JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


KAMATI YA BUNGE YAWABANA WAKANDARASI, YATAKA MIRADI YA DAR ES SALAAM IKAMILIKE KWA WAKATI

Share This

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeitaka Serikali kuimarisha usimamizi wa wakandarasi wanaotekeleza miradi ya miundombinu jijini Dar es Salaam ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyokubaliwa katika mikataba.

Kamati hiyo imeridhishwa na kasi ya utekelezaji wa ujenzi wa Daraja la Jangwani, huku ikitaka kasi zaidi katika utekelezaji wa miradi ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) Awamu ya Nne.

Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua miradi hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Selemani Moshi Kakoso, ameitaka Serikali kuondoa changamoto zinazokwamisha utekelezaji wa miradi na kuwawajibisha wakandarasi wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa mikataba.

Kakoso amesema Kamati imeridhishwa na usimamizi wa mradi wa ujenzi wa Daraja la Jangwani unaogharimu takribani Shilingi bilioni 97, lakini amesisitiza umuhimu wa kuimarisha usimamizi ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati na ubora unaotakiwa.

Aidha, ameitaka Serikali kuhakikisha wakandarasi wanaongeza nguvu kazi, wataalamu, mitambo na muda wa kazi ili kuharakisha utekelezaji wa miradi hiyo.

Katika hatua nyingine, Kamati hiyo imeishauri Serikali kuweka utaratibu wa kutoza ada kwa watumiaji wa baadhi ya miundombinu mikubwa, ikiwemo Daraja la Tanzanite, kwa lengo la kuongeza vyanzo vya mapato vitakavyosaidia kugharamia ujenzi wa madaraja na barabara nyingine nchini.

Pia, Kamati imesisitiza umuhimu wa Serikali kuongeza ushirikiano na sekta binafsi katika ujenzi wa barabara na madaraja makubwa kupitia mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP), ambao unaweza kusaidia kuharakisha upatikanaji wa miundombinu ya kisasa na kupunguza mzigo wa kifedha kwa Serikali.

Kakoso amesisitiza kuwa wakandarasi wanaotekeleza miradi mikubwa wanapaswa kutoa mchango kwa jamii zinazozunguka maeneo ya miradi kupitia Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), akipendekeza ujenzi wa vituo vya afya, shule na huduma nyingine muhimu.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema Serikali imepokea maelekezo na ushauri wa Kamati hiyo na itaendelea kuyafanyia kazi.

Amesema ziara za Kamati ni muhimu katika kuhakikisha fedha zinazotengwa kwa miradi ya maendeleo zinatoa thamani halisi kwa wananchi na miundombinu inayojengwa inakidhi viwango vilivyokusudiwa.

Aidha, Kasekenya ameeleza kuwa Serikali ina mpango wa kujenga barabara mpya itakayoanzia eneo la Bandari ya Dar es Salaam kupitia Kigamboni, Chanika na Kisarawe hadi Kiluvya, hatua inayolenga kupunguza msongamano wa magari yanayotoka bandarini kuelekea mikoani.

Amesema mradi huo ni sehemu ya mpango mpana wa ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje ya Jiji la Dar es Salaam (Outer Ring Road), huku Serikali ikitarajia kuanza kuona hatua za utekelezaji mapema mwaka 2027.

Kuhusu ujenzi wa Daraja la Jangwani, Kasekenya amesema usanifu wa mradi huo umezingatia changamoto ya mafuriko katika eneo hilo, ambapo urefu na kimo cha daraja vimeboreshwa ili kuruhusu maji kupita kwa urahisi na kupunguza hatari ya mafuriko katika maeneo ya Jangwani na Kariakoo.









 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad