
Dar es Salaam, Tanzania – Aprili 15, 2026
Punchline Africa imetangaza rasmi uzinduzi wa Tamasha la Kimataifa la Vichekesho la Punchline (PICF) 2026, litakalofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Mei 25 hadi Juni 1, 2026.
Tamasha hilo la wiki moja linatarajiwa kuwakutanisha wachekeshaji kutoka nchi mbalimbali za Afrika, likijumuisha maonesho ya moja kwa moja, shughuli za vyombo vya habari pamoja na ubadilishanaji wa utamaduni. Tamasha litahitimishwa kwa onesho kubwa la fainali litakalofanyika katika ukumbi wa Superdome.
PICF 2026 itajumuisha maonesho ya vichekesho kwa lugha ya Kiingereza na Kiswahili, ikiwa ni juhudi za kuonesha utofauti na utajiri wa vipaji vya ucheshi barani Afrika.
Mbali na burudani, waandaaji wamesema tamasha hilo pia linalenga kuhamasisha ustawi wa afya ya akili kwa kuonesha umuhimu wa kicheko kama nyenzo ya kupunguza msongo wa mawazo na kuimarisha mshikamano wa kijamii.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mwanzilishi Mwenza wa Punchline Africa, Evans Bukuku, alisema ucheshi una mchango mkubwa zaidi ya burudani.
“Comedy siyo kuchekesha tu, bali ni njia ya kuwasaidia watu kuelewa maisha, kupunguza msongo wa mawazo na kuunganishwa kijamii. Kupitia PICF tunataka kuunda jukwaa la watu kukutana, kucheka na kuondoka wakiwa na nafuu zaidi,” alisema.
Kwa upande wake, Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Anne Sophie Ave, alisema wameamua kuunga mkono tamasha hilo kutokana na imani yao katika nguvu ya sanaa ya ubunifu, hasa kwa vijana.
“Vijana wengi wana vipaji vikubwa lakini hukosa kujiamini kujitokeza. Tunaamini tamasha hili litawasaidia kupata ujasiri na kufikia fursa za kimataifa,” alisema.
Aliongeza kuwa Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji kutokana na nafasi yake kama kitovu cha Afrika Mashariki pamoja na historia yake katika harakati za Pan-Afrika.
Naye Mkurugenzi wa Maendeleo ya Filamu kutoka Tanzania Film Board, Emmanuel Ndumukwa, alilipongeza tamasha hilo akieleza kuwa ni hatua muhimu kwa ukuaji wa tasnia ya ucheshi nchini.
Alisema serikali ipo tayari kuunga mkono jitihada kama hizo kupitia mifuko ya utamaduni huku akisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa vigezo vya wazi kwa washiriki
Akizungumza kwa niaba ya wachekeshaji wa Tanzania, Humphrey Richard maarufu kama MC Kisoli, alisema tamasha hilo lina uwezo wa kubadilisha maisha ya wasanii wengi.
“Hili ni zaidi ya burudani; ni jukwaa la kujifunza, kubadilishana uzoefu na kukuza sanaa ya ucheshi. Ni tamasha la kila mtu,” alisema.
Tamasha hilo pia ni sehemu ya mradi wa Création Africa unaofadhiliwa na Ubalozi wa Ufaransa na kuratibiwa na Alliance Française Dar es Salaam, unaolenga kuwawezesha wasanii na taasisi za ubunifu nchini.
Uzinduzi rasmi ulifanyika kupitia mkutano na waandishi wa habari katika Punchline Comedy Club, Masaki, ukihudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo SGA Security ambao watatoa huduma za ulinzi katika matukio yote ya tamasha.
Waandaaji wanatarajia tamasha hilo kuvutia hadhira kubwa, hususan vijana na wabunifu, pamoja na kuwafikia zaidi ya watu milioni moja kupitia majukwaa ya kidijitali.
Ratiba kamili ya matukio, majina ya wasanii pamoja na taarifa za tiketi zinatarajiwa kutolewa hivi karibuni.
.jpeg)


No comments:
Post a Comment