NIC Insurance wakiwa na Makombe ya Yanga kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Meneja Maudhui wa Yanga Priva Shayo akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana kuleta makombe ya Yanga ndani ya Banda la NIC Insurance kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Na Mwandishi Wetu
BANDA la NIC Insurance katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) limevutia mamia ya wananchi na mashabiki wa soka baada ya kupokea makombe yaliyotwaliwa na Klabu ya Young Africans SC (Yanga), yakionyeshwa kwa umma kama sehemu ya kuenzi mafanikio ya ushirikiano kati ya klabu hiyo na kampuni hiyo ya bima.
Makombe hayo yamefikishwa katika banda la NIC Insurance kutokana na kuwa mdhamini wa Yanga kwa misimu mitatu mfululizo, ambapo imekuwa ikitoa bima kwa wachezaji pamoja na kudhamini tuzo za wachezaji bora wa timu hiyo.
Akizungumza mara baada ya kuwasili kwa makombe hayo katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Sabasaba jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Uhusiano na Masoko wa NIC Insurance, Karim Meshaki, alisema kampuni hiyo inajivunia kuwa sehemu ya mafanikio ya Yanga kwa kipindi chote cha udhamini wake.
Alisema katika misimu yote mitatu ambayo NIC Insurance imeidhamini Yanga, klabu hiyo imeendelea kufanya vizuri na kutwaa mataji mbalimbali, jambo linaloonyesha mafanikio ya ushirikiano huo.
"Tunafurahia kuona wananchi wakipata nafasi ya kushuhudia makombe haya kwa karibu. Ushirikiano wetu na Yanga umeendelea kuzaa matunda, na mafanikio haya yanatupa nguvu ya kuendelea kuiunga mkono klabu hiyo," alisema Meshaki.
Kwa upande wake, Meneja wa Maudhui ya Dijiti wa Young Africans SC, Priva Shayo, alisema jukumu lao ni kuhakikisha makombe hayo yanawafikia wadhamini pamoja na mashabiki ili waweze kusherehekea mafanikio ya klabu hiyo.
Alisema ushirikiano kati ya Yanga na NIC Insurance umeendelea kuimarika na umechangia mafanikio ya timu ndani na nje ya uwanja.
Shayo alitoa ahadi kuwa katika msimu wa 2026/2027, Yanga inalenga kufanya makubwa zaidi na kurejea katika Maonesho ya Sabasaba ikiwa na makombe saba, ikiwa ni ishara ya mafanikio mapya ambayo klabu hiyo inakusudia kuyapata.
Uwepo wa makombe hayo katika banda la NIC Insurance umeendelea kuvutia idadi kubwa ya wageni wa maonesho, huku wengi wakitumia fursa hiyo kupiga picha na kujionea kwa karibu historia ya mafanikio ya mabingwa hao wa Tanzania
Mkurugenzi wa Uhusiano na Masoko wa NIC Insurance Karim Meshaki akizungumza na Waandishi wa habari kuhusiana na ujio wa makombe ya Yanga katika Banda la NIC Insurance kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere



No comments:
Post a Comment