
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imezitaka taasisi za umma na binafsi kuimarisha ushirikiano na waandishi wa habari wanapofika kukusanya taarifa, ili kuwezesha upatikanaji na usambazaji wa habari sahihi kwa manufaa ya umma.
Wito huo umetolewa Novemba 11, 2026, na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Anthony Kipangula, wakati akihitimisha mafunzo ya siku tatu kwa waandishi wa habari, watangazaji, waandaaji wa vipindi, wapiga picha na wahariri wa Azam Media.
Kipangula amesema ushirikiano wa taasisi na vyanzo vya habari ni muhimu katika kuwasaidia waandishi kutekeleza wajibu wao wa kuhabarisha jamii kwa kuzingatia ukweli, usahihi na maslahi ya Taifa.
Amesema Kifungu cha 7(1) cha Sheria ya Huduma za Habari kinatambua haki ya kukusanya na kusambaza habari na taarifa kwa mujibu wa sheria, hivyo ni muhimu taasisi kutambua nafasi ya wanahabari katika kuifikishia jamii taarifa zinazohusu shughuli na huduma zao.
“Waandishi wanapofika kukusanya taarifa kwa ajili ya kuzichakata na kuzisambaza kwa maslahi ya umma, ni vyema kuwapa ushirikiano ili waweze kuandaa na kuchapisha habari sahihi kwa manufaa ya nchi,” amesema.Katika hatua nyingine, amewataka waandishi wa habari kuzingatia mwonekano, mwenendo na weledi katika utekelezaji wa majukumu yao, akisema mambo hayo yana mchango mkubwa katika kujenga imani kwa vyanzo vya habari na jamii.
Amesema mwonekano wa mwandishi si suala la mavazi pekee, bali ni sehemu ya utambulisho wa kitaaluma inayoweza kuathiri namna anavyopokelewa na kusikilizwa na vyanzo vya habari.

Amesisitiza kuwa waandishi wanapaswa kuvaa kulingana na mazingira na hadhi ya matukio wanayokwenda kuripoti, hususan shughuli rasmi zinazohusisha viongozi wa Serikali na wageni mashuhuri.
Aidha, amewataka wanahabari kuisoma na kuielewa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na sheria zinazohusu sekta hiyo ili kufahamu haki, wajibu na mipaka yao katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mafunzo hayo yaliandaliwa na JAB kwa lengo la kuongeza uelewa wa washiriki kuhusu Sheria ya Huduma za Habari, kanuni, maadili na misingi ya taaluma ya uandishi wa habari, ili kuimarisha weledi na uwajibikaji katika utoaji wa habari.
Yana sehemu ya juhudi za Bodi kuimarisha taaluma ya uandishi wa habari nchini kwa kujenga uwezo wa wanahabari na kuhamasisha uzingatiaji wa sheria na maadili ya taaluma.












No comments:
Post a Comment