
DAR ES SALAAM:
MDAU na mwekezaji katika sekta ya kilimo, Malebo Lucas wa kampuni ya Malebo Farm, ameishauri Serikali kupitia Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP-CENTRE) pamoja na Wizara ya Maji kubadili mbinu na kuanza kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na wafanyabiashara ili kubaini changamoto zinazowazuia kushiriki katika miradi ya ubia.
Malebo alitoa ushauri huo wakati akichangia mada katika Kongamano la Kitaifa kuhusu Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) katika Sekta ya Maji lililofanyika jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kwenye kongamano hilo, Malebo alisema licha ya kuwepo kwa fursa nyingi zinazowasilishwa kwenye mikutano na makongamano mbalimbali, bado mwitikio wa wafanyabiashara wa ndani kuwekeza katika miradi ya PPP ni mdogo, jambo linaloashiria kuwa kuna changamoto zinazohitaji kusikilizwa na kutafutiwa ufumbuzi wa moja kwa moja.
Aliitaka PPP-CENTRE pamoja na Wizara ya Maji kukaa meza moja na wawekezaji na wafanyabiashara wa ndani ili kupata maoni yao kuhusu mazingira ya uwekezaji, urasimu, gharama za kuanzisha miradi pamoja na changamoto za upatikanaji wa mitaji.


No comments:
Post a Comment