Na Mwandishi Wetu, Chunya
Benki ya NMB imetangaza fursa za kifedha kwa wadau wa sekta ya madini nchini kwa kutoa dhamana za zabuni (Bid Bonds) zisizohitaji dhamana ya mali za hadi dola za Marekani milioni 11, pamoja na dhamana za malipo ya awali (Advance Payment Guarantees) na utekelezaji wa mikataba (Performance Guarantees) za hadi Sh bilioni 11, ili kuwawezesha kushiriki zabuni na kutekeleza mikataba mikubwa ya biashara.
Akizungumza katika hafla ya NMB Business Executive Network iliyowakutanisha wachimbaji wa dhahabu na wadau wa sekta ya madini kutoka Chunya mkoani Mbeya na Songwe, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi, amesema huduma hizo zinalenga kupunguza vikwazo vya kifedha vinavyowakabili wafanyabiashara na watoa huduma migodini. Amesema benki itaendelea pia kutoa elimu ya fedha ili kuwasaidia wateja kusimamia biashara zao na kutumia fursa zilizopo kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Meneja wa NMB Kanda ya Nyanda za Juu, Wogofya Mfalamagoha, amesema shughuli za uchimbaji madini zimefungua fursa za ajira na biashara, hivyo kuifanya benki kuimarisha ushirikiano na wadau wa sekta hiyo. Naye mwakilishi wa Chama cha Watoa Huduma Migodini (TAMISA), Gilbo Thomas, amesisitiza umuhimu wa upatikanaji wa vifaa vya uchimbaji ili kuongeza tija na kuboresha shughuli za wachimbaji.
Mwakilishi wa Chama cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Mbeya (MBEREMA), Saddam Kyando, ameiomba NMB kuangalia uwezekano wa kutumia leseni za uchimbaji kama dhamana ya mikopo kwa wachimbaji wadogo. Nao wachimbaji Fredrick Meshack, Sophia Mwanauta, Mussa Wilfred na Simon Mbalawata wamepongeza mikutano ya benki na wateja wake, wakisema inatoa nafasi ya kujadili changamoto na fursa za kukuza biashara katika sekta ya madini.

.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)



No comments:
Post a Comment