
Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
TANZANIA imepiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya usugu wa vimelea vya maradhi kwa dawa (AMR), kwa kupunguza matumizi holela ya dawa za antibiotiks kwa asilimia 88 na kupunguza vifo vinavyohusishwa na tatizo hilo kwa asilimia 14.
Hatua hiyp inatajwa kuwa mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya moja ya vitisho vikubwa vya afya vinavyoongezeka duniani.
Mafanikio hayo yametangazwaa leo Juni 3, 2026 Kongamano la 17 la Uwasilishaji wa Matokeo ya Tafiti za Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), ambapo wataalamu walionya kuwa maambukizi yanayosababishwa na vimelea sugu kwa dawa bado ni tishio kubwa kwa afya ya umma, usalama wa chakula na ukuaji wa uchumi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Uratibu wa Sekta Mbalimbali kuhusu Usugu wa Vimelea dhidi ya Dawa (MCC), Profesa Hezron Nonga, amesema mafanikio hayo yametokana na utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Kitaifa wa Kukabiliana na AMR wa mwaka 2023–2028, unaotumia mkakati wa Afya Moja (One Health) unaounganisha afya ya binadamu, wanyama na mazingira.
"Tanzania imepiga hatua kubwa kutoka kuwa na uwezo mdogo wa kukabiliana na AMR mwaka 2016 hadi kuwa na mifumo imara ya kukabiliana na tatizo hilo kufikia mwaka 2024," amesema Profesa Nonga.
Ameeleza kuwa nchi imeimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa, kuboresha ushirikishanaji wa taarifa, kuongeza fedha za ndani kwa ajili ya shughuli za AMR na kuendesha kampeni za uhamasishaji wa umma kuhusu matumizi sahihi ya antibiotiki.
Hata hivyo, Profesa Nonga ameonya kuwa usugu wa vimelea dhidi ya dawa bado ni changamoto kubwa inayohitaji juhudi endelevu.
"AMR inaweza kufuta mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya afya kwa miongo mingi. Ni muhimu kuendelea kuwekeza katika ufuatiliaji, tafiti na matumizi sahihi ya dawa za kuua vimelea ili kulinda ufanisi wa dawa zinazookoa maisha," amesema.
Duniani kote, AMR inahusishwa na takribani vifo milioni 4.71 kila mwaka, huku vifo milioni 1.14 vikisababishwa moja kwa moja na maambukizi ya bakteria sugu kwa dawa.
Tanzania pia imeongeza juhudi za kutoa elimu kwa umma kupitia kampeni ya "Holelaholela Itakukosti" pamoja na kuanzisha istilahi ya Kiswahili ya "Usugu wa Vimelea vya Magonjwa Dhidi ya Dawa (UVIDA)." Kampeni hiyo imewafikia karibu watu milioni 25 na kupata kutambuliwa na Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC).
Kwa mujibu wa Profesa Nonga, utekelezaji wa hatua za kudhibiti maambukizi katika vituo vya afya umeongezeka kwa asilimia 60. Aidha, maboresho katika chanjo za mifugo, usalama wa kibaiolojia na usalama wa chakula yamechangia kupunguza milipuko ya magonjwa na matumizi yasiyo ya lazima ya dawa kwa wanyama.
Mkuu wa Ushirikiano wa Ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Luc Blanco, alisema usugu wa vimelea dhidi ya dawa ni miongoni mwa vitisho vikubwa vya afya duniani na akasisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa.
"Mapambano dhidi ya AMR yanahitaji ushirikiano wa sekta mbalimbali na nchi mbalimbali. Tafiti, ufuatiliaji na kubadilishana taarifa ni mambo muhimu kwa mafanikio ya juhudi hizi," amesema.
Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS anayeshughulikia Mipango, Fedha na Utawala amesema vyuo vikuu vina nafasi muhimu katika kuzalisha ushahidi wa kisayansi unaosaidia kutunga sera na kuimarisha uwezo wa taifa wa kukabiliana na changamoto mpya za afya.
Kongamano hilo limewakutanisha watafiti, watunga sera, wataalamu wa afya na wadau wa maendeleo chini ya kaulimbiu: "Kuendeleza Mapambano dhidi ya AMR Tanzania: Taarifa za Mfumo wa Afya Moja kuhusu Mafanikio, Changamoto na Mwelekeo wa Baadaye."

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)


No comments:
Post a Comment