Benki ya NMB imeingia ushirikiano na kampuni ya teknolojia ya afya, Dawa Mkononi, utakaowezesha Mpango wa Ufadhili wa Mitaji kwa Maduka ya Dawa na Viwanda vya Dawa. Mpango huu utasaidia wasambazaji na wafanyabiashara wa bidhaa za dawa waliokidhi vigezo kupata mitaji ya kuendesha biashara zao.
Hati ya Makubaliano (MoU) iliyosainiwa jijini Kigali, Rwanda, itaifanya benki ya NMB kutoa mikopo kwa jukwaa la kidigitali la Dawa Mkononi hatua itakayopunguza changamoto za ukwasi zinazoathiri ununuzi na upatikanaji na usambazaji wa dawa katika mnyororo wa huduma za afya.
Mkurugenzi wa Mikakati na Ukuaji wa Benki ya NMB, Francis Mittah, alisema ushirikiano huo unaonesha fursa iliyopo kwa benki na kampuni za teknolojia kubuni mifumo ya kifedha inayokidhi mahitaji ya biashara kupitia mifumo ya kidijitali.
Kwa upande wake Joseph Paul, Mkurugenzi Mtendaji wa Dawa Mkononi alisema upatikanaji wa mitaji ni sehemu muhimu katika kujenga mnyororo imara na wenye ufanisi wa usambazaji wa dawa, hususan kwa biashara zinazohitaji ukwasi wa kutosha ili kuhakikisha dawa zinapatikana wakati wote.
Ushirikiano huo unatarajiwa kuimarisha zaidi mahusiano kati ya taasisi hizo mbili katika kuendeleza suluhisho za kifedha zinazoongozwa na teknolojia kwa biashara zinazofanya kazi katika mnyororo wa thamani wa sekta ya afya.



.jpeg)




No comments:
Post a Comment