JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


SERIKALI YAPANGA MABORESHO YA MFUMO WA STAKABADHI GHALANI

Share This

 


︎ Dkt. Mwigulu asema maghala yawafuate wakulima badala ya wakulima kufuata maghala
︎ Serikali kuitisha kikao maalumu cha mikoa inayozalisha mazao ya biashara


WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali inapanga kufanya maboresho katika mfumo wa stakabadhi ghalani ili kuondoa changamoto zinazowakabili wakulima hususan gharama na usumbufu wa kufuata huduma za maghala yaliyo mbali na maeneo yao ya uzalishaji.

Amesema hayo leo Jumamosi, Mei 16, 2026 wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Mnenia, Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma katika mwendelezo wa ziara yake ya kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi.

Waziri Mkuu amesema Serikali imepokea malalamiko mbalimbali kuhusu utekelezaji wa mfumo huo na kwamba hatua zinaendelea kuchukuliwa ili kuhakikisha mfumo huo unawanufaisha wakulima kama ilivyokusudiwa.

“Maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ni wananchi wasiyafuate maghala, maghala yawafuate wananchi pale walipo,” amesema.

Aidha, Waziri Mkuu amesema ataitisha kikao maalumu kitakachowahusisha wakuu wa mikoa pamoja na sekta zinazohusika kutoka maeneo yanayozalisha mazao yanayotumia mfumo wa stakabadhi ghalani ili kufanya tathmini ya changamoto zilizopo na namna ya kuzitatua.

“Nitaitisha kikao cha wakuu wa mikoa ya maeneo haya yanayozalisha mazao ambayo wananchi wake wamekuwa wakipata changamoto ili tupate mpango kazi wa namna ya kumaliza tatizo hili,” amesema.

Ametaja baadhi ya mikoa inayohusika kuwa ni Dodoma, Singida, Simiyu, Tabora pamoja na baadhi ya mikoa ya Kusini inayozalisha mazao ya biashara ikiwemo ufuta na dengu.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali imeelekeza wanunuzi wa mazao kutumia taasisi za kifedha kupata mikopo badala ya kuwakopesha wakulima kabla ya mauzo ya mazao yao.

“Wenzetu wanaokwenda kununua haya mazao wasiwakope wakulima, wao wakakope benki. Benki ndiyo taasisi zinazotoa mikopo,” amesema.

Amesema Serikali itaendelea kufuatilia utekelezaji wa mfumo huo ili kuhakikisha wakulima wanapata huduma kwa urahisi na kunufaika ipasavyo na mazao yao.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad