JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


MAKAMU WA RAIS AWEKA JIWE LA MSINGI MRADI WA MAJI WA BILIONI 38.4 NANYUMBU

Share This
Nanyumbu, Mtwara

MAKAMU wa Rais ameweka jiwe la msingi la mradi wa maji wa Nanyumbu wenye thamani ya Shilingi bilioni 38.4, unaotarajiwa kunufaisha zaidi ya wananchi 81,000 na kupunguza adha ya kutafuta maji, ikiwemo hatari ya kushambuliwa na mamba katika Mto Ruvuma.

Akizungumza katika hafla hiyo, akiwa katika Kijiji cha Masuguru Wilaya ya Nanyumbu wakati wa ziara yake mkoani Mtwara, Makamu wa Rais amesema mradi huo ni sehemu ya juhudi za Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuwafikishia wananchi maji safi na salama karibu na makazi yao.

Amesema wananchi wa Masuguru na maeneo ya jirani wamekuwa wakitegemea maji ya mtoni, hali iliyosababisha baadhi yao kupoteza maisha kwa kushambuliwa na mamba, huku wanawake na wasichana wakikabiliwa na hatari ya ukatili wa kijinsia wakati wa kutafuta maji.

Ameeleza kuwa Serikali ilichukua hatua baada ya Mwakilishi wa Jimbo hilo, , Yahya Mhata kuwasilisha changamoto hizo kwa Rais Samia.

“Kazi ya Serikali ni kusikia kilio cha wananchi na kutafuta majawabu ambayo yanaleta mabadiliko katika maisha yao,” amesema.

Makamu wa Rais amesema utekelezaji wa mradi huo unaonesha dhamira ya Serikali ya kufikisha uwekezaji mkubwa wa huduma za msingi vijijini. Amesema wananchi waliokuwa wakitarajia kuchimbiwa visima sasa wamepata miundombinu ya kuwafikishia maji karibu na makazi yao.

“Leo hii mradi ule uko hapa kijijini kwenu, mnauona kwa macho, siyo kwa kuhadithiwa,” amesema na kuahidi kumfikishia Rais Samia taarifa ya mafanikio ya mradi huo pamoja na furaha ya wananchi wanaonufaika na huduma hiyo. Makamu wa Rais ameipongeza Wizara ya Maji kwa ufanisi na ubora katika utekelezaji wa mradi huo.

Aidha, amewataka wananchi kuutunza mradi na kuhifadhi mazingira ya Mto Ruvuma, akisema umebuniwa kukidhi mahitaji ya maji kwa miaka 40 na uendelevu wake unategemea pia ulinzi wa chanzo hicho.

Kwa upande wake, Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amesema mradi huo ni kielelezo cha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha huduma za msingi zinawafikia wananchi wote bila kujali maeneo wanayoishi.

Amepongeza ushirikiano wa watendaji wa Wizara ya Maji, RUWASA, wataalamu, viongozi wa Serikali za mitaa na wananchi katika kufanikisha mradi huo. Pia amelishukuru Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kwa kuwezesha upatikanaji wa umeme wa kuendesha miundombinu ya mradi huo.

Akiwasilisha taarifa ya mradi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amesema utekelezaji umefikia asilimia 98.45 na huduma imeanza kutolewa kupitia vioski na miunganisho ya majumbani.

Amesema mradi huo ni sehemu ya mpango wa maji wa miji 28 nchini. Mkataba wake wa ujenzi ulisainiwa Juni 6, 2022, na utekelezaji kuanza Aprili 23, 2023.

Mradi unahusisha uchukuaji wa maji kutoka Mto Ruvuma katika kijiji cha Masuguru, mtambo wa kutibu maji wenye uwezo wa lita milioni tano, matanki mawili yenye jumla ya ujazo wa lita milioni 1.1, bomba kuu la kilomita 65.3, mtandao wa usambazaji wa kilomita 35 na vituo 20 vya kuchotea maji.

Mhandisi Mwajuma amesema mradi ulikabidhiwa kwa mwendeshaji Oktoba 23, 2026, na tayari unahudumia maeneo ya Masuguru, Nachura, Lidede, Mwambani, Sengenya, Mangaka, Kilimanihewa, Mkwajuni na Ngalinje, huku kazi za umaliziaji zikiendelea. Mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na India.














 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad