pwani kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuchangia miradi ya maendeleo, hususan katika sekta ya elimu.
Amesema katika kipindi cha mwaka 2021/22 hadi 2025/26, Mkoa wa Pwani ulipokea jumla ya Shilingi bilioni 118.31 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu, ambapo utekelezaji wake umehusisha ujenzi wa shule mpya 75, zikiwemo shule 35 za Awali na Msingi na shule 40 za Sekondari. Shule hizo ni pamoja na Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Sayansi Bibi Titi Mohamed na Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Kanda Mkuranga Boys.
Aidha, Serikali imejenga jumla ya vyumba vya madarasa 1,889, vikiwemo 64 vya Elimu ya Awali, 809 vya Elimu ya Msingi na 1,016 vya Elimu ya Sekondari, pamoja na matundu ya vyoo, maabara, maktaba, mabwalo, mabweni na majengo ya utawala, sambamba na ukarabati wa miundombinu ya shule.
Mkuu wa Mkoa Pia amesisitiza umuhimu wa wazazi na walezi kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanandikishwa na wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka 2027 wanaripoti katika shule walizopangiwa.
Kwa upande wake Katibu tawala Mkoa wa Pwani Richard Kayombo shule hiyo imepata nafasi ya kipekee na kuwataka wanafunzi kutumia maabara hiyo kama nyenzo muhimu katika kuongeza tija kwenye masuala ya teknolojia.
Naye Mkurugenzi wa Taafisi ya Capital pay Foundation kwa upande wa Tanzania Isack Nchunda amesema maabara hiyo itawafanya wanafunzi kuwa wabuni katika teknologia za mifumo na kuahidi kuwa kwa wale watakaokuwa wabobezi wataweza kupata fursa za ajira katika taasisi hiyo.
Uzinduzi wa maabara hiyo ni sehemu ya ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo katika kuimarisha elimu na kuwawezesha wanafunzi kupata maarifa na ujuzi wa TEHAMA.


No comments:
Post a Comment