Na Munir Shemweta
Serikali kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ushiriki wa wadau katika maendeleo ya makazi, kwa kuzingatia sera, sheria na mipango ya kitaifa.
Hayo yameelezwa leo tarehe 30 Sept 2026 na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo wakati wa sherehe za miaka 40 ya UN Habitat for Humanity Tanzania jijini Dar es Salaam. Maadhimisho hayo yameambatana pia na kampeni ya ‘’Opening the door campaign’’ pamoja na uzinduzi wa mpango mkakati wa miaka mitano ya shirika hilo (Strategic Plan 2025-2029).
Mhe. Dkt Leonard Akwilapo amesema, Serikali, inatamani kuona Tanzania ambayo kila familia inapata fursa ya kuishi katika makazi salama, bora, yenye huduma muhimu na yanayomudu uwezo wa kiuchumi.
Amebainisha kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria kuhakikisha kuwa watanzania wanakuwa na makazi salama.
Amesema, wizara yake inafanya juhudi pia za Kuimarisha upangaji na usimamizi wa ardhi; Urasimishaji wa makazi yasiyopangwa na Kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi na wadau wengine kushiriki katika utoaji wa makazi bora na nafuu nchini.
Amelipongeza Shirika la Habitat for Humanity Tanzania kwa kuandaa na kuzindua Mkakati wake wa Miaka Mitano (Strategic Plan 2025-2029) mkakati alioueleza kuwa, utatoa fursa ya kuangalia miaka ijayo kwa mtazamo mpana zaidi.
Akielezea kampeni ya “Opening the Door Campaign” ya Habitat for Humanity amesema, kampeni hiyo inao ujumbe mzito na muhimu ambapo ametoa rai kuwa kampeni hiyo itumike kuhamasisha wadau wengi zaidi kuwekeza katika makazi na fursa zinazotokana na makazi bora.
‘’Ninaamini kwamba mafanikio ya kampeni hii yatategemea uwezo wetu wa kuunganisha nguvu za wadau mbalimbali na kuzifanya rasilimali zifike kwa wananchi wenye uhitaji zaidi ili lengo la kuwafikia watu millioni tatu na laki mbili ifikiwe’’. Amesema
Ametoa wito kwa sekta binafsi, taasisi za fedha, wafadhili, mashirika ya kimataifa, wataalamu na wananchi kuendelea kushirikiana na Habitat for Humanity Tanzania katika kufikia malengo yao haya.
Amesema, Wizara yake inapongeza kuanzishwa kwa Mkakati wa Miaka Mitano na “Opening the Door Campaign” ambapo ameeleza kuwa, iwapo utatekelezwa vyema utachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto ya makazi nchini.
Mkurugenzi wa Taifa wa Un Habitat for Humanity Tanzania Bi. Magdalena George amesema shirika hilo limekuwa msaada mkubwa kwa jamii hususan katika upande wa makazi bora na kubainisha kuwa tayari shirika hilo limewafikia zaidi ya watu milioni 1.3.
Hata hivyo, amesema Pamoja na shirika hilo kutilia mkazo ujenzi wa nyumba salama na za gharama nafuu pia linaangalia vifaa vya ujenzi ili jamii iweze kumudu gharama za ujenzi.
Kwa upande wake Mlezi wa Un Habitat for Humanity Tanzania ambaye ni mke wa Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu Mama Anna Mkapa amesema, amekuwa akilishawishi Shirika la Un Habitat for Humanity Tanzania kujenga nyumba za wahitaji wasiojiweza na kutolea mfano wa ujenzi wa nyumba eneo la Chamwino Mkoani Dodoma na kueleza kuwa ujenzi huo uliacha alama.
Shirika la Un Habitat for Humanity Tanzania mbali na kushiriki kusaidia ujenzi wa nyumba kwa wasiojiweza na wenye uhitaji pia linashiriki kwenye miradi ya majisafi na usafi wa mazingira pamoja na Matumizi ya Nishati Safi ya Jua katika mashule.Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akipata maelezo ya utekelezaji miradi mbalimbali ya shirika la Un Habitat for Humanity Tanzania kutoka kwa Mkurugenzi wa Taifa wa shirika hilo Bi. Magdalena George wakati wa sherehe za miaka 40 zilizofanyika jijini Dar es Salaam Sept 30, 2026. Kushoto ni mlezi wa shirika hilo Mama Anna Mkapa.


No comments:
Post a Comment