JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


FPRF Yasisitiza Dhamira ya Kuimarisha Uwekezaji wa Kustaafu Nchini.

Share This
-Yatangaza Kampeni ya Kitaifa Kuhusu Elimu ya Uwekezaji wa Kustaafu.

Mfuko mpya wa uwekezaji wa kustaafu wa Foresight Private Retirement Fund (FPRF) umesisitiza dhamira yake ya kuleta mapinduzi katika mfumo wa uwekezaji wa kustaafu nchini kwa kuwapa Watanzania fursa ya kujenga uhuru wa kifedha kupitia uwekezaji wa hiari, salama na unaosimamiwa kitaalamu, huku ikitangaza kuanza kwa kampeni kubwa ya kitaifa ya elimu ya fedha itakayowafikia wadau mbalimbali nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Afisa Mtendaji Mkuu wa CORE Securities Limited, wasimamizi wa FPRF, CPA George Fumbuka, alisema kampeni hiyo ni hatua inayofuata baada ya uzinduzi rasmi wa mfuko huo na inalenga kujenga uelewa mpana kuhusu umuhimu wa kuwekeza mapema kwa ajili ya maisha ya baada ya kustaafu.

Alisema FPRF imeanzishwa kama suluhisho la muda mrefu litakalowasaidia Watanzania kujenga utajiri endelevu, kupunguza utegemezi wanapostaafu na kuimarisha ustawi wa familia zao.

"Tunataka kuanzisha utamaduni mpya wa kifedha nchini. Kwa muda mrefu watu wamekuwa wakifikiria kustaafu pale wanapokaribia kuacha kazi. Sisi tunasema maandalizi ya maisha ya baada ya kustaafu yanapaswa kuanza mapema. Swali si kama utastaafu, bali utaishije baada ya kustaafu. Ndiyo maana tunawahamasisha Watanzania waanze kuwekeza leo ili waishi kwa uhuru kesho," alisema CPA Fumbuka.

Alisema kwa miongo kadhaa mifumo ya pensheni imeonekana zaidi kuwa ya watu walio katika ajira rasmi, hali iliyosababisha mamilioni ya Watanzania wanaofanya kazi katika sekta isiyo rasmi kukosa fursa ya kujenga akiba na uwekezaji wa muda mrefu kwa ajili ya maisha yao ya baadaye.

Kwa mujibu wa CPA Fumbuka, FPRF imekuja kuziba pengo hilo kwa kutoa jukwaa linalowakaribisha Watanzania wote bila kujali aina ya shughuli wanazofanya, wakiwemo waajiriwa wa sekta ya umma na binafsi, wafanyabiashara, wakulima, wavuvi, wajasiriamali, vikundi vya kijamii, SACCOS, kampuni na taasisi mbalimbali.

Alieleza kuwa kampeni ya elimu itafanyika kupitia warsha, semina, mikutano ya wadau na majukwaa mbalimbali ya elimu ya fedha, kwa lengo la kuwawezesha wananchi kuelewa misingi ya uwekezaji wa kustaafu, namna ya kujiunga na mfuko huo, faida za kuwekeza kwa muda mrefu pamoja na mbinu bora za kupanga maisha ya kifedha baada ya kustaafu.

"Mafanikio ya FPRF hayatapimwa kwa idadi ya wanachama pekee, bali kwa kiwango cha uelewa tutakachojenga kwa Watanzania kuhusu umuhimu wa kupanga maisha yao ya baadaye. Elimu ndiyo msingi wa mkakati wetu. Tutawafuata wananchi walipo na kuwapa maarifa yatakayowasaidia kufanya maamuzi sahihi ya kifedha," alisema.

CPA Fumbuka alisisitiza kuwa FPRF haijaanzishwa kuchukua nafasi ya mifuko ya hifadhi ya jamii iliyopo, bali kuikamilisha kwa kutoa fursa za ziada za uwekezaji zitakazoongeza uwezo wa wananchi kujenga kipato na utajiri wa muda mrefu baada ya kustaafu.

"Tofauti na mifuko mingine inayojikita zaidi kwenye michango ya lazima, FPRF imejengwa katika misingi ya uchaguzi wa hiari, unyumbufu wa uwekezaji na uhuru wa mwananchi kupanga mustakabali wake wa kifedha kulingana na malengo na uwezo wake," alifafanua.

Aliongeza kuwa moja ya sifa kuu za FPRF ni kumpa mwekezaji uhuru wa kuchagua namna ya kunufaika na uwekezaji wake baada ya kutimiza masharti ya mfuko.

"Mwekezaji anaweza kuchagua kupokea mafao yake kwa mkupuo, kwa malipo ya kila mwezi kama pensheni au kwa mchanganyiko wa njia hizo kulingana na mahitaji yake. Vilevile anaweza kuanza kwa kiwango anachomudu na kuongeza uwekezaji wake kadri uwezo wake wa kifedha unavyoongezeka," alisema.

Kwa upande wake, Meneja wa Mfuko wa FPRF, Bw. Richard Matekele, alisema mfuko huo umeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji tofauti ya wawekezaji kupitia mipango mitatu ya uwekezaji inayozingatia umri na malengo ya kifedha ya mwanachama inayofahamika kama Youngsters' Plan, Middle-Agers' Plan na Seniors' Plan

“Youngsters' Plan inalenga vijana walio chini ya miaka 35 kwa lengo la kukuza mtaji kwa kipindi kirefu, Middle-Agers' Plan imeundwa kwa watu wenye umri wa miaka 35 hadi 50 wanaohitaji uwiano kati ya ukuaji wa uwekezaji na usalama wa mtaji, huku Seniors' Plan ikiwalenga wawekezaji wenye zaidi ya miaka 50 kwa kuzingatia zaidi uhifadhi wa mtaji na upatikanaji wa mapato yenye uhakika.’’ Alitaja.

Bw. Matekele alibainisha kuwa wawekezaji wanaweza kuchangia kwa mkupuo au kwa michango ya kila mwezi kulingana na uwezo wao, huku fedha zao zikiwekezwa katika hisa, hati fungani, dhamana za Serikali na vyombo vingine vya masoko ya mitaji vinavyolenga kuongeza thamani ya uwekezaji kwa muda mrefu.

Akifafanua zaidi kuhusu kampeni hiyo, Bw Matekele alisema itawafikia waajiri, wafanyakazi, taasisi za elimu, vyama vya wafanyakazi, SACCOS, vikundi vya kijamii, wafanyabiashara, wajasiriamali, wakulima, wanawake na vijana ili kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kuwekeza mapema kwa ajili ya maisha ya baada ya kustaafu.

"Kila hatua unayoanza leo ni uwekezaji katika heshima yako, familia yako na uhuru wako wa kifedha kesho. Usisubiri ustaafu ndipo uanze kupanga maisha ya baadaye. Anza Leo – Wekeza Kustaafu, Ishi kwa Uhuru Kesho” alisisitiza.

Foresight Private Retirement Fund (FPRF) ni mfuko wa uwekezaji wa kustaafu uliopata idhini ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) na unasimamiwa na CORE Securities Limited, huku mali za mfuko zikihifadhiwa na NMB Bank PLC kama Mdhamini na Mlezi (Trustee/Custodian). Mfuko huo umeanzishwa kwa lengo la kupanua fursa za uwekezaji wa muda mrefu na kuwasaidia Watanzania kujenga ustawi wa kifedha na maisha yenye heshima baada ya kustaafu.


Mtendaji Mkuu wa CORE Securities Limited, wasimamizi wa Mfuko mpya wa uwekezaji wa kustaafu wa FPRF, CPA George Fumbuka (kulia) akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akizungumza kuhusu mapokeo ya wadau kwa mfuko huo sambamba na ujio wa kampeni ya kitaifa inayolenga kujenga uelewa mpana kuhusu umuhimu wa kuwekeza mapema kwa ajili ya maisha ya baada ya kustaafu. Mkutano huo umefanyika leo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Meneja wa Mfuko wa FPRF, Bw. Richard Matekele


Meneja wa Mfuko mpya wa uwekezaji wa kustaafu wa FPRF, Bw. Richard Matekele (kushoto) akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akizungumza kuhusu mapokeo ya wadau kwa mfuko huo sambamba na ujio wa kampeni ya kitaifa inayolenga kujenga uelewa mpana kuhusu umuhimu wa kuwekeza mapema kwa ajili ya maisha ya baada ya kustaafu. Mkutano huo umefanyika leo jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mtendaji Mkuu wa CORE Securities Limited, wasimamizi wa Mfuko mpya wa uwekezaji wa kustaafu wa FPRF, CPA George Fumbuka.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad