JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


GST YAWEKEZA UJUZI, TEKNOLOJIA KUBORESHA TAFITI ZA MADINI NCHINI

Share This

Mkurugenzi wa Utawala na Uendeshaji wa GST,  Neema  Mhagama akizungumza na waandishi wa habari  alipotembelea banda la GST katika Maonesho ya  Kilimo ya Kimatiafa Nane Nane yanayoendelea  kwenye Viwanja vya Dkt.John Samwel Malecela ,Nzuguni jijini Dodoma,
Na Mwandishi Wetu

TAASISI ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imesema inaendelea kuwekeza katika mafunzo na ushirikiano na taasisi mbalimbali za kitaifa na kimataifa, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuimarisha uwezo wa kitaalamu katika tafiti za jiosayansi na uchunguzi wa sampuli maabara.

Akizungumza wakati wa ziara katika Banda la GST kwenye Maonesho ya Kilimo ya Kimataifa Nane Nane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samwel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Utawala na Uendeshaji wa GST, Neema Mhagama, amesema taasisi hiyo imekuwa ikiwajengea uwezo watumishi wake kupitia mafunzo na ushirikiano wa kitaalamu na taasisi za ndani na nje ya nchi

Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha GST inaendelea kuendana na mabadiliko ya teknolojia na kutumia mbinu za kisasa katika kufanya tafiti za jiosayansi pamoja na uchunguzi wa sampuli mbalimbali za miamba na madini.


“Ushirikiano huu umeendelea kuimarisha uwezo wa wataalamu wetu kwa kubadilishana uzoefu na teknolojia, jambo ambalo linaongeza tija katika shughuli za taasisi na kuchangia maendeleo ya Sekta ya Madini nchini,” amesema Mhagama.
Kwa mujibu wa Mhagama, GST imekuwa ikishirikiana na taasisi mbalimbali za ndani, zikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), pamoja na taasisi za kimataifa kutoka Uingereza, Finland, Korea Kusini na pamoja na China.


Amesema kupitia mafunzo, programu za kubadilishana uzoefu na ushirikiano wa kitaalamu, wataalamu wa GST wameweza kupata maarifa na teknolojia mpya zinazochochea ubunifu na kuongeza ufanisi katika tafiti za jiosayansi

Ameongeza kuwa maarifa hayo yamekuwa na mchango katika kuboresha huduma zinazotolewa kwa wachimbaji, wawekezaji na wadau wengine wa Sekta ya Madini.

Aidha, Mhagama amewahimiza wadau wa Sekta ya Madini kutumia wataalamu wa GST katika shughuli zao za uchimbaji ili kupata taarifa sahihi kuhusu miamba, namna bora ya uchimbaji pamoja na uchukuaji na uchunguzi wa sampuli za miamba.

“Tunawahimiza wadau kutumia wataalamu wa GST ili kupata taarifa sahihi zitakazowawezesha kufanya uchimbaji wenye tija na kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza katika shughuli za uchimbaji,” amesema.

Vilevile, Mhagama amewaalika wananchi na wadau mbalimbali waliopo Dodoma na maeneo mengine nchini kutembelea Banda la GST katika Maonesho ya Nane Nane yanayoendelea jijini Dodoma, ili kupata elimu na kujifunza masuala mbalimbali yanayohusu jiolojia na madini.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad