Na Mwandishi Wetu, Arusha
MKURUGENZI wa Mauzo wa Turaco Collection Tanzania, Florenso Kirambata, amesema kuwa maonesho ya Karibu-KiliFAIR 2026 ni jukwaa muhimu la kuitangaza Tanzania kimataifa, kubadilishana uzoefu na kujenga ushirikiano wa kibiashara katika sekta ya utalii inayokua kwa kasi duniani.
Akizungumza wakati akiwasilisha hoteli za Turaco Collection katika maonesho hayo yanayofanyika jijini Arusha, Florenso alisema tukio hilo linawakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya utalii, ukarimu, safari na uwekezaji kutoka Tanzania na mataifa mengine duniani.
Maonesho ya Karibu-KiliFAIR 2026 yanafanyika kuanzia Juni 4 hadi 7, 2026 katika Viwanja vya Magereza, Arusha.
Florenso alisema Turaco Collection imeendelea kuimarisha uwepo wake nchini kupitia hoteli zake katika maeneo mbalimbali. Dar es Salaam kuna Element by Westin Dar es Salaam na Delta Hotels by Marriott Dar es Salaam, huku Kaskazini mwa Tanzania kukiwa na Turaco Ngorongoro Valley Lodge, Tribute Portfolio na Turaco Manyara View Lodge, Tribute Portfolio. Zanzibar, kampuni inamiliki Turaco Nungwi Resort, Tribute Portfolio, Turaco Spice Tree Stone Town, Tribute Portfolio pamoja na Beyt Al Salaam by Turaco.
Alieleza kuwa hoteli zote za Turaco Collection zinazobeba chapa za kimataifa zinaendeshwa kwa kuzingatia viwango vya Marriott International, jambo linalochangia kuimarisha ubora wa huduma, matumizi ya teknolojia za kisasa na utoaji wa uzoefu wa kiwango cha kimataifa kwa wageni wanaotembelea Tanzania.
Akizungumzia matumizi ya Akili Bandia (AI) katika sekta ya ukarimu, Florenso alisema Marriott International inaamini teknolojia hiyo inapaswa kuboresha uzoefu wa wageni kwa kuufanya kuwa wa kibinafsi zaidi, wenye ufanisi mkubwa na rahisi, huku ikidumisha misingi ya ukarimu unaozingatia mahusiano ya kibinadamu.
Alisema kampuni hiyo inaendelea kuwekeza katika teknolojia za AI ili kuboresha mifumo ya uwekaji nafasi za malazi, shughuli za uendeshaji wa hoteli, programu za uaminifu kwa wateja na huduma mbalimbali za wageni.
“Teknolojia haitachukua nafasi ya ukarimu wa kibinadamu, bali itaongeza uwezo wa wafanyakazi wetu kutoa huduma bora zaidi. Mwelekeo wa Marriott International ni kutumia AI kuifanya safari ya mgeni, kuanzia kupanga safari, kuweka nafasi, kuwasili hotelini hadi kuondoka, kuwa rahisi, ya haraka na yenye uzoefu wa kipekee,” alisema Florenso.
Aliongeza kuwa kupitia ushirikiano wake na Marriott International, Turaco Collection inaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya teknolojia katika sekta ya ukarimu ili kuhakikisha wageni wanaotembelea Tanzania wanapata huduma zinazokidhi viwango vya kisasa vya kimataifa.

.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)



No comments:
Post a Comment