Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, amesema Wizara yake iko tayari kutoa hati miliki za ardhi kwa maeneo yatakayotumika katika shughuli za utafiti, elimu ya ujuzi na ubunifu nchini.
Dkt. Akwilapo ameyasema hayo leo, Agosti 18, 2026, wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu kwa mwaka 2026, inayoendelea viwanja vya Usagara jijini Tanga.
Amesema, Wizara ya Ardhi iko tayari kushirikiana na taasisi za elimu na utafiti kwa kuhakikisha maeneo yanayotumika katika shughuli hizo yanapatiwa hati miliki ili kuwezesha utekelezaji wa tafiti na ubunifu kwa ufanisi.
“Nichukue fursa hii kuipongeza Wizara ya Elimu, sambamba na kuwashukuru wahadhiri na wakufunzi wote kwa kazi nzuri ya kuandaa vijana katika kazi za ujuzi na ubunifu. Wizara yangu iko tayari kutoa hati miliki katika maeneo ya utafiti,” amesema Dkt. Akwilapo.
Akizungumzia Maonesho ya wiki ya kitaifa ya elimu, ujuzi na ubunifu nchini, Dkt. Akwilapo amepongeza kazi inayofanywa na taasisi za elimu, akisema Tanzania imepiga hatua kubwa katika matumizi ya teknolojia na ubunifu.
“Nipongeze ubunifu pamoja na maonesho. Kwa kweli yamefana sana, na ubunifu mliouonesha ni wa hali ya juu. Nawapongeza kwa yote mnayoyafanya katika taasisi zenu,” amesema.
Dkt. Akwilapo, ambaye aliwahi kuwa katika Wizara ya Elimu, ameeleza kuwa, mabadiliko yaliyofanyika katika sekta hiyo yanaonesha kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa, hususan katika mabadiliko ya mitaala na kuibua vipaji vya vijana.
“Mimi nilikuwa Wizara ya Elimu na nilivyoiacha siyo ilivyo sasa. Mmepiga hatua kubwa, mmebadilisha. Tulivyoiacha siyo ilivyo leo. Mmerekebisha mtaala wa Amali na Sera, na matokeo yake tunayoyaona sasa, ambapo vijana wa kidato cha kwanza na cha pili wanaonesha uwezo wao,” amesema.
Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu kwa mwaka 2026 imezinduliwa rasmi na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda, ikiwa na lengo la kuendeleza ujuzi, ubunifu na matumizi ya teknolojia miongoni mwa vijana na jamii kwa ujumla.
Kaulimbiu ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu mwaka 2026 ni: “Elimu, Ujuzi na Ubunifu: Njia ya Kufikia Dira ya 2050.”

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo akizungumza wakati wa Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na ubunifu inayoendelea katika viwanja vya Usagara mkoani Tanga. (PICHA NA WIZARA YA ARDHI)
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda wakipata maelezo ya bunifu mbalimbali walipotembelea mabanda katika wiki ya kitaifa ya elimu, ujuzi na ubunifu inayoendelea viwanja vya usagara jijini Tanga.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akikabidhi cheti cha tuzo ya utafiti kwa mmoja wa washindi wakati wa Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na ubunifu kwa mwaka 2026 inayoendelea katika viwanja vya Usagara mkoani Tanga.






No comments:
Post a Comment