Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imeibuka mshindi wa kwanza katika kundi la Taasisi za Udhibiti kutokana na utoaji bora wa elimu kwa wananchi katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) 2026.
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Meneja wa PPRA Kanda ya Pwani, Vicky Mollel, alisema ushindi huo ni heshima kubwa kwa mamlaka hiyo na umetokana na imani na ushirikiano mkubwa waliooneshwa na Watanzania waliotembelea banda la PPRA wakati wa maonesho hayo.
Alisema PPRA itaendelea kuboresha huduma zake ili kuhakikisha wananchi wanapata elimu na huduma za ununuzi wa umma kwa viwango vya juu, sambamba na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
"Ushindi huu ni heshima kwa PPRA na unatupa nguvu ya kuendelea kuwahudumia Watanzania kwa ufanisi zaidi. Tunaendelea kujizatiti kuhakikisha huduma zetu zinabaki kuwa bora wakati wote," alisema Mollel.
Alibainisha kuwa katika kipindi chote cha maonesho, wananchi wengi walifika kwenye banda la PPRA kupata elimu kuhusu mfumo wa kielektroniki wa ununuzi wa umma (NeST), huku idadi kubwa wakijisajili ili kushiriki katika zabuni na fursa mbalimbali za ununuzi wa umma.
Mollel alisema mwitikio huo unaonesha kuongezeka kwa uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kushiriki katika ununuzi wa umma kwa kutumia mifumo ya kidijitali, jambo linalochangia uwazi, ushindani na uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma.
Alisisitiza kuwa PPRA itaendelea kutoa elimu kwa wadau na wananchi nchini kote ili kuongeza ushiriki wa Watanzania katika fursa za ununuzi wa umma, huku ikihakikisha shughuli zote zinaendeshwa kwa kuzingatia sheria na taratibu zinazotawala sekta hiyo.



No comments:
Post a Comment