JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


USALAMA WA RELI NI JUKUMU LA KILA MMOJA: LATRA YAWAKUMBUSHA WADAU MOROGORO

Share This

 

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imeendelea kutoa elimu kwa wadau ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Usalama wa Reli yanayofanyika katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) tarehe 4 hadi 10 Oktoba 2026.

Maadhimisho hayo kwa upande wa Tanzania yamefanyika kwa uratibu wa Wizara ya Uchukuzi yakihusisha LATRA, Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Mamlaka ya Reli ya Tanzania-Zambia (TAZARA). Mkoani Morogoro, wataalamu wa LATRA wakiongozwa na Bw. Salum Pazzy, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano, aliyeambatana na Mha. John Shirima, Mkaguzi wa Reli LATRA, wameshiriki semina za kutoa elimu kwa watendaji wa Karakana ya Reli, Chuo cha Reli (TIRTEC) na Kituo cha Treni ya Kisasa (SGR) Jakaya Kikwete kwa lengo la kuwakumbusha wadau hao umuhimu wa kuzingatia usalama katika shughuli za usafirishaji kwa njia ya reli.

Akizungumza katika semina hizo, Bw. Salum Pazzy, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano LATRA, amewasihi wadau kuzingatia usalama wa reli katika nyanja zote ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea ikiwa usalama utapuuzwa.

“Usalama wa usafiri wa reli unaanza na wanaoongoza vitembea reli, mafundi mpaka kwa wananchi. Kila kitendo unachokifanya kitachangia kuleta athari hasi au chanya. Uzembe mdogo katika eneo lolote unaweza kuleta madhara makubwa ambayo ni hasara kwa Taifa, hivyo ni muhimu kukumbushana na kuzingatia dhana nzima ya usalama ili kuufanya usafiri wa reli nchini kuendelea kuwa salama na wa mfano,” amesema Bw. Pazzy.

Kwa upande wake, Mha. Shirima amesema kuwa Maadhimisho ya Wiki ya Usalama wa Reli yalianzishwa kwa lengo la kupunguza ajali, hivyo watendaji wote wanapaswa kufanya kazi zao kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya kazi zao na kujiepusha kufanya kazi kwa mazoea.

Wiki ya Usalama wa Reli mwaka huu inaendelea kuhamasisha jamii kwa ujumla kuzingatia kaulimbiu isemayo, “Fikiria Usalama, Tenda kwa Usalama, Kuanzia Mahali pa Kazi hadi kwa Jamii. Kila Tendo lina Athari.”

 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad