Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati akizindua kituo cha Kijitonyama FTTx Experience Centre Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL,) David Nchimbi amesema kituo hicho cha ubunifu wa matumizi ya teknolojia ni cha kipekee na kinachotoa uzoefu wa pamoja na elimu kuhusu matumizi ya teknolojia za kidigitali ambapo kupitia kituo hicho wananchi watapa fursa ya kuona kwa vitendo namna ambavyo intaneti ya TTCL inavyoweza kubadilisha nyumba, ofisi au biashara kwa za kidigitali na zenye ufanisi.
Amesema kituo hicho kitakuwa jukwaa la kujifunza na kubadilisha uzoefu kuhusu matumizi teknolojia za kisasa nyumbani, mifumo ya ofisi za kidigitali, na suluhisho katika biashara za mtandaoni pamoja na kuchochea na kujenga uelewa kwa jamii juu ya umuhimu wa TEHAMA katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Nchimbi amesema,ubunifu unaoendelea kufanywa na Shirika hilo ni katika kuhakikisha wateja wanapata huduma bora kwa wakati na uhakika na zenye kurahisisha shughuli mbalimbali ikiwemo mtandao, biashara mtandao, huduma za kifedha na mawasilino yenye tija.
Amesema, Serikali itaendelea kuhakikisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano nchini zinapewa kipaumbele na hiyo ni pamoja na kuongeza ubunifu na wigo wa utoaji huduma wa Shirika hilo kwa wananchi, kuongeza ufanisi, mapato na kujiendesha kibiashara ili kuendelea kuwahudumia wananchi kwa ubora zaidi,
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Moremi Marwa amesema kuwa, Shirika linatekeleza Mpango Mkakati wa miaka 10 ulioanza katika mwaka wa fedha wa 2025/ 2026 kwa lengo la kuleta mageuzi katika uwajibikaji, kuongeza uzalishaji wenye tija na kufanya uendelevu katika miradi waliyoianzisha.
“Pamoja na mageuzi mengineyo mradi huu wa ´Faiba ´Fiber to The X´( FTTx) ambao umelenga kusambaza huduma ya intaneti yenye kasi , uhakika na ubora katika makazi, ofisi na maeneo ya biashara na kupitia huduma ya ´Faiba Mlangoni Kwako´shirika linaendelea kutoa huduma katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Dar es Salaam, Unguja, Arusha, Dodoma, Mwanza, Geita, Iringa na Mbeya na kwa mwaka 2026/27 Shirika limejipanga kufikisha huduma hii ya Faiba katika mikoa iliyobaki.” Amesema.
Akieleza kuhusu FTTX Experience Centre, Marwa amesema kituo hicho ni mwendelezo wa ubunifu katika utoaji huduma za intaneti nchini ambapo kwa sasa wateja wanapata huduma za inataneti zilizounganishwa, ambapo mteja anaweza kupata huduma tatu katika kifurushi kimoja yaani intaneti bila kikomo akiwa nyumbani, dakika anazoweza kuzitumia katika simu ya mkononi au mezani pamoja na GB za intaneti katika simu ya mkononi.
Amefafanua kuwa kupitia kituo hicho wateja watapata fursa ya kuona matumizi ya kidigitali kwenye smart home, uwekaji wa huduma ya intaneti ya Faiba majumbani, ofisini na maeneo ya biashara pamoja na teknolojia inayotumika katika utoaji wa huduma hizo.
Kuhusiana na faida kwa Shirika hilo Marwa amesema kwa mwaka wa fedha 2024/25 lilipata faida ya Shilingi Bilioni 22.9 kabla ya kodi na ni faida ambayo imethibitishwa na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG,) na wamejipanga zaidi katika kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wateja pamoja na kuliendesha Shirika hilo kibiashara na kuwashukuru wadau wao kutoka kampuni za Hisence na Huawei kwa ushirikiano wao katika ujenzi wa kituo hicho.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL,) Moremi Marwa akizungumza wakati wa uzinduzi huo na kueleza kuwa kupitia kituo hicho wananchi watapata fursa ya kuona kwa vitendo namna TTCL inavyotumia teknolojia katika utoaji wa huduma. Leo jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL,) David Nchimbi akizungumza mara baada ya kuzindua kituo hicho na kueleza kuwa upekee na ubunifu wa kituo hicho ni jukwaa la kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu matumizi ya teknolojia. Leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Biashara wa TTCL Vedastus Mwita akieleza namna TTCL inavyotumia teknolojia katika utoaji huduma. Leo jijini Dar es Salaam.








No comments:
Post a Comment