
Na Mwandishi Wetu, Shelisheli
NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Hamad Chande (Mb.) ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 69 wa Shirika la Utalii Duniani Kamisheni ya Afrika uliofanyika mjini Mahe, Jamhuri ya Ushelisheli.
Mkutano huo ulifunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Ushelisheli, Mhe. Dkt. Patrick Herminie Julai 2, 2026 ukiwa na dhima ya "Kuimarisha Rasilimali Watu ili Kuchochea Ukuaji wa Utalii Barani Afrika.”
Pamoja na mambo mengine mkutano huo ulijadili hali ya Sekta ya Utalii Barani Afrika na Duniani kwa ujumla ikijumuisha mwenendo wa ukuaji wa watalii, changamoto na fursa zilizopo; pamoja na hatua zinazochukuliwa katika utekelezaji wa programu na mipango ya Shirika la Utalii la Umoja wa Mataifa (UN Tourism) katika ngazi ya Kimataifa na Kikanda; utalii endelevu; maendeleo ya rasilimali watu na elimu ya utalii; uwekezaji na ubunifu katika sekta; pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya nchi wanachama na wadau mbalimbali.
Kupitia Mkutano huo Mkurugenzi wa Shirika la Utalii Kanda ya Afrika Bi. Elcia Grandcourt aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mpango Kazi wa Afrika kwa kipindi cha Mwaka 2025/26 iliyosheheni shughuli zilizotekelezwa kwa kushirikiana na nchi wanachama na wadau mbalimbali, ikiwemo kuimarisha uwezo wa rasilimali watu, kukuza utalii endelevu, kuendeleza ubunifu na matumizi ya teknolojia, kuongeza uwekezaji na ushindani katika Sekta ya Utalii, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa Kikanda ili kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo jumuishi kupitia utalii.
Sambamba na taarifa hiyo Bi. Grandcourt, aliwasilisha matokeo ya Utafiti kuhusu Kukuza Upatikanaji wa Elimu ya Utalii na Maendeleo ya Rasilimali Watu Barani Afrika.
Aidha, nchi wanachama walijadili kwa kina kuhusiana na uwezeshaji wa usafiri ndani ya nchi za Afrika kuwa na muunganiko wa safari ya pamoja, kurahisisha upatikanaji wa Visa, sambamba na utoaji wa elimu na maendeleo ya rasilimali watu.








No comments:
Post a Comment