Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, 18 Agosti 2026, wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa Uwanja wa AFCON pamoja na Bandari ya Fumba, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amesema kukamilika kwa uwanja huo kutaiweka Zanzibar katika nafasi nzuri ya kunufaika na fursa za biashara, huduma na shughuli nyingine za kiuchumi zitakazotokana na ongezeko la wageni, hususan wakati wa Michuano ya AFCON 2027.
Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuhakikisha miundombinu inayozunguka uwanja huo inajengwa kwa ubora na viwango vinavyokubalika kimataifa, ili kuongeza thamani ya eneo hilo na kuleta tija kwa Zanzibar kwa muda mrefu.
Kwa sasa, ujenzi wa Uwanja wa AFCON umefikia takribani asilimia 80, huku miundombinu mbalimbali ikiendelea kujengwa, ikiwemo barabara ya kisasa itakayoboresha usafiri na kuongeza haiba ya eneo hilo.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali inaendelea kujenga viwanja vya michezo katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar kwa lengo la kukuza vipaji vya vijana na kuwawezesha kupata fursa za kushiriki mashindano ya kitaifa na kimataifa.
Ameipongeza Kampuni ya Orkun kwa utekelezaji wa ujenzi wa uwanja huo kwa kuzingatia ubora na hadhi ya kimataifa, pamoja na kuweka miundombinu inayouwezesha kuhudumia shughuli mbalimbali za michezo na kijamii.
Uwanja wa AFCON Fumba utakuwa na uwezo wa kuchukua watazamaji 36,500, pamoja na viwanja viwili vya nje vyenye uwezo wa kuchukua watazamaji 5,000 kila kimoja.
Uwanja huo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Desemba 2026, ikiwa ni sehemu muhimu ya maandalizi ya Zanzibar kuelekea AFCON 2027.














No comments:
Post a Comment