Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, akikagua mitambo na teknolojia mbalimbali zinazotumika katika shughuli za uchimbaji wakati wa ziara ya mabanda katika Maonesho ya Kitaifa ya Tisa ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini, leo katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bomba Mbili, Geita.
Na Mwandishi Wetu, Bombambili, Geita
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amezitaka kampuni za Kitanzania kuunganisha mitaji, teknolojia, utaalamu na uzoefu ili kujenga kampuni imara zenye uwezo wa kushindana na kushiriki kikamilifu katika fursa kubwa za biashara na uwekezaji zinazotarajiwa kutokana na kuanzishwa kwa miradi mipya ya uchimbaji madini nchini.
Amesema hatua hiyo ni muhimu kwa kampuni za ndani kujiandaa mapema, kuongeza uwezo wa uzalishaji na utoaji huduma na kuhakikisha zinakuwa sehemu muhimu ya mnyororo wa thamani wa sekta ya madini, badala ya kusubiri fursa hizo zije wakati hazina uwezo wa kuzitekeleza.
Mavunde amesema hayo leo, Oktoba 2, 2026, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini yaliyofanyika katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bombambili mkoani Geita, sambamba na Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini Geita.
Amesema Serikali inalenga kuhakikisha asilimia 90 ya Sh5.1 trilioni zinazotumika kila mwaka kununua bidhaa na huduma katika sekta ya madini zinabaki nchini kupitia utekelezaji wa Sera ya Ushirikishwaji wa Watanzania, hatua inayolenga kuongeza fursa za kiuchumi kwa wazawa na kuhakikisha ukuaji wa sekta hiyo unaacha manufaa mapana zaidi katika uchumi wa Tanzania.
.jpeg)
Kwa mujibu wa Mavunde, ukubwa wa fursa hizo unatarajiwa kuongezeka zaidi kutokana na kampuni 14 zinazotarajiwa kuanzisha miradi mikubwa ya madini pamoja na leseni 28 za uchimbaji wa madini ya kinywe (graphite), ambazo Serikali imekuwa ikisisitiza ziingie katika uzalishaji. Serikali tayari imewataka wamiliki wa leseni hizo za graphite kuharakisha utekelezaji wa miradi yao.
Amesema hali hiyo inapaswa kuzifanya kampuni za Kitanzania kuacha kufanya biashara kwa kutegemea uwezo wa kampuni moja moja pekee na badala yake kuangalia namna ya kuunganisha mitaji, vifaa, teknolojia na utaalamu ili kushindania kazi kubwa zinazohitaji uwezo mkubwa wa kifedha na kiufundi.
Mavunde amewashukuru wachimbaji, kampuni za madini na wadau wengine kwa mchango wao katika ukuaji wa sekta hiyo, huku akimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo na maono yaliyowezesha mageuzi makubwa na kuongeza nafasi ya Watanzania katika mnyororo wa thamani wa madini.
Amesema chini ya uongozi wa Rais Samia, Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wazawa kushiriki katika ugavi wa bidhaa na huduma, ajira, uongozi wa kampuni za madini, utafiti na hatua kwa hatua uzalishaji wa bidhaa zinazotumiwa na migodi..jpeg)
Katika kuimarisha zaidi ushirikishwaji huo, Mavunde ameielekeza Tume ya Madini kufanya ukaguzi wa kampuni zilizoingia ubia na Watanzania ili kubaini iwapo washirika wazawa wanashiriki kikamilifu katika shughuli za biashara, miamala na manufaa yanayotokana na umiliki wao.
Amesisitiza kuwa ushirikishwaji wa Watanzania haupaswi kuishia kwenye majina na nyaraka za kampuni, bali lazima uonekane katika shughuli halisi za biashara na kujenga uwezo wa kifedha, kiteknolojia na kitaalamu wa kampuni za ndani.
Mfumo wa local content unazitaka kampuni zisizo za Kitanzania zinazotaka kutoa bidhaa au huduma migodini kushirikiana na kampuni zinazokidhi masharti ya ushirikishwaji wa Watanzania, huku Tume ya Madini ikiwa na jukumu la kusimamia mipango hiyo. Serikali pia imetenga makundi 20 ya bidhaa na huduma kwa kampuni zinazomilikiwa kwa asilimia 100 na Watanzania.

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Reuben Lekashingo, amesema ubia na kampuni za nje umekuwa muhimu katika kuleta teknolojia, mitaji, ujuzi na uzoefu nchini, lakini lengo haliwezi kuwa kampuni za Kitanzania kubaki washirika wadogo kwa muda usio na mwisho.
Amesema mwelekeo ni kuzitoa kampuni za Kitanzania kutoka kwenye ushiriki kwenda kwenye umiliki, kutoka shughuli za thamani ndogo kwenda kwenye shughuli za thamani kubwa, na kutoka utegemezi kwenda kwenye ushindani wa kweli.
Mavunde amesema Serikali pia inataka Watanzania waongeze ushiriki katika maeneo kama uchorongaji, uhandisi, teknolojia, matengenezo ya mitambo, vilipuzi, usambazaji wa mitambo na vipuri pamoja na huduma nyingine za kitaalamu zinazobeba thamani kubwa katika sekta ya madini.
Amesisitiza pia umuhimu wa kuongeza uzalishaji wa bidhaa hizo ndani ya Tanzania ili local content isibaki kwenye biashara ya kununua na kuuza pekee, bali ijenge viwanda, teknolojia na kampuni zenye uwezo wa kuhudumia migodi ya Tanzania na baadaye masoko ya nchi jirani.

Ameitaja Buzwagi Special Economic Zone, Kahama, kuwa moja ya maeneo yanayokusudiwa kusaidia kujenga msingi huo wa uzalishaji na viwanda vinavyohudumia sekta ya madini.
Akizungumzia kupanua fursa za baadaye, Mavunde amesema Serikali imetenga asilimia 10 ya makusanyo yatokanayo na sekta ya madini kwa ajili ya kugharamia utafiti wa kina wa rasilimali madini, hatua iliyolenga kuongeza taarifa sahihi za kijiolojia na kufungua maeneo mapya kwa uchimbaji na uwekezaji. Uamuzi huo ulitangazwa rasmi Juni mwaka huu.
Amesema Tanzania pia imepata Dola za Marekani milioni 60 kutoka Serikali ya China kwa ajili ya utafiti wa kina katika mikoa ya Dodoma, Singida na Tabora, hatua ambayo pamoja na tafiti nyingine zinazofanyika nchini inatarajiwa kupanua zaidi wigo wa miradi na fursa katika sekta hiyo.
Mavunde amewataka Watanzania kuchangamkia fursa hizo, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwaunga mkono ili kuhakikisha utajiri wa madini unaleta manufaa mapana kwa wananchi na kujenga kampuni zenye uwezo wa kukua na kushindana hata nje ya Tanzania.
Katika hatua nyingine, Mavunde amesema sekta ya madini imeendelea kuwa nguzo muhimu ya uchumi, ikichangia asilimia 10.3 ya Pato la Taifa na kuongoza katika mapato yasiyo ya kodi kwa mujibu wa taarifa za Serikali.

Amesema kati ya Sh1.343 trilioni zilizokusanywa katika mwaka wa fedha uliopita, wachimbaji wadogo walichangia takribani asilimia 40, jambo linaloonesha nafasi inayoongezeka ya kundi hilo katika uchumi wa madini.
Katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/27, sekta imekusanya Sh411 bilioni, sawa na asilimia 117 ya lengo la Sh350 bilioni.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Alexander Mnyeti, amesema kupanuka kwa fursa za local content lazima kuende sambamba na uwezo wa Watanzania kutoa bidhaa na huduma zinazokidhi vigezo vya ubora, usalama, bei na mahitaji ya kiufundi ya migodi.
Amesema kampuni za Kitanzania zinapaswa kutumia fursa zilizofunguliwa na Serikali kujenga uwezo na ushindani, badala ya kutegemea ulinzi wa kisera bila kuwekeza katika viwango vinavyohitajika na sekta.
Naye Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Tanzania (FEMATA), John Bina, ameishukuru Serikali kwa usimamizi wa sheria, kanuni na taratibu katika sekta ya madini, akisema hatua hiyo imepanua ushiriki wa Watanzania katika uchimbaji, biashara ya madini, utoaji huduma na ugavi wa bidhaa.
Mbunge wa Geita Mjini, Mhe. Chacha Wambura, amesema Serikali imeendelea kufanyia kazi maoni na ushauri wa wadau na Bunge katika kuboresha sera, sheria na mifumo ya usimamizi wa sekta, huku akisisitiza umuhimu wa kampuni za Kitanzania kutumia vizuri fursa zinazofunguliwa na Serikali.
Kwa Serikali, ukubwa wa soko linalokuja ndio unaofanya maandalizi ya kampuni za Kitanzania kuwa muhimu sasa. Miradi 14 mikubwa, maendeleo ya miradi ya graphite na ongezeko la utafiti wa madini vinatarajiwa kuongeza mahitaji ya bidhaa, huduma, teknolojia na utaalamu—na dhamira ni kuona sehemu kubwa ya biashara hiyo ikijenga kampuni imara zinazomilikiwa na Watanzania.
.jpeg)


No comments:
Post a Comment