
Na Mwandishi Wetu, Tanga
MWANAFUNZI wa Kidato cha Tatu katika Shule ya Ufundi Tanga, Neema Bundala, amesema mkondo wa Amali katika shule za sekondari unawajengea wanafunzi ujuzi unaowawezesha kujiajiri mara baada ya kumaliza masomo, huku wakisubiri matokeo ya mitihani ya Taifa.
Neema ameyasema hayo wakati akizungumza katika Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu inayoendelea katika Banda la Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, jijini Tanga
Amesema anasoma fani ya Ufundi wa Magari (Motor Vehicle Mechanics), ambapo mafunzo hayo yanamwezesha kupata ujuzi wa vitendo utakaomsaidia kuanza kujiajiri mara baada ya kuhitimu.
“Kwa mfano mimi nasoma Ufundi wa Magari, hivyo ninapohitimu nitakuwa na ujuzi wa kutengeneza magari na ninaweza kuanza kujiajiri na nikisoma Kidato cha Tano na cha Sita, nitakuwa nimeongeza umahiri na nikifika chuo nitakuwa mbobezi zaidi,” amesema Neema.
Amesema mkondo wa Amali ni muhimu kwa wanafunzi wa kike kwa kuwa unawapa fursa ya kujenga uwezo wa kujiajiri na pia kuajirika katika taasisi mbalimbali kutokana na kuwa na ujuzi unaohitajika katika soko la ajira.


No comments:
Post a Comment