JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


DIWANI NYATORI AAHIDI KUSHUGHULIKIA CHANGAMOTO ZA BARABARA, UMEME NA MAJI GODIANA

Share This

Na Mwandishi Wetu. Ubungo, Dar es Salaam

MBEZI. Shule ya Msingi Godiana iliyopo Mtaa wa Mpigi Mgoe, Kata ya Mbezi, Wilaya ya Ubungo, imeadhimisha mahafali yake ya tisa ya kuwapokeza wahitimu wa Darasa la Saba.

Mahafali hayo yalihudhuriwa na viongozi wa Kata ya Mbezi, uongozi wa shule, walimu, wazazi pamoja na wanafunzi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Diwani wa Kata ya Mbezi, Mheshimiwa Pius Nyatori, aliipongeza shule hiyo kwa juhudi zake katika kutoa elimu na kuahidi kushirikiana na uongozi wa shule pamoja na wadau kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili shule hiyo.

Miongoni mwa changamoto hizo ni barabara, umeme na maji, ambazo zinaathiri mazingira ya kujifunzia na shughuli za kila siku za shule.

Nyatori alisema suala la maji ni miongoni mwa changamoto zinazohitaji kufanyiwa kazi, akieleza kuwa atazungumza na wadau na mwekezaji ili kuona namna ya kupata ufumbuzi.

“Tunatambua shida ya maji hapa. Tutaongea na mwekezaji ili tuone jinsi ya kuwekeza, kwa sababu watu wengi wanategemea shule hii,” alisema Nyatori.
Kwa upande wake, mmiliki wa Shule ya Godiana alisema ataendelea kushirikiana na serikali, walimu na wazazi kuhakikisha watoto wanapata elimu katika mazingira bora.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Godiana, Bw. Macmin  Silumbu, alisema shule hiyo imekuwa ikifanya vizuri katika matokeo ya kitaifa na anaamini wahitimu wa mwaka huu watafanya vizuri zaidi.

“Leo tumefanikiwa kuwa na mahafali ya tisa. Ukweli ni Mungu ametujalia. Tuna walimu ambao wameshafundisha na tunaamini watoto wetu wanaenda kufanya vizuri,” alisema Silumbu.

Uongozi wa shule umetoa wito wa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Kata ya Mbezi pamoja na wadau mbalimbali ili changamoto za barabara, umeme na maji zipatiwe ufumbuzi na kuwezesha wanafunzi kusoma katika mazingira bora.







 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad