JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


Naibu Waziri Aipongeza FCC kwa Kuimarisha Haki za Walaji na Biashara

Share This

Na Mwandishi Wetu, Dodoma
SERIKALI imewataka wakulima, wafugaji, wavuvi na wajasiriamali nchini kutumia elimu ya ushindani wa haki na ulinzi wa mlaji kama nyenzo ya kuongeza thamani ya bidhaa zao, kupanua masoko na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Hassan Chande, alipotembelea banda la Tume ya Ushindani (FCC) katika Maonesho ya 33 ya Kilimo ya Kimataifa ya Nane Nane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samwel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma.

Mhe. Chande amesema elimu inayotolewa na FCC imekuwa na mchango mkubwa katika kuwajengea uwezo wazalishaji na wafanyabiashara kuzalisha bidhaa zenye ubora wa kushindana katika soko la ndani na la kimataifa.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kujenga mazingira rafiki ya biashara yanayozingatia ushindani wa haki, fursa sawa kwa washiriki wa soko na ulinzi wa maslahi ya walaji.

"Msingi huo unachochea uwekezaji, huongeza tija katika uzalishaji na kuimarisha mchango wa sekta mbalimbali katika kukuza uchumi wa Taifa," amesema Chande.

Aidha, amewahimiza wakulima, wafugaji, wavuvi na wajasiriamali kutumia kikamilifu elimu inayotolewa na FCC kwa kuzingatia sheria za ushindani, kuepuka vitendo vinavyopotosha soko na kujikita katika uzalishaji wa bidhaa bora zinazokidhi mahitaji ya walaji.

Amesema hatua hiyo itaongeza thamani ya mazao, kuinua kipato cha wazalishaji na kufungua fursa zaidi za biashara ndani na nje ya nchi.

Naibu Waziri huyo pia ameipongeza FCC kwa kuendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali katika kutoa elimu kwa umma kuhusu haki za walaji na ushindani wa haki, akieleza kuwa juhudi hizo zinaimarisha mazingira ya biashara yenye uwazi na usawa kwa manufaa ya wazalishaji na watumiaji wa bidhaa na huduma.

Amesisitiza kuwa Maonesho ya Nane Nane yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwafikia wananchi moja kwa moja na kuwapa maarifa yatakayowawezesha kuongeza ubora wa mazao na bidhaa zao.

Aidha, ametoa rai kwa FCC kuendeleza kampeni za elimu katika maeneo mbalimbali nchini ili Watanzania wengi zaidi wanufaike na fursa zinazotokana na soko lenye ushindani wa haki na hivyo kuchangia kwa kiwango kikubwa maendeleo ya uchumi wa Taifa

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad