Na Mwandishi wetu.
FILAMU ya uchunguzi iliyotengenezwa na mwanahabari wa uchunguzi kutoka Nigeria anayeishi Ghana, David Hundeyin, imeibua mjadala mpana kuhusu nafasi ya vijana, wajibu wa vyombo vya habari na umuhimu wa kulinda amani na utulivu katika jamii za Afrika.
Akizungumza baada ya kuonyeshwa kwa filamu hiyo, Waziri wa zamani wa Afya Zanzibar na mwanasiasa mkongwe,Hamad Rashid amesema kazi hiyo imefungua macho kwa wananchi kuhusu namna matukio makubwa ya kijamii na kisiasa yanavyoweza kuathiriwa na nguvu za nje, huku akisisitiza umuhimu wa Waafrika kujenga uwezo wao wa kufanya tafiti na uchunguzi wa kina kuhusu masuala yanayowahusu.
Amesema pamoja na filamu hiyo kutoa mafunzo muhimu kwa jamii, kinachopaswa kufanyika sasa ni kutumia yaliyobainishwa kama somo la kujenga taifa lenye amani, umoja na maendeleo badala ya kuendeleza migawanyiko. Alisisitiza kuwa changamoto kubwa zinazowakabili wananchi ni ajira, afya, elimu na ustawi wa maisha, hivyo nguvu kubwa inapaswa kuelekezwa katika kutatua mahitaji hayo.
Kwa upande wake, mwanazuoni na mchambuzi wa masuala ya maendeleo kutoka Zimbabwe, Joshua Maponga, alisema tukio hilo limeonesha umuhimu wa vyombo vya habari vya ndani kuwa na uwezo wa kuripoti kwa kina masuala yanayotokea katika jamii zao ili kutoa taswira halisi kabla simulizi za nje hazijatawala mjadala.
Ameongeza kuwa vijana wanapaswa kuwa waangalifu dhidi ya ushawishi unaoweza kuwaingiza katika migogoro inayoweza kuhatarisha mustakabali wao na maendeleo ya nchi zao kwani nguvu za vijana zinapaswa kuelekezwa katika ubunifu, uzalishaji na kujenga uchumi badala ya kushiriki katika matukio yanayoweza kuhatarisha amani.
Akielezea sababu za kuandaa filamu hiyo, David Hundeyin amesema lengo kuu lilikuwa kuonesha namna ambavyo ushawishi wa nje unaweza kujitokeza katika jamii za Afrika kupitia njia mbalimbali, ikiwemo mitandao ya kijamii na mashirika yenye maslahi ya kisiasa au kiuchumi.
Amesema Waafrika wengi bado hawatambui kwa kiwango kikubwa namna masuala ya kimataifa yanavyoweza kuathiri maisha yao ya kila siku, hivyo aliona umuhimu wa kutumia tukio hilo kama mfano wa kufundisha jamii kuhusu mazingira mapana ya kisiasa na kijamii yanayoikabili Afrika ya sasa.
Naye Mhariri Mkuu wa Wasafi Media, David Rweikiza Ronyagira, amesema filamu hiyo imewakumbusha wanahabari umuhimu wa kutafuta chanzo cha matukio badala ya kuripoti matokeo pekee kwani wanahabari wana wajibu wa kufanya tafiti za kina ili kusaidia jamii kuelewa sababu za changamoto mbalimbali na namna ya kuzitatua.
Aidha Ronyagira, filamu hiyo imeonesha kuwa kila mwananchi ana nafasi katika kulinda amani ya taifa, kuanzia viongozi, wanahabari, wanaharakati hadi wananchi wa kawaida. Alisema kila kundi linapaswa kutimiza wajibu wake kwa uwajibikaji ili kuzuia migogoro inayoweza kuepukika.
Akizungumzia vijana, amesema wanahitaji kupewa nafasi za kushiriki katika maendeleo ya taifa na kusikilizwa kuhusu changamoto zinazowakabili. Alionya dhidi ya tabia ya kutumia hasira za vijana kwa maslahi ya watu wengine badala ya kuwasaidia kupata suluhisho la matatizo yao.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Said salim, amesema pamoja na filamu hiyo kuwa mwanzo mzuri wa mjadala, bado ina maeneo yanayohitaji maboresho ya kitaaluma ili kutoa taswira pana zaidi ya matukio na athari zake kwa wananchi wa kawaida.
Washiriki wa mjadala huo walikubaliana kuwa somo kubwa lililotokana na filamu hiyo ni umuhimu wa kuimarisha elimu ya uraia, kuwajengea vijana uwezo wa kufanya maamuzi sahihi, kuimarisha uwajibikaji wa taasisi mbalimbali na kuhakikisha vyombo vya habari vinatimiza wajibu wake wa kuelimisha na kuhabarisha jamii kwa usahihi.
Wamesisitiza kuwa maendeleo ya taifa lolote hayawezi kupatikana bila amani, umoja na ushirikiano wa wananchi wake, huku wakitaka nguvu zaidi kuelekezwa katika kutatua changamoto za ajira, elimu na maisha bora kwa vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya sasa na ya baadaye.


.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)


No comments:
Post a Comment