
Mchungaji wa Makanisa ya Mlima wa Moto, Rose Mgeta akizungumza jijini Dar es Salaam leo Agosti 07, 2026 wakati wa Ibada ya Shukrani ya mwanzilishi wa shule za St. Mary’s.

Meneja wa Shule za St. Mary’s, Muta Rwakatare akizungumza jijini Dar es Salaam leo Agosti 07, 2026 wakati wa Ibada ya Shukrani ya mwanzilishi wa shule za St. Mary’s.
Na Mwandishi Wetu
MENEJA wa Shule za St. Mary’s, Muta Rwakatare, amesema mabadiliko ya mitaala ya elimu yanayoendelea nchini yanaifanya shule hiyo kujiandaa zaidi kukidhi mahitaji mapya ya wazazi, wanafunzi na taifa kwa ujumla.
Rwakatare ameyasema hayo leo Agosti 7, 2026 wakati wa ibada ya shukrani kufuatia kifo cha Mchungaji Getrude Rwakatale ambaye alikuwa mmiliki wa shule hizo amesema mtaala wa sasa umeelekezwa zaidi katika matumizi ya teknolojia za kidijitali na ujuzi wa kiufundi, hivyo St. Mary’s imejipanga kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu inayokwenda sambamba na mahitaji ya wakati.
“Ni kweli mtaala umebadilika. Sasa hivi uko kiufundi na kidijitali zaidi. Lakini kwa St. Mary’s tumejipanga kuhakikisha kwamba mtaala uliopo sasa, ambao umeletwa ukiwa mpya, unakidhi mahitaji ya wateja wetu ambao ni wazazi wetu,” amesema.
Amesema pamoja na masomo ya kitaaluma, shule hiyo itaendelea kuzingatia michezo, sanaa na tasnia mbalimbali katika malezi ya wanafunzi ili kukuza vipaji vyao na kuwaandaa kukabiliana na mahitaji ya jamii na taifa.
Aidha, ameiomba Serikali kuendelea kushirikiana na shule katika utekelezaji wa maboresho ya elimu, hususan katika eneo la teknolojia za kidijitali, akisema hatua hiyo itasaidia kurahisisha utoaji wa elimu na kuongeza ufanisi katika shule, ikiwamo binafsi.
“Kikubwa ni kwamba kwenye tasnia ya sasa tuko kidijitali zaidi. Kwa kutusaidia katika kuboresha mtaala huu, tunaamini elimu itakuwa nyepesi na nzuri zaidi kwa shule zote, hususan shule binafsi,” amesema.
Kwa upande wake, Mchungaji wa Makanisa ya Mlima wa Moto, Rose Mgeta, amesema mabadiliko ya mitaala yanahitaji jamii ya shule kujiandaa ipasavyo ili wanafunzi wapate elimu inayokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye.
Mgeta amesema Serikali inapaswa kuendelea kushirikiana na shule binafsi katika kuwezesha matumizi ya teknolojia katika elimu, huku akisisitiza umuhimu wa kuimarisha michezo, sayansi na masomo mengine yatakayowawezesha wanafunzi kuwa na ujuzi unaohitajika katika dunia ya sasa.
“Tunaiomba Serikali itusaidie katika hilo ili tujikite zaidi kwenye michezo na vilevile katika tasnia ya elimu kwa ujumla, lakini zaidi katika eneo la kidijitali. Tuwe na mtaala wa kidijitali zaidi, sayansi na masomo mengine yote ili tuweze kukidhi vigezo vya wazazi wetu,” amesema.
Licha ya hayo amesema shule hizo zinaendeleza misingi na tamaduni zilizoachwa na Askofu Mama, Getrude Rwakatare, huku akieleza kuwa uongozi wa sasa unaendelea kuthamini na kuendeleza kazi nzuri inayofanywa na viongozi wa Kanisa na taasisi za St. Mary’s, akiwamo Bishop Rose Mgeta.
“Kwa hiyo, kwa wazazi ambao bado hamjapata nafasi ya kuleta watoto wenu katika shule hizi, huu ni wakati sahihi na sehemu sahihi ya kuwapeleka watoto wenu kusoma katika shule za St. Mary’s,” amesema Mgeta
Amesema shule hizo zinaongozwa na wakurugenzi wenye hofu ya Mungu, maadili na upendo kwa watoto, jambo ambalo amesema ni muhimu katika kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunza na kukua.
Kwa mujibu wa Mgeta St. Mary’s inalenga kuhakikisha watoto wanapata elimu bora huku wakipewa malezi yanayowajenga kuwa na maadili mema na kuwawezesha kutumia vipaji vyao kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla.
Matukio mbalimbali katika picha.









No comments:
Post a Comment