WAZIRI wa Afya, Mohamed Mchengerwa, ameiagiza Bodi mpya ya Wadhamini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kusimamia kwa karibu ubora wa huduma, uwajibikaji, matengenezo ya miundombinu na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Muhimbili Mpya.
Mchengerwa ametoa maagizo hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Wadhamini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili pamoja na miradi minne ya kimkakati iliyotekelezwa na hospitali hiyo.
Miradi hiyo ni Kitengo cha Afya ya Mama na Mtoto Tumboni (Maternal-Fetal Unit), Chumba cha Kisasa cha Upasuaji wa Uzazi (Modular Theatre), Mtambo wa Kuzalisha na Kusambaza Hewa Tiba pamoja na Kliniki ya Huduma za Haraka (Fast Track/VIP).
Amesema bodi hiyo imepewa dhamana kubwa ya kusimamia taasisi ambayo ni kituo cha mwisho cha rufaa nchini na yenye jukumu la kutoa huduma za kibobezi kwa wagonjwa kutoka maeneo mbalimbali.
“Bodi haiteuliwi ili ikae; inateuliwa ili isimame kwa ajili ya mgonjwa, isimame kwa ajili ya ukweli na isimame hata pale ambapo kusimama kunagharimu,” amesema.
Mchengerwa amempongeza Profesa Muhammad Bakari Kambi kwa kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu, akisema uteuzi huo unatokana na uzoefu na uwezo wake katika kusimamia taasisi kubwa.
Amesisitiza kuwa bodi inapaswa kuhakikisha Muhimbili inaendeshwa kwa misingi ya utawala bora, uwazi, uwajibikaji na nidhamu, huku ikishirikiana kwa karibu na menejimenti ya hospitali.
Aidha, ameelekeza bodi kuhakikisha vifaa tiba, mitambo na miundombinu vinapatiwa matengenezo kwa wakati ili kuepusha kusimama kwa huduma.
Akizungumzia mtambo mpya wa hewa tiba, amesema umegharimu takribani Sh1.63 bilioni na unatarajiwa kuondoa changamoto ya upatikanaji wa hewa tiba ambayo imekuwa ikilalamikiwa katika hospitali hiyo.
“Naelekeza usimamizi wa mtambo huu ufanyike ipasavyo, kwa matengenezo kinga kwa wakati, ili huduma iwe endelevu. Hewa tiba ni dawa na dawa isiyopatikana kwa wakati si dawa tena,” amesema.
Katika hatua nyingine, Mchengerwa amesema Kitengo cha Afya ya Mama na Mtoto Tumboni kitasaidia kubaini mapema changamoto na hatari zinazoweza kujitokeza kwa mama mjamzito na mtoto akiwa bado tumboni.
Amesema huduma hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali katika kutekeleza mkakati wa kupunguza vifo vya mama na watoto wachanga, kwa kuhamisha mfumo wa huduma kutoka kusubiri dharura hadi kuzuia na kutambua hatari mapema.
Kuhusu Chumba cha Kisasa cha Upasuaji wa Uzazi, amesema kituo hicho kinapaswa kutumika kupunguza muda wa kusubiri huduma za upasuaji, maambukizi na vifo vya akina mama na watoto.
Mchengerwa pia ameagiza hospitali nyingine kubwa nchini kujifunza kutoka mradi huo na kuweka mipango ya kuboresha mazingira ya vyumba vya upasuaji.
Akizungumzia Kliniki ya Huduma za Haraka (VIP), amesema huduma hiyo inalenga kuwapa Watanzania wenye uwezo wa kiuchumi huduma za hadhi ya juu nchini na hivyo kupunguza ulazima wa baadhi yao kusafiri nje ya nchi kutafuta huduma.
Amesema mapato yatakayopatikana kupitia kliniki hiyo yanapaswa kutumika pia kuboresha huduma kwa wagonjwa wasio na uwezo, kupitia mfumo wa ruzuku mtambuka.
“Ubunifu wa mapato usiwe kamwe sababu ya kusahau kwa nini tunakusanya mapato,” alisema.
Mchengerwa ametaka kliniki hiyo ijengewe chapa na kutangazwa ili kuwavutia wateja wa ndani na nje ya nchi wanaohitaji huduma za kibobezi.
Katika eneo la uwajibikaji, Waziri huyo ameiagiza bodi kuwasilisha ripoti za mara kwa mara zinazoonyesha matokeo ya miradi hiyo, ikiwemo idadi ya akina mama waliohudumiwa, kiwango cha kupungua kwa maambukizi, uzalishaji wa hewa tiba na mapato yanayotokana na Kliniki ya Huduma za Haraka.
Amesema takwimu hizo zitasaidia Serikali kupima matokeo ya uwekezaji uliofanyika na kupanga hatua nyingine za kuboresha huduma.
Mchengerwa pia ameipa Bodi ya Wadhamini jukumu la kusimamia utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Muhimbili Mpya, akisema ni mradi mkubwa wa kimkakati unaolenga kuipa hospitali hiyo sura mpya inayokwenda sambamba na mahitaji ya Karne ya 21 na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
“Katika majukumu ya mara kwa mara ya bodi, mradi huu upewe kipaumbele ili utekelezaji wake uende sambamba na mpango kazi uliowekwa,” amesema.
Amesema Serikali inalenga kuifanya Muhimbili kuwa kituo chenye huduma za kibobezi za hadhi ya kimataifa zitakazowafanya Watanzania kupata huduma hizo nchini badala ya kusafiri nje ya nchi.
Amewataka wajumbe wa bodi hiyo kutumia uzoefu wao katika tiba, uongozi, fedha, sheria na uhandisi kuhakikisha hospitali inaendelea kuboresha huduma na kutekeleza malengo yaliyowekwa na Serikali.
Kwa upande mwingine, ameipongeza Menejimenti ya Hospitali ya Taifa Muhimbili chini ya Mkurugenzi Mtendaji, Dkt. Delilah Kimambo, kwa kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo na kuwataka kuendelea kushirikiana na bodi mpya.
Amesema uwekezaji katika miundombinu ya afya unapaswa kwenda sambamba na usimamizi madhubuti, ili wananchi wanufaike na huduma bora na endelevu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Dkt. Delilah Charles Kimambo, amesema hospitali hiyo imenufaika na uwekezaji mkubwa katika kipindi cha uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesema miongoni mwa miradi mikubwa ni ujenzi wa Muhimbili Mpya unaogharimu Sh1.2 trilioni, ambao kwa sasa umefikia hatua ya kumpata mshauri elekezi kwa ajili ya utekelezaji.
Dkt. Kimambo amesema hospitali hiyo pia imepokea vifaa tiba vya kisasa ikiwemo Mammography, Angio Suite, MRI, CT Scan za kisasa na Hyperbaric Chamber, ambavyo vimeongeza uwezo wa kutoa huduma za vipimo na matibabu ya kibingwa na kibingwa bobezi.
Amesema uwekezaji huo umesaidia pia kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kupata huduma za matibabu.
Katika hatua nyingine, Muhimbili imezindua chumba cha upasuaji cha kisasa chenye thamani ya Sh1.8 bilioni, kikilenga kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto.
.jpeg)


.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)


No comments:
Post a Comment