Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameielekeza Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kuongeza juhudi za kutafuta na kupanua masoko ya kimataifa kwa kubaini bidhaa zinazohitajika pamoja na viwango vya ubora vinavyotakiwa katika masoko hayo.
Amesema hatua hiyo itawasaidia wazalishaji nchini kuendana na mahitaji ya wanunuzi wa kimataifa, kuongeza ushindani wa bidhaa zao na kupanua mauzo nje ya nchi.
Makamu wa Rais ametoa maelekezo hayo wakati akitembelea mabanda ya Maonesho ya Kimataifa ya Biashara na Uwekezaji wa Mazao ya Bustani, HortiLogistica Africa 2026, katika viwanja vya TGT mkoani Arusha, kabla ya ufunguzi rasmi.
Katika ziara hiyo, amepongeza mchango wa sekta binafsi kupitia Chama cha Wakulima wa Mazao ya Bustani Tanzania (TAHA) katika kuwawezesha wakulima na wajasiriamali wadogo kushiriki katika uzalishaji na biashara ya mazao ya bustani.
Aidha, ameielekeza Wizara ya Kilimo kuongeza jitihada za kuendeleza kilimo cha parachichi kutokana na fursa zake katika kuongeza mapato ya fedha za kigeni. Ametaja maeneo ya kupewa msukumo kuwa ni uhifadhi wa mazao, uzalishaji wa miche bora na utoaji wa mafunzo kwa vijana ili kuwavutia wengi zaidi kushiriki katika kilimo hicho.
Akitoa mfano wa mafanikio ya vijana katika sekta hiyo, Makamu wa Rais ameeleza kuvutiwa na kampuni ya Onocado Farm, inayoongozwa na kijana ambaye, kupitia ushirikiano na TAHA, amefanikiwa kuingia katika kilimo cha parachichi na sasa anasafirisha nje ya nchi zaidi ya tani 430 kwa mwaka.
Amesisitiza umuhimu wa TANTRADE kuunga mkono ushiriki wa vijana katika kilimo kwa kuimarisha uunganishaji wao na masoko na kushirikiana na wadau katika mafunzo kuhusu mahitaji ya masoko na ubora wa bidhaa.
Ameeleza kuwa Serikali ikiunga mkono jitihada za vijana wanaojihusisha na uzalishaji, idadi ya wazalishaji itaongezeka na kuchangia ukuaji wa pato la Taifa.
HortiLogistica Africa 2026 inafanyika Novemba 8 hadi 10, 2026, katika viwanja vya TGT mkoani Arusha, kwa ushirikiano wa Serikali na wadau wa sekta ya mazao ya bustani, wakiwemo TAHA.
Jukwaa hilo linawakutanisha wakulima, wazalishaji, wafanyabiashara, wanunuzi, wasafirishaji, wawekezaji na watoa huduma za teknolojia kutoka Afrika na masoko ya kimataifa, kwa lengo la kufungua fursa za biashara, uwekezaji na ushirikiano.
Kupitia jukwaa hilo, Tanzania inalenga kuimarisha nafasi yake kama kitovu cha biashara na uwekezaji wa mazao ya bustani barani Afrika, huku ikipanua mchango wa sekta hiyo katika ajira, kipato cha wakulima na mapato ya fedha za kigeni.


.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)


.jpeg)



No comments:
Post a Comment