JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


IPU YAITAKA DUNIA KUIMARISHA SHERIA, UWEKEZAJI AFYA YA MAMA NA MTOTO

Share This




RAIS wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dkt. Tulia Ackson, ameyataka mabunge duniani kuimarisha sheria, kuongeza uwekezaji na kuweka mifumo madhubuti ya uwajibikaji ili kuhakikisha wanawake, watoto, watoto wachanga na vijana wanapata huduma bora za afya.

Dkt. Tulia ameyasema hayo wakati wa mazungumzo ya pamoja ya kibunge kuhusu afya ya uzazi, mama na mtoto yaliyofanyika jijini Arusha sambamba na Mkutano wa 153 wa IPU.

Amesema afya ya wanawake, watoto, watoto wachanga na vijana si suala la afya pekee, bali ni suala linalogusa haki za binadamu, usawa, maendeleo na utulivu wa taifa.

Dkt. Tulia ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali, Bunge la Tanzania na wananchi kwa ukarimu wao na kuwezesha mazingira mazuri ya kufanyika kwa mkutano huo muhimu wa kimataifa wa mabunge.

Amesema uongozi na dhamira ya Rais Samia vimechangia kuileta pamoja jumuiya ya wabunge duniani katika mkutano huo, huku akieleza kuwa uongozi wake umeendelea kusukuma ajenda ya kuboresha afya na ustawi wa jamii, kuimarisha mifumo ya afya pamoja na kuhakikisha uwekezaji endelevu na uwajibikaji katika sekta hiyo.

Kwa mujibu wa Dkt. Tulia, wabunge wana nafasi muhimu ya kutunga sheria zinazolinda afya na haki za wanawake na watoto, kutenga rasilimali zinazohitajika, kusimamia matumizi yake na kuhakikisha Serikali zinawajibika katika utoaji wa huduma hizo.

Amesema ni muhimu ahadi za kisiasa kutafsiriwa katika bajeti kwa kuwekeza katika huduma za afya ya msingi, afya ya mama na mtoto mchanga, lishe pamoja na upatikanaji wa dawa muhimu za kuokoa maisha.

Dkt. Tulia pia amesisitiza umuhimu wa kuimarisha usimamizi na uwajibikaji, akisema matumizi ya takwimu na ushahidi wa kuaminika ni muhimu katika kubaini maeneo yenye ukosefu wa usawa na kuhakikisha wanawake, vijana na jamii wanashirikishwa katika maamuzi yanayohusu maisha yao.

Aidha, amewataka wabunge kuimarisha ushirikiano na kubadilishana uzoefu, suluhisho na mbinu bora kati ya mabunge ili kutafsiri ahadi za kimataifa kuwa vipaumbele vya kitaifa na matokeo yanayopimika.

Amesema IPU imejizatiti kuwa mshirika wa vitendo kwa mabunge katika kuimarisha uwezo wa kutunga sheria madhubuti za afya, kuandaa na kusimamia bajeti, kufanya uangalizi na kudai uwajibikaji.

Dkt. Tulia amesema lengo linapaswa kuwa “kutoka kwenye ahadi kwenda utekelezaji, kutoka utekelezaji kwenda uwajibikaji na kutoka uwajibikaji kwenda kwenye matokeo,” akisisitiza kuwa hakuna muda wa kuchelewesha hatua za kukabiliana na vifo na madhara yanayoweza kuzuilika.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu, amesema ni heshima na fursa kubwa kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mazungumzo hayo ya kibunge yanayolenga kuimarisha uongozi katika masuala ya afya ya wanawake, akina mama, watoto, watoto wachanga na vijana.

Spika Zungu amesema afya ya makundi hayo si suala la afya pekee, bali linahusiana pia na haki za binadamu, usawa, maendeleo na utulivu wa taifa.

Amesisitiza umuhimu wa huduma muhimu za kuokoa maisha kupewa kipaumbele katika ufadhili, akitolea mfano dawa na huduma za kudhibiti na kuzuia kuvuja damu wakati wa kujifungua.

Aidha, Spika Zungu amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi na kujitoa katika kuhakikisha huduma za afya ya mama na mtoto zinaendelea kuboreshwa nchini, akisema juhudi hizo ni sehemu muhimu ya kuimarisha afya na ustawi wa wanawake na watoto Tanzania.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad