JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


Shehena ya Vipodozi Vyenye Sumu Yakamatwa Chimala Mbeya, Watuhumiwa Wawili Mbaroni

Share This

 







Na Mwandishi Wetu, Mbeya
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kushirikiana na wananchi na wadau mbalimbali katika kuimarisha ulinzi na usalama wa maisha na mali kupitia doria, misako na oparesheni za kuzuia na kubaini uhalifu. Katika kipindi cha mwezi Mei 2026, jumla ya watuhumiwa 871 wa makosa mbalimbali ya jinai walikamatwa katika maeneo tofauti ya mkoa huo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, makosa yaliyohusika ni pamoja na mauaji, kujeruhi, ubakaji, kupatikana na silaha bila kibali, dawa za kulevya pamoja na wizi. Watuhumiwa waliokamilishiwa upelelezi walifikishwa mahakamani, ambapo baadhi yao wamekutikana na hatia na kuhukumiwa vifungo mbalimbali kwa mujibu wa sheria.

Katika matukio ya hivi karibuni, Polisi wanawashikilia watuhumiwa wawili, Baraka Mwakatobe (31) na Said Baraka (39) wakazi wa Dodoma, kwa tuhuma za kusafirisha vipodozi vyenye viambata sumu vilivyopigwa marufuku nchini. Watuhumiwa hao walikamatwa Mei 28, 2026 katika kizuizi cha Polisi Chimala wakiwa na shehena ya boksi 403 za vipodozi hivyo pamoja na bidhaa nyingine zisizo rasmi.

Aidha, Jeshi hilo linamshikilia Shaban Safari (48) mkazi wa Kyela kwa tuhuma za kupatikana na dawa za kulevya aina ya heroin kete 27 pamoja na bangi. Inadaiwa mtuhumiwa huyo alikamatwa akiwa na dawa hizo zilizofichwa kwenye mfuko wa khaki, huku akituhumiwa kuwa muuzaji wa dawa hizo katika eneo hilo.

Kwa kipindi hicho hicho cha Mei 2026, Polisi wamesema pia waliwakamata watuhumiwa 20 wakiwa na bangi kilo 12.24, watuhumiwa wawili wakiwa na gongo lita 30 na wengine wawili wakiwa na silaha aina ya gobole, hatua inayoonesha kuendelea kudhibiti uhalifu na vitendo vya kihalifu mkoani humo. Aidha, kesi 224 zilifikishwa mahakamani ambapo 122 zilimalizika kwa hukumu za hatia na 73 bado zinaendelea.

Jeshi la Polisi limehimiza wananchi kuendelea kushirikiana kwa kutoa taarifa za uhalifu na kufika mahakamani kutoa ushahidi ili kusaidia haki kutendeka. Pia limetoa onyo kwa watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu kuacha mara moja, likisisitiza kuwa uhalifu haulipi na hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wote watakaobainika.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad